Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Jukumu la wakunga ni zaidi ya kusaidia mjamzito kujifungua- UNFPA 

Mkunga akitembelea mama mjamzito nyumbani kwa ajili ya ufuatiliaji wakati wa uja uzito.
© UNICEF/Srikanth Kolari
Mkunga akitembelea mama mjamzito nyumbani kwa ajili ya ufuatiliaji wakati wa uja uzito.

Jukumu la wakunga ni zaidi ya kusaidia mjamzito kujifungua- UNFPA 

Afya

Hii leo ikiwa ni siku ya kimataifa ya wakunga duniani, shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu, UNFPA linamulika miaka 100 ya mafanikio ya shirikisho la kimataifa la wakunga, ICM. 

UNFPA katika wavuti wake inasema kuwa ICM ilianza kama Chama cha kimataifa cha wakunga huko Ubelgiji miaka 100 iliyopita imekuwa na mafanikio makubwa katika kuimarisha stadi za wakunga ambao majukumu yao ni zaidi ya kusaidia wajawazito pale wanapojifungua. 

Tangu mwaka 2008 ICM yenye wanachama zaidi ya milioni 1 duniani kote, ilipoanzisha Programu ya Kimataifa ya Ukunga, kupitia msaada wa UNFPA, wakunga katika nchi zaidi ya 120 wamepatiwa mafunzo na usaidizi. 

“Tumeshuhudia wakifanya majukummu yao kwenye mazingira yenye mabadiliko ya tabianchi, kuanzia kusaidia wajawazito kujifungua salama umeme ukiwa unakatikakatika hadi kwenye hospitali zilizofurika maji huko Bangladesh bila kusahau chini ya daraja baada ya kimbunga huko Honduras na matetemeko ya ardhi Haiti,” imesema UNFPA kwenye taarifa yake iliyotolewa leo jijini New York, Marekani. 

Wakunga wameweka rehani maisha yao ili kusaidia wajawazito wakati wa milipuko ya COVID-19 na Ebola. Huko Yemen ambako ni asilimia 50 tu ya vituo vya afya vinafanya kazi, wakunga waligeuza nyumba zao kuwa wodi za muda za wazazi. 

Wakunga pia wanatoa huduma kwa wakimbizi, wahamiaji na kuna wakati wanafanya kazi wakiwa wanatishiwa na vikundi vilivyojihami. 

Mkunga akitayarisha dawa kwa mtoto wa wiki mbili aliye na VVU nchini Uganda.
© UNICEF/Jimmy Adriko
Mkunga akitayarisha dawa kwa mtoto wa wiki mbili aliye na VVU nchini Uganda.

Jukumu la wakunga ni zaidi ya kusaidia mjamzito kujifungua 

Taswira inayojia watu wengi ya wakunga ni kuzalisha wajawazito, lakini zaidi ya kutoa huduma za kabla ya kujifungua, kujifungua na baada ya kujifungua, wakunga wanasaidia familia katika huduma za uzazi wa mpango, unyonyeshaji na uchunguzi wa saratani ya shingo ya kizazi. 

Wanaweza pia kutoa huduma za dharura kwa mtoto iwapo zitahitajika, sambamba na kutoa ushauri wa kuzuia ukeketaji, ukatili wa kijinsia na huduma za afya ya uzazi kwa vijana balehe. 

Ripoti ya hali ya wakunga duniani ya mwaka 2021 iliyotolewa kwa pamoja na UNFPA, ICM na shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni, WHO inasema iwapo serikali zitawekeza kwa wakunga, basi maisha ya watu milioni 4.3  yanaweza kuokolewa kila mwaka ifikapo mwaka 2035, idadi ambayo inajumuisha vifo wakati wa kujifungua, vifo vya watoto wachanga na vizazi mfu. 

Idadi kubwa ya wakunga ni wanawake na kutokana na ueledi wao wanaweza kukidhi asilimia 90 ya mahitaji ya afya ya uzazi na kuzuia asilimia 65 ya vifo vya wazazi na watoto wachanga. 

Hata hivyo bado duniani kote bado kuna pengo la wakunga 900,000.