Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tubadili mwelekeo wa kukabili uhaba wa chakula- Ripoti

Mizozo imesalia kuwa kichocheo kikubwa cha ukosefu wa uhakika wa kupata chakula duniani.
© FAO/Sonia Nguyen.
Mizozo imesalia kuwa kichocheo kikubwa cha ukosefu wa uhakika wa kupata chakula duniani.

Tubadili mwelekeo wa kukabili uhaba wa chakula- Ripoti

Msaada wa Kibinadamu

Mtandao wa kimataifa duniani dhidi ya janga la chakula, GNAFC umezindua ripoti yake hii leo huko Roma, Italia kuhusu janga la chakula inayosema kuwa idadi ya watu wanaokabiliwa na ukosefu mkubwa wa chakula sambamba na wanaohitaji siyo tu msaada wa chakula kuokoa maisha yao bali pia msaada wa kuendesha maisha yao inaongezeka kwa kiasi kinachotia mashaka makubwa. 

Mtandao huo unaoundwa na mashirika ya Umoja wa Mataifa likiwemo lile la mpango wa chakula duniani, WFP, chakula na kilimo FAO pamoja na Muungano wa Ulaya, EU umesema kutokana na mwelekeo huo kinachopaswa kufanyika sasa ni kushughulikia chanzo cha janga la uhaba wa chakula badala ya kuibua majawabu baada ya uhaba wa chakula kutokea. 

Kilichobainika: Watu 570,000 wako hatarini kufa kwa njaa 

Ripoti iyojikita kwenye nchi na maeneo ambamo kiwango cha ukosefu wa chakula kinazidi rasilimali na uwezo uliopo kupata chakula na hivyo kuna ulazima wa jamii ya kimataifa kuingilia kati. 

Imebainika kuwa watu milioni 193 katika nchi 53 na maeneo walikuwa kati ya awamu ya 3 na 5 ya ukosefu wa uhakika wa kupata chakula mwaka 2021. Kwa mujibu wa vipimo vya Umoja wa Mataifa, awamu ya juu zaidi  ni 5. 

“Hii ina maana ongezeko la watu takribani milioni 40 ikilinganishwa na kiwango kilichovunja rekodi mwaka 2020,” imesema ripoti hiyo. 

Kati yao hao, watu 570,000 wako Ethiopia, kusini mwa Madagascar, Sudan Kusini na Yemen na ripoti inawaweka katika awamu ya 5 ya ukosefu wa chakula hivyo wanahitaji msaada wa dharura kuepusha kutwama kwa mbinu za kujipatia kipato sambamba na kufa kwa njaa. 

Madagasscar inayokabiliwa na ukame mkali imeelezewa kama eneo linalokabiliwa na njaa.
© UNICEF/Safidy Andriananten
Madagasscar inayokabiliwa na ukame mkali imeelezewa kama eneo linalokabiliwa na njaa.

Chanzo cha janga la chakula 

Ripoti inataja vichocheo lukuki kuanzia mapigano ya kivita, mabadiliko ya tabianchi, changamoto za kiuchumi, majanga ya kiafya huku umaskini na ukosefu wa usawa kuwa sababu zilizojikita. 

Pamoja na ripoti kusema kuwa uvamizi wa Urusi nchini Ukraine umefichua jinsi mtandao wa mifumo ya chakula duniani ilivyo hatarini pindi vita inatokea, imetaja pia vichocheo mahsusi vya janga la njaa mwaka 2021. 

Mizozo 

Mapigano ya kivita yamefanya watu milioni 139 wakose kabisa uhakika wa kupata chakula katika nchi 24, idadi ambayo imeongeza kutoka milioni 99 mwaka 2020 katika nchi 23. 

Mtoto mvulana wa umri wa kwenda shule akiwasaidia wanaume kuwanywesha maji mifugo katika kijiji cha Bandarero kilichoathiriwa na ukame huko Kaunti ya Moyale, Kenya.
Rita Maingi/OCHA
Mtoto mvulana wa umri wa kwenda shule akiwasaidia wanaume kuwanywesha maji mifugo katika kijiji cha Bandarero kilichoathiriwa na ukame huko Kaunti ya Moyale, Kenya.

Hali ya hewa 

Hali ya hewa nayo imekuwa si ya kawaida na hivyo watu milioni 28 katika nchi 8 na maeneo ikiwa ni ongezeko kutoka watu milioni 15.7 mwaka 2020. 

Mparaganyiko wa kiuchumi 

Kuvurugika kwa uchumi kumesukuma watu zaidi ya milioni 30 katika nchi 21 kushindwa kupata chakula na hii ni kutokana na janga la Corona au COVID-19. Hata hivyo idadi imepungua kutoka milioni 40 mwaka 2020. 

Mwaka wa 2019 Nchi ya Ethiopia ilikua inaongoza katika ukosefu wa chakula  kote duniani
FAO/IFAD/WFP/Michael Tewelde
Mwaka wa 2019 Nchi ya Ethiopia ilikua inaongoza katika ukosefu wa chakula kote duniani

Nini kifanyike? 

Mkurugenzi Mkuu wa FAO, Qu Dongyu anasema, “Muunganiko kati ya mizozo na ukosefu wa uhakika wa chakula, kwa mara nyingine tena uko dhahiri na unatia mashaka. Wakati jamii ya kimataifa imechukua hatua kwa ujasiri zichukuliwe hatua za kuepusha baa la njaa na hatua za kupunguza makali, bado kuna changamoto kubwa ya kupata rasilimali na fedha ili kukidhi mahitaji yanayoongezeka.” 

Amesema matokeo ya ripoti hii yanaonesha zaidi umuhimu wa hatua za pamoja kushughulikia janga la ukosefu wa chakula duniani kwa misingi ya misaada ya kibinadamu, kimaendeleo na kusongesha amani. 

Mwelekeo unaotakiwa 

Kunatakiwa mbinu za pamoja na jumuishi kuzuia, kubaini yanayoweza kutokea na kulenga kwa usahihi sababu kuu za janga la chakula duniani, ikiwemo umaskini wa kimfumo, kuenguliwa baadhi ya jamii kwenye maendeleo, ongezeko la idadi ya watu na kupatia majawabu mifumo dhaifu ya chakula duniani,” imesema taarifa hiyo ya pamoja ya EU, FAO na WFP pamoja na shirika la maendeleo ya kimataifa la kimarekani, USAID na Benki ya Dunia.