Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mafunzo ya ILO yamuinua aliyekosa ajira baada ya kuhitimu Chuo Kikuu

Hawa Sindika, Afisa Mtendaji Mkuu na muasisi wa Plenus, kampuni ya kutengeza mafuta ya nazi akihojiwa na Mary Kabora wa UNIC, Dar es salaam nchini Tanzania.
UN/ Tanzania
Hawa Sindika, Afisa Mtendaji Mkuu na muasisi wa Plenus, kampuni ya kutengeza mafuta ya nazi akihojiwa na Mary Kabora wa UNIC, Dar es salaam nchini Tanzania.

Mafunzo ya ILO yamuinua aliyekosa ajira baada ya kuhitimu Chuo Kikuu

Ukuaji wa Kiuchumi

Kukosa ajira kwa muda mrefu na majukumu ya kuhudumia familia ni mambo yaliyosababisha Hawa Sindika, mjasiriamali kutoka Tanzania kusaka ujuzi wa kutengeneza mafuta asili ya nazi na sasa ni miongoni mwa wanaosongesha malengo ya Umoja wa Mataifa ya maendeleo endelevu, SDGs  ikiwemo lile la kutokomeza umaskini. 

Bi. Sindika ambaye amefungua kiwanda kiitwacho Plenus ambacho huzalisha mafuta asili ya nazi ya mgando na kujipatia kipato tangu aanzishe kiwanda hicho mwaka 2019. 

Anaendesha shughuli zake kwenye eneo la Sinza, jijini Dar es salaam nchini Tanzania. Alihitimu elimu ya elimu ya juu katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustine mkoani Mwanza nchini Tanzania mwaka 2015 na kutunukiwa shahada ya Biashara. 

Mafunzo alipatiwa wapi? 

Mafunzo ya wiki mbili alipata Hawa Sindika kupitia programu ya Start and Improve Your Business au  Anza na Boresha Biashara Yako kupitia shirika la Umoja wa Mataifa la kazi duniani, ILO

Halikadhalika a mafunzo mengine ya wiki mbili ya usindikaji wa chakula yaliyotolewa na Shirika la maendeleo ya viwanda vidogo vidogo nchini Tanzaina, SIDO  pamoja na mafunzo ya stadi za maisha na ujasiriamali kutoka shirika la Youth Foundation aliyopata kwa muda wa mwezi mmoja. 

Uzalishaji wa mafuta ya nazi hufanyika vipi? 

Meneja uzalishaji katika Plenus, Gachuli John ameeleza kwa kina hatua za utengenezaji wa mafuta asili ya nazi ambazo huanzia kwenye ununuzi wa nazi, nazi kupasuliwa na kukaushwa kwa siku mbili. Hatua inayofuata ni kutenganisha nyama za nazi na magome ya nazi. Baada ya kukauka vipande vya nazi kuingizwa kwenye mashine na mashine inafanya kazi ya kukamua nazi na kupata mafuta yenye mchanganyiko wa vumbi au rangi ya nazi. 

Hatua ya mwisho mafuta huchunjwa kwa kutumia pamba au kitambaa na kupakia katika vichupa kwa ajili ya kuuza na wateja kutumia.  

Soko la Plenus ni wapi? 

Bi. Sindika anasema wateja wake ni ndani na nje ya Tanzania, “tunamshukuru Mungu kupitia bidhaa hizi tunapata wateja wengi kila kona na kila nyanja tunasafirisha nje ya nchi sehemu kama Kenya, Uganda, Sweden na mikoani mafuta yetu yamefika.” 

Changamoto hazikosekani 

Safari ya ujasiriamali ya Hawa Sindika, haikosi changamoto akisema, “ninazitumia kama fursa ya kukuza biashara yangu. Mteja aliagiza mzigo lakini kwenye malipo ikawa tabu, nikaamua kubadili jinsi ya kunilipa ikawa mteja akitaka mzigo analipa kwanza nusu nikimpelekea anamaliza nusu iliyobaki,” alisema Bi. Sindika. 

Changamoto nyingine ni baadhi ya wateja kutoamini kile wanachoona mtandaoni hadi washike au waone kwa macho yao bidhaa husika, hivyo analazimika kutoa elimu zaidi. 

Plenus ni fursa ya ajira 

Kiwanda cha Plenus kimeajiri wafanyakazi 10. Miongoni mwao ni John Mathew ambaye ni Mhasibu. Amefanya kazi kwa miaka mitatu  sasa na kupata mafanikio mengi kupitia kazi yake. 

“Nimeweza kusomesha ndugu zangu, nimejiendeleza kielimu, nimepata usafiri na nimejenga nyumba.” 

Ujumbe wa Bi. Sindika kwa wasichana na wanawake 

“Ujumbe wangu kwa wasichana na wanawake walioko majumbani,  wasipende kukaa nyumbani, watoke nje, waende kujifunza kwa wanawake wengine na kuangalia wanafanya nini,” anasema Bi. Sindika na kumalizia ujumbe wake kuwa, “wachukue kitu ambacho wataweza kufanya na kuingiza kipato ambacho kitawasaidia wao na familia zao.”