Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mwanaharakati wa Cameroon Cécile Ndjebet aibuka kidedea tuzo ya 2022 ya Wangari Maathai  

Mwanaharakati Cécile Ndjebet ni mshindi wa tuzo ya mabingwa wa misitu ya Wangari Maathai kwa mwaka huu 2022
© FAO/Pilar Valbuena
Mwanaharakati Cécile Ndjebet ni mshindi wa tuzo ya mabingwa wa misitu ya Wangari Maathai kwa mwaka huu 2022

Mwanaharakati wa Cameroon Cécile Ndjebet aibuka kidedea tuzo ya 2022 ya Wangari Maathai  

Tabianchi na mazingira

Mwanaharakati Cécile Ndjebet, kutoka nchini Cameroon, leo ameshinda tuzo ya mabingwa wa misitu ya Wangari Maathai kwa mwaka huu 2022 (Wangari Maathai Forest Champions Award)  kwa kutambua mchango wake bora katika kuhifadhi misitu na kuboresha maisha ya watu wanaoitegemea. 

Tuzo hiyo imetolewa na ushirikiano wa Misitu (CPF), ambao unaongozwa na shirika la Umoja wa Mataifa la chakula na kilimo (FAO), na imekabidhiwa leo katika sherehe maalum wakati wa kongamano la XV la misitu la dunia linalofanyika huko Seoul, Jamhuri ya Korea. 

Naibu mkurugenzi mkuu wa FAO na mwenyekiti wa CPF Maria Helena Semedo akikabidhi tuzo hiyo amesema "Tuzo hii inaadhimisha nishati na kujitolea kwa Cécile Ndjebet kwa kipindi cha miongo mitatu katika kukuza haki za wanawake kwa suala la ardhi na misitu. Ameonyesha kikamilifu kwamba ushiriki wa wanawake katika utawala na uhifadhi wa misitu ni jambo la msingi katika kufikia usimamizi endelevu wa misitu.” 

Kuchagiza usawa wa kijinsia  

Kwa mujibu wa FAO takriban asilimia 70 ya wanawake nchini Cameroon wanaishi vijijini na wanategemea angalau kwa kiasi fulani kuvuna mazao ya misitu ya mwituni kwa ajili ya kuendesha maisha yao, lakini katika baadhi ya jamii wanawake wananyimwa haki ya kumiliki ardhi ya misitu, kurithi ikiwa mume wao amefariki au hata kupanda miti kwenye ardhi iliyoharibiwa. 

“Ndjebet ameendeleza bila kuchoka dhana kwamba wanawake wanapaswa kushirikishwa katika usimamizi wa misitu na kuwa na haki sawa kwa ardhi na rasilimali za misitu na kwamba wanapofanya hivyo, misitu inahifadhiwa vyema na jamii nzima kunufaika.” Ameongeza afisa huyo wa FAO 

Kupitia “Mtandao wa Wanawake wa Kiafrika kwa ajili ya usimamizi wa jamii wa Misitu,” ambao aliuanzisha mwaka 2009, Ndjebet amekuwa sauti inayoongoza, nchini Cameroon na kimataifa, katika kuchagiza utambuzi wa kimataifa juu ya umuhimu wa usawa wa kijinsia katika usimamizi wa misitu.  

Shirika hilo sasa lina nchi wanachama 20 kote barani Afrika. 

Akipokea tuzo hiyo Ndjebet amesema. "Wanaume kwa ujumla wanatambua jukumu kubwa la wanawake katika kuboresha viwango vya maisha ya familia. Lakini ni muhimu kwao pia kutambua kwamba ili wanawake waendelee kutekeleza jukumu hilo, na hata kuboresha jukumu hilo, wanahitaji upatikanaji salama na sawa wa ardhi na misitu." 

Kwa muda mrefu Ndjebet amekuwa msukumo katika kutekeleza sheria ya misitu na utawala bora nchini Cameroon na kuanzisha mbinu mpya kuhusu misitu ya jamii na kurejesha ardhi na misitu iliyoharibiwa kupitia mkakati wa ikolojia ya Cameroon (Cam-Eco), ambao aliuanzisha mwaka wa 2001.  

Cam-Eco imefanya kazi ya kufahamisha, kutoa mafunzo na kusaidia wanawake kuelewa masuala endelevu na kushiriki katika uhifadhi na urejeshaji wa misitu. 

Tuzo ya Wangari Maathai 

Tuzo hii ilianzishwa na CPF mwaka wa 2012 kwa kumbukumbu ya mwanamazingira wa Kenya na mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel Wangari Maathai, Tuzo hii ya Mabingwa wa Misitu inawatambua watu wenye hamasa ambao wamesaidia kuhifadhi, kurejesha na kusimamia misitu kwa njia endelevu. 

Mshindi wa tuzo ya mwaka huu alikutana na Wangari Maathai mwaka wa 2009, na mwanamazingira huyo alimtia moyo Ndjebet katika kazi yake ya kusaidia wanawake wanaopanda miti. 

Miongoni mwa washindi waliotangulia wa Tuzo ya Bingwa wa Msitu ya Wangari Maathai ni kiongozi wa vuguvugu la jamii ya misitu wa Nepal Narayan Kaji Shrestha (2012), mwanaharakati wa mazingira wa Mexico Martha Isabel 'Pati' Ruiz Corzo (2014), mwanaharakati wa misitu kutoka Uganda Gertrude Kabusimbi Kenyangi (2015), mwanaharakati wa misitu wa Brazili Maria Margarida Ribeiro da Silva (2017), na mwanaharakati wa misitu wa Burundi Léonidas Nzigiyimpa (2019). 

CPF inajumuisha mashirika 15 ya kimataifa yanayofanya kazi pamoja ili kukuza usimamizi endelevu wa aina zote za misitu na kuimarisha dhamira ya muda mrefu ya kisiasa kwa lengo hili.