Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu
Judith Candiru, Muuguzi Msaidizi katika kituo cha afya cha Midigo, wilaya ya Yumbe nchini Uganda.

Hawavumi ila wamo; mashujaa wa COVID-19 

© UNICEF/Zahara Abdul
Judith Candiru, Muuguzi Msaidizi katika kituo cha afya cha Midigo, wilaya ya Yumbe nchini Uganda.

Hawavumi ila wamo; mashujaa wa COVID-19 

Afya

Kwa baadhi ya watu, huhisi ni kazi. Kwa wengine ni wajibu. Na kuna wale wanaona ni muhimu. Miaka miwili iliyopita, shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni, WHO lilitangaza mlipuko wa ugonjwa wa Corona au COVID-19 kuwa janga duniani. Hakuna yeyote aliyetambua kinachofuatia. Lakini katika kipindi cha miezi 24 baada ya tangazo hilo, watu wa kipekee, wanawake kwa wanaume wameibuka na kunusuru jamii zao. Majina yao hayafahamiki, lakini vitendo vya mashujaa hawa bila shaka yoyote ile, vimefanya dunia kuwa pahala salama na bora. Je ni akina nani? 

Mhudumu wa afya nchini Uganda atumiaye kipaza sauti kuchagiza jamii yake ipate chanjo ya COVID-19 

Wakati akikua, Judith Candiru alivutiwa sana na vazi jeupe la wauguzi. Kwake yeye zaidi ni ile huduma waliyokuwa wanatoa. Leo hii, ni miongoni mwao. Anajivunia kuvaa vazi hilo nadhifu pamoja na mkanda wa manjano. 

 

Kwa Bi. Candiru, COVID-19 anaitambua sana kwa kuwa aliugua na kuna wakati yeye na familia yake walinyanyapaliwa. 

“Hiki kilikuwa kipindi cha huzuni sana kwenye ajira yangu. Jamii ilinitenga mimi na familia yangu.” 

Hata hivyo, hiyo haikumvunja moyo. Alipona na kurejea kazini. Bi. Candiru anahudumia kwa upendo wakazi wa wilaya ya Yumbe, kaskazini mwa Uganda, eneo lililosambaa hadi mpaka na Sudan Kusini. 

 

Judith Candiru akiwa kwenye bodaboda na kipaza sauti chake akielekea wilaya ya Yumbe nchini Uganda kuelimisha umma umuhimu na faida ya chanjo ya COVID-19
© UNICEF/Zahara Abdul
Judith Candiru akiwa kwenye bodaboda na kipaza sauti chake akielekea wilaya ya Yumbe nchini Uganda kuelimisha umma umuhimu na faida ya chanjo ya COVID-19

Asubuhi anasimamia wodi ya wazazi ambako anahudumia watoto njiti. Kupitia mafunzo yaliyofadhiliwa na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF, Bi. Candiru anaweza kuhudumia watoto wachanga wagonjwa na kuhakikisha kuwa wanaishi. 

Lakini hiyo ni sehemu tu ya jukumu lake la siku. Wakati wote wa janga la COVID-19, baada ya mashauriano na kupitia wazazi wodini, hutembelea jamii yake iwe kwa mguu au kwa pikipiki. 

Akiwa na kipaza sauti chake, Bi. Candiru amekuwa anapazia sauti ujumbe juu ya umuhimu na usalama wa chanjo dhidi ya COVID-19. 

 

Judith Candiru, Muuguzi Msaidizi huko wilaya ya Yumbe nchini Uganda akitoa huduma za chanjo kwa wanajamii wa eneo la Midigo.
© UNICEF/Zahara Abdul
Judith Candiru, Muuguzi Msaidizi huko wilaya ya Yumbe nchini Uganda akitoa huduma za chanjo kwa wanajamii wa eneo la Midigo.

Ujumbe wake unafikika na kusikika na kukubalika. Wanajamii wanamuamini kwa kuwa mmoja baada ya mwingine huketi kwenye kiti na kupatiwa chanjo kutoka kwake. 

Kupanda milima na kuvuka mabonde Nepal huku amebeba chanjo mgongoni 

Kwa miaka kadhaa sasa Birma Kunwar amekuwa akipandisha milima na kuvuka madaraja yanayoning’inia. Akiwa amebeba mgongoni boksi lenye chanjo, hupandisha njia zilizoko milimani kwenye maeneo ya ndani zaidi huko Nepal. 

Tarehe 3 Agosti mwaka 2021 Birma Kunwar akivuka mabonde na milima kufikisha chanjo maeneo ya ndani kabisa nchini Nepal.
© UNICEF/Laxmi Prasad Ngakhusi
Tarehe 3 Agosti mwaka 2021 Birma Kunwar akivuka mabonde na milima kufikisha chanjo maeneo ya ndani kabisa nchini Nepal.

Hata kabla ya janga la COVID-19, Bi. Kunwar amekuwa anakusanya chanjo za kuokoa maisha kwenye mji wa Khalanga, ambao ni makao makuu ya wilaya ya Darchula. Dozi hizo ni zile za chanjo za kwenye ratiba ya kawaida kwa ajili ya watoto wanaoishi kwenye vijiji vilivyoko milimani. 

Janga la Corona lilileta changamoto mpya na fursa mpya: “Nimekuwa nikipita nji hizo hizo lakini sasa nikiwa na chanjo za COVID-19,” anasema Bi. Kunwar. 

Tamati ya safari yake hiyo ni kituo cha afya kilichoko kijijini Duhun. Na kuna majira mengine ya mwaka ambako eneo hilo hufikika kwa mguu pekee. 

“Kwa miezi mingi ya mwaka, barabara hapa haziaminiki hasa wakati wa mvua,” anasema Bi. Kunwar akielezea changamoto zitokanazo na maporomoko ya udongo. “Ni safari yenye hatari.” 

Lalita Dhami, (kulia) mhudumu wa afya akizungumza na mtoto aliyebebwa na mfanyakazi mwenzake Birma Kunwar.
© UNICEF/Prasad Ngakhusi
Lalita Dhami, (kulia) mhudumu wa afya akizungumza na mtoto aliyebebwa na mfanyakazi mwenzake Birma Kunwar.

Kwa hiyo afya ya jamii yake iko mgongoni mwake, mara nyingi safari nzima huifanya kwa kutembea. Hii humchukua kati ya saa tatu hadi nne za kutembea.  

Kwa Bi. Kunwar, safari hii ina thamani kubwa. Kupeleka chanjo muhimu kw ajamii yake siyo tu ni kazi bali wajibu. 

“Watu husubiri kwa hamu chanjo, wanauliza mara kwa mara, zitafika lini? Tutapatiwa lini? Lini itakuwa zamu yangu. Kila wakati.” 

Kijana balehe na ubunifu wa mfumo salama wa kunawa mikono 

Emmanuel Cosmos Msoka ni mbunifu na mwanaharakati. Si bure kwamba kijana huyu balehe mwenye  umri wa miaka 18 kutoka Tanzania alibuni kifaa muhimu cha kujisafi wakati wa janga la Corona. 

Emmanuel Msoka, mwenye umri wa miaka 18 ni mbunifu kijana nchini Tanzania ambaye wakati wa COVID-19 alibuni kifaa cha kunawia mikono.
© UNICEF/UN0510836/
Emmanuel Msoka, mwenye umri wa miaka 18 ni mbunifu kijana nchini Tanzania ambaye wakati wa COVID-19 alibuni kifaa cha kunawia mikono.

“Nilizaliwa kwenye miteremko yam lima mrefu kabisa barani Afrika, Kilimanjaro,” anasema Emmanuel. Ni sehemu pekee nchini mwangu ambako maji yanageuka theluji na barafu.  

Emmanuel alikua huku akiwa na hamu ya kubadili jinsi mambo yanafanywa na kusaidia kutatua changamoto za kijamii. Hilo alifanikiwa. Ugonjwa wa COVID-19 ulipobisha hodi Tanzania, na jamii yake ikaanza kuhaha, yeye alichukua hatua.   

Wazo lake: machine ya kunawa mikono ambayo inafanya kazi pindi mguu unapokanyaga pedali, kwa kufanya hivyo alisaidia kupunguza kusambaa kwa virusi. Tangu abuni teknolojia hiyo, ameweza kusambaza zaidi ya machine 400 maeneo ya kaskazini mwaTanzania. 

Kwa ubunifu huu, Emmanuel alichaguliwa kuwa Mchechemuzi Kijana wa UNICEF na pia aliteuliwa kuwania tuzo ya kimataifa ya watoto, tuzo inayotolewa kila mwaka kwa mtoto ambaye ameleta mchango mkubwa katika kusongesha haki za watoto. 

Ahudumia nduguze huku akisoma wakati amefiwa 

Keysha ana umri wa miaka 14. Ingawa ni mdogo, busara zake na fikra zake ni zaidi ya umri wake na alilazimika kukua haraka kifikra. Mama yake mzazi ambaye alikuwa anafanya kazi kwenye mgahawa alikufa kwa COVID-19. 

Keysha (kulia) akiwa na nduguze wawili, Afiqa mwenye umri wa miaka 7 na Khansa mwenye umri wa miaka 3 kwenye nyumba  yao Sragen, Java ya Kati, nchini Indonesia.
© UNICEF/Jiro Ose
Keysha (kulia) akiwa na nduguze wawili, Afiqa mwenye umri wa miaka 7 na Khansa mwenye umri wa miaka 3 kwenye nyumba yao Sragen, Java ya Kati, nchini Indonesia.

“Mama yetu alifanya kazi kwa saa 12 kwenye mgahawa pindi mgahawa ulipofunguliwa tena baada ya Corona,” anasema Keysha akiongeza kuwa “kinga yake mwilini ilikuwa dhaifu na pengine ndio maana aliambukizwa COVID-19.” 

Keysha alilazibika kubeba jukumu zaidi, kulea wadogo zake wawili. Amekuwa akimlea mdogo wake wa kike, Afiqa mwenye umri wa miaka 7, Afiqa ndiye ameathirika zaidi vibaya kufuatia kifo cha mama yao. Afiqa mara nyingi hukaa chumbani akitumia muda mwingi kutazama video zenye sauti ya  mama yao. 

Pamoja na jukumu la malezi ya nduguze, Keysha anatambua changamoto za kifedha zinazomkabili baba yao ambaye ndiye pekee anafanya kazi. 

Baba yao anafanya kazi ya kuegesha magari kwenye mgahawa ambako mkewe marehemu alikuwa anafanya kazi. Kwa hiyo basi ili kusaidia kuongeza kipato, Keysha ana mpango wa kujiandikisha kwenye shule ya stadi za kazi ,mafunzo ambayo yatamwezesha kupata ajira haraka na hivyo kumsaidia baba yake. 

Keysha akiwa anafanya kazi zake za shuleni, nyumbani kwao Sragen, jimbo la Kati la Java nchini Indonesia.
© UNICEF/Jiro Ose
Keysha akiwa anafanya kazi zake za shuleni, nyumbani kwao Sragen, jimbo la Kati la Java nchini Indonesia.

Keysha na nduguze, ni miongoni mwa maelfu ya watoto ambao wamepoteza mzazi au mlezi kutokana na COVID-19 nchini Indonesia. Kwa sasa serikali za mitaa pamoja na mradi wa UNICEF wa kusaidia watoto kiafya na kisaikolojia ndio tegemeo lao.