Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

FAO yachagiza umuhimu wa kuthamini miti na misitu katika kongamano la 15

Wanajamii wakisaidia katika utunzaji wa misitu Viet Nam.
ADB/Lester Ledesma
Wanajamii wakisaidia katika utunzaji wa misitu Viet Nam.

FAO yachagiza umuhimu wa kuthamini miti na misitu katika kongamano la 15

Tabianchi na mazingira

Misitu na miti ni muhimu sana katika kujikwamua kimazingira na kujenga mnepo katika uchumi na jamii amesema mkurugenzi mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la chakula na kilimo FAO QU Dongyu.

Qu ameyasema hayo mjini Seoul Jamhuri ya Korea kunakofanyika kongamano la 15 la misitu lililobeba maudhui "Kujenga mustakabali unaojali mazingira, wenye afya na mnepo na misitu" kongamano ambalo ni la kwanza kufanyika Asia kwa kipindi cha miaka 43 tangu lilipofanyika mara ya mwisho nchini Indonesia.

FAO inasema pia hili ni kongamano la kwanza kufanyika ana kwa ana na kwa njia ya mtandao na hivyo kutoa fursa kubwa kwa maelfu ya watu kutoka kote duniani kushiriki.

Misitu ni nguzo ya kufikia SDG’s

"Misitu ni washirika wetu wakuu katika kufikia malengo ya ajenda ya maendeleo ya mwaka 2030 ikiwa ni pamoja na kupambana na kuenea kwa jangwa, kufikia uhakika wa chakula na kuboresha maisha, pamoja na malengo ya kimataifa ya misitu, mkataba wa Paris, muongo wa Umoja wa Mataifa wa urejeshaji wa Mfumo wa mazingira, na mkakati wa kimataifa wa baada ya 2020 wa mfumo wa bayoanuai”, Amesema mkuu wa FAO.

Qu ameongeza kuwa “Huu ni ujumbe muhimu unaopaswa kubebwa kwa mikutano muhimu ya kimataifa ya mikataba ya Rio na vikao vingine vya kimataifa ambapo maamuzi yatafanywa kuhusu mustakabali wa sayari na watu wake, ili kuhakikisha kuwa misitu ni sehemu muhimu ya suluhisho la changamoto za sasa na zijazo."

Mwanadamu anakabiliwa na changamoto nyingi

Mkurugenzi huyo mkuu wa FAO amesema kongamano hili limekuja wakati ubinadamu unakabiliwa na changamoto nyingi, ambayo mara nyingi zinahusiana na kuingiliana ikiwemo janga la mabadiliko ya tabianchi, upotezaji wa bayoanuai, mizozo, janga la COVID-19 na kupanda kwa bei ya vyakula, ambayo inawakumba maskini zaidi ambao ndio waathirika wakubwa.

Leo, zaidi ya watu milioni 800 bado wanakabiliwa na njaa, na bilioni 3 hawawezi kumudu lishe bora. "Misitu inaweza kuchukua jukumu muhimu katika kurejesha mifumo ya ikolojia kwa lengo la kuhakikisha maisha bora kwa wote,"

Kwa upande wake Rais wa Jamhuri ya Korea Moon Jae-in katika hotuba yake alisisitiza haja ya jumuiya ya kimataifa kufanya mipango ya kina na kuiweka katika vitendo ili kujenga mustakabali endelevu wa kizazi kijacho. 

Naye Binti Mfalme wa Jordan Basma bint Ali wakati huo huo amehimiza udharura wa kukabiliana na kurejesha mfumo wa ikolojia, huku akisisitiza umuhimu wa mbinu mbalimbali za kukabiliana na kazi hiyo.

Ujumbe wa video wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres katika kongamano hilo umetaka “kutambuliwa vyema kwa thamani ya misitu na kuwataka washikadau wote kuja na mawazo na ahadi ambazo zinaweza kutekelezwa.”

Nchini Indonesia watu wengi hutegemea bioanuwai ya misitu ili kujipatia riziki.
CIFOR/Ulet Ifansasti
Nchini Indonesia watu wengi hutegemea bioanuwai ya misitu ili kujipatia riziki.

Njia 3 za miti na misitu kusaidia uchumi na mazingira

Bwana Qu ameainisha njia tatu zinazoshabihiana kwa ajili ya mitin a misitu kusaidia uchumi na kujikwamua kimazingira kwa

Mosi: kukomesha ukataji miti na kudumisha upandaji miti

Pili: kwa kukarabati ardhi iliyoharibiwa na mmomonyoko wa udongo na kupanua wigo wa kilimo cha misitu

Na tatu: Kuwa na matumizi endelevu ya misitu na kujenga mnyororo wa tahamni wa misitu unaojali mazingira.

Misitu na kilimo vinasaidiana

Qu amesisitiza umuhimu wa mtindo ambao misitu na kilimo vinasaidiana. "Kwa pamoja, kilimo na misitu vina jukumu la msingi katika maendeleo ya nyenzo na bidhaa mpya zinazoweza kurejelezwa, pamoja na mbinu za ubunifu za mazingira na minyororo ya thamani, ili kunufaisha watu na sayari."

Kufikia maono haya  amesema kunahitaji kuweka vipaumbele sahihi vya sera, kuoanisha motisha za kifedha, malengo endelevu na kukuza uwekezaji. Wazalishaji wadogo na wa kati, jumuiya za wenyeji na watu wa asili wana jukumu kubwa katika kuongeza ufumbuzi wa misitu.

Hata hivyo amebainisha kuwa wazalishaji wadogo wanapokea chini ya asilimia 2 ya fedha za kukabili mabadiliko ya tabianchi duniani.

Amesisitiza kuwa ufadhili wa fedha kwa ajili ya njia hizo tatu lazima uongezwe angalau mara tatu ifikapo 2030 ili kufikia malengo yakukabili mabadiliko ya tabianchi, bayoanuai na udhibiti wa uharibifu wa ardhi.

Hii ni pamoja na uwekezaji mpya kupitia ufadhili wa mabadiliko ya tabianchi, programu za uokoaji wa mazingira na sekta kibinafsi.

Qu pia alisisitiza umuhimu wa kuacha kujitenga na maghala na kuchukua mtazamo wa pamoja ulioratibiwa vyema  na kuongeza kuwa FAO inaimarisha kazi yake na serikali, sekta binafsi, wanazuoni, jamii, wanawake na vijana.

"Kwa pamoja, tunaweza kuibua uwezo kamili wa misitu kufikia uzalishaji bora, lishe bora, mazingira bora, na maisha bora kwa wote, bila kumwacha mtu yeyote nyuma," amemalizia mkurugenzi huyo mkuu wa FAO.