Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu
Victor Maleko afisa wa Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania  UTPC akizungumza katika maadhimisho ya Uhuru wa Vyombo vya Habari jijini Arusha

Waandishi wa habari Afrika wakutana kuboresha mpango wa Umoja wa Mataifa kuhusu Usalama wa Waandishi wa Habari

UN News
Victor Maleko afisa wa Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania UTPC akizungumza katika maadhimisho ya Uhuru wa Vyombo vya Habari jijini Arusha

Waandishi wa habari Afrika wakutana kuboresha mpango wa Umoja wa Mataifa kuhusu Usalama wa Waandishi wa Habari

Amani na Usalama

Waandishi wa Habari kutoka nchi mbalimbali barani Afrika wamekutana jijini Arusha nchini Tanzania katika maadhimisho ya siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari kujadili maboresho ya mpango wa utekelezaji wa Umoja wa Mataifa kuhusu Usalama wa Waandishi wa Habari. 

Akizungumza baada ya kukamilika kwa majadiliano hayo Afisa kutoka Umoja wa klabu za waandishi wa habari nchini Tanzania UTPC Victor Maleko amesema mpango huo ulioandaliwa na Umoja wa Mataifa umekuwa muongozo madhubuti kwa taasisi za waandishi wa habari nchini humo kwakuwa unaendana na hali halisi ya nchi. 

“Mpango huu wakati unatengenezwa na Umoja wa Mataifa ulishirikisha taasisi mbalimbali ambazo zipo Tanzania kwa ajili ya kujua ni nini ambacho waandishi wa habari wanataka kitokee au kifanyike katika mpango huu na taasisi zilifanya hivyo na sasa ni miaka 10 na umeletwa tena kwenye maadhimisho haya ili tuuboreshe.”

Kuhusu Mpango huo

Mpango wa Utekelezaji wa Umoja wa Mataifa kuhusu Usalama wa Waandishi wa Habari na ulinzi wao unalenga kuweka mazingira huru na salama kwa waandishi wa habari na wafanyakazi wa vyombo vya habari, wakati wote ikiwa kuna migogoro na hata pasipokuwa na migogoro, kwa nia ya kuimarisha amani, demokrasia na maendeleo duniani kote.

Mpango huu umetoa miongozo kadhaa ikiwemo uanzishwaji wa utaratibu ulioratibiwa wa asasi zinazo washughulikia waandishi katika masuala yanayohusu usalama wa wanahabari.

Pia mpango unachagiza nchi kutunga sheria na taratibu zinazofaa kwa uhuru wa kujieleza na habari, na kuunga mkono juhudi zao za kutekeleza sheria na kanuni za kimataifa zilizopo.

Maleko anasema nchini Tanzania taasisi yao ya UPTC wanashirkiana na jeshi la polisi. “Moja ya mpango ambao UTPC umeshatekeleza ni kuandaa midahalo baina ya jeshi la polisi la Tanzania na waandishi wa habari katika kutengeneza mahusiano mazuri ya utendaji kazi kati ya Jeshi la polisi na waandishi wa habari.”

UTPC pia imenya mafunzo maalum kwa waandishi wa habari 100 ambao watasaidia kujisaidia wao wenyewe pamoja na waandishi wengine pale watakapo kutana na madhila mbalimbali na kujilinda wakati wakitekeleza majukumu yao. 

Ili kuimarisha kinga kwa waandishi wa habari, Mpango wa Utekelezaji wa Umoja wa Mataifa unapendekeza kufanya kazi kwa ushirikiano na serikali, vyombo vya habari, vyama vya kitaaluma na mashirika yasiyo ya kiserikali kufanya kampeni za kuongeza uelewa juu ya masuala mbalimbali kama vile mikataba ya kimataifa iliyopo, hatari inayoongezeka kutokana na vitisho vinavyojitokeza kwa wanataaluma wa habari, wakiwemo watendaji wasio wa serikali, pamoja na miongozo mbalimbali iliyopo kuhusu usalama wa wanahabari.