Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Udukuzi wa kidijitali na kuwanyamazisha kisiasa ni tishio kwa waandishi wa habari: UN 

Mwandishi wa habari akichukua tukio kwa video
Unsplash/Jovaughn Stephens
Mwandishi wa habari akichukua tukio kwa video

Udukuzi wa kidijitali na kuwanyamazisha kisiasa ni tishio kwa waandishi wa habari: UN 

Masuala ya UM

Ikiwa leo ni siku ya uhuru wa vyombo vya habari duniani Umoja wa Mataifa umeeleza kuwa waandishi wa habari na wafanyakazi wa vyombo vya habari wanakabiliwa na vitisho dhidi ya uhuru wao wa kufanya kazi zao ikiwemo kudukuliwa kidigitali na kunyamazishwa kisiasa.

Kupitia ujumbe wake alioutoa kwa njia ya video Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema pamoja na ukweli kuwa waaandishi wa habari wamekuwa na jukumu kubwa la kuifahamisha jamii kuhusu masuala mbalimbali ikiwemo afya na mabadiliko ya tabianchi lakini vitisho wanavyokabiliana navyo wakati wa kuripoti na kusimulia matukio hayo kwa haki na kwa usahihi, vinaongezeka kila siku. 

Guterres amesema “kuanzia masuala ya afya duniani hadi janga la tabianchi, rushwa, na ukiukwaji wa haki za binadamu, waandishi wanakabiliwa na ongezeko la siasa katika utendaji wa kazi zao na majaribio ya kuwanyamazisha kutoka pande nyingi.” 

Ameongeza ingawa teknolojia ya kidijitali ina demokrasia ya kupata habari, pia  imezua changamoto kubwa kwa wanahabari suala lililoungwa mkono na Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa Mataifa Michelle Bachelet ambaye ameelezea ongezeko la matumizi ya zana za uchunguzi kama vile Pegasus au Candiru spyware ambazo hudukua na kuingilia maisha ya watu. 

Bachelet amesema “zana hizo za kiteknolojia ambazo zimeripotiwa kutumika angalau nchi 45 duniani ni dharau kwa haki ya faragha na kizuizi cha uhuru wa kujieleza na kwamba matumizi yake  yamesababisha kukamatwa, vitisho na hata mauaji ya waandishi wa habari, kuhatarisha vyanzo vya habari pamoja na kuweka familia zao hatarini.” 

Mataifa yote yamekumbushwa kuwa wanahitaji kuanzisha mbinu za kudhibiti ununuzi na usambazaji wa teknolojia za uchunguzi akisema, lazima yahakikishe kampuni husika zinawajibika. 

“Kuheshimu haki za binadamu sio jukumu la serikali pekee bali pia kampuni za uchunguzi wa kibinafsi zithibitishe  hadharani wajibu wao wa kuheshimu uhuru wa kujieleza na faragha, kuzingatia haki za binadamu, na kutoa ripoti kwa uwazi kuhusu shughuli zao. Muhimu zaidi, hii inapaswa kufanywa kwa mashauriano ya mara kwa mara na mashirika ya kiraia,” amesema Bi. Bachelet