Mradi wa maji wadhibiti kipindupindu DRC 

Maji safi ya kunywa
World Bank/Arne Hoel
Maji safi ya kunywa

Mradi wa maji wadhibiti kipindupindu DRC 

Afya

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF kwa ushirikiano na kituo cha kimarekani cha kudhibiti magonjwa, CDC wamesaidia ujenzi wa tenki za maji kwa ajili ya wakazi wa Kiziba mjini Goma, jimboni Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC na hivyo kusaidia kuepusha maambukizi ya magonjwa yatokanayo na matumizi ya  maji machafu. 

Mradi huo katika kitongoji cha Kizba, eneo la  Nyiragongo, mjini Goma, jimboni Kivu Kaskazini, umewezesha wanawake, wanaume na watoto kuteka maji katika mabomba yanayotoa maji safi, kufuatia msaada kutoka kituo cha kimarekani cha udhibiti wa magonjwa, CDC na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF

Mabomba 14 yamewekwa katika tanki mbili za kutoa maji, tanki ambazo maji yake yanasukumwa kutoka ardhini kwa nishati ya sola. Mradi uliweka paneli za sola ili kuhakikisha huduma ya maji inarejea baada ya mlipuko wa mwaka jana wa volcano katika mlima Nyiragongo kuharibu mifumo ya maji. 

Mlipuko wa kwanza wa volkano ulitokea tarehe 22  mwezi Mei mwaka jana wa 2021 na kusababisha vifo vya watu 32, maelfu kukimbia makazi huku miundombinu ya kijamii kama vile maji, afya na shule ikiharibiwa. 

Wakazi wa eneo la Kiziba wananufaika na huduma ya maji akiwemo Yvette mama wa watoto sita ambaye baada ya kuteka maji anasema, “Kabla ya kuweko kw a mradi huu, ilikuwa shida sana kupata maji. Tuliteka maji kutoka katika vyanzo vya asili na hivi vilikuwa chanzo cha matatizo yetu ya afya, hasa kwa watoto ambao waliugua kipindupindu na homa ya matumbo. Tangu kuwekwa kwa mabomba haya, tumeona mabadiliko kwa kuwa tunakunywa maji safi.” 

Bomba lingine limepeleka maji katika kituo cha afya cha Kiziba, kituo ambacho pia kinahudumia wagonjwa wa Kipindupindu.  

Marc Kamulanda, muuguzi katika kituo hiki anasema, “bila maji hatuwezi kufanya chochote kile kwenye kituo cha afya kwa sababu zaidi ya asilimia 95 ya huduma zetu zinahitaji maji. Tulipokosa maji, idadi ya wagonjwa wa Kipindupindu iliongezeka. Baada ya maji kuanza kupatikana, idadi ya wagonjwa imepungua. Tunaamini kuwa maji yamekuwa jawabu sahihi kwa tatizo hili.”