Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vikwazo lukuki kwa harakati za maendeleo nchi zinazoendelea- ILO

Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa maendeleo ya mitaji, UNCDF unasaidia kuwawezesha kiuchumi wanawake katika nchi 46 zinazoendelea, (LDCs)
UNCDF
Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa maendeleo ya mitaji, UNCDF unasaidia kuwawezesha kiuchumi wanawake katika nchi 46 zinazoendelea, (LDCs)

Vikwazo lukuki kwa harakati za maendeleo nchi zinazoendelea- ILO

Ukuaji wa Kiuchumi

Ripoti mpya ya shirika la Umoja wa Mataifa la kazi duniani, ILO, inasema maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika nchi zinazoendelea, LDCs, yamedorora kutokana na athari za janga la ugonjwa wa Corona, au COVID-19, mabadiliko ya tabianchi na majanga yanayoendelea hivi sasa ya uhaba wa nishati na chakula   

Taarifa iliyotolewa na ILO hii leo jijini New York, Marekani  imenukuu ripoti hiyo ikisema kuwa nchini nyingi zinazoendelea zilichukua hatua lukuki kukabiliana na COVID-19 kama vile kutoa mafungu kadhaa ya usaidizi, licha ya pengo kubwa la fedha na ukata.

Hata hivyo, udhaifu wa kimuundo umefanya nchi hizo ziwe hatarini zaidi na mitikisiko ya sasa na hali inaweza kuwa mbaya zaidi iwapo mataifa hayo ya LDCs hayatashiriki kikamilifu katika harakati za sasa za dunia kujikwamua kiuchumi.

Mchuuzi wa matunda katika soko la Port Victoria nchini Seychelles
UN Women/Ryan Brown
Mchuuzi wa matunda katika soko la Port Victoria nchini Seychelles

Ikipatiwa jina, “Hali ya sasa ya ajira na mustakabali wake Katia LDCs,” ripoti inawasilisha tathmini ya maendeleo ya changamoto za kimuundo zinazokabili mataifa hayo katika marekebisho ya kimuundo, kipindi cha mpito kuelekea uchumi usioharibu mazingira na kuanzishwa kwa ajira bora zenye hadhi.

Ripoti inaelezea mwelekeo wa sasa wa uzalishaji, tija, ajira na kazi zenye utu, pamoja na nafasi ya hifadhi ya jamii na taasisi za kazi.

LDCs ni ngapi na hali ya maisha ikoje?

Kwa sasa kuna nchi 46 katika kundi la nchi zinazoendelea, zikiwa na idadi ya asilimia 12 ya watu wote duniani. “Mataifa haya sifa zake ni vipato vya chini na kuwa hatarini kuathiriwa vibaya na mitetemo ya kiuchumi na mazingira, maendeleo duni ya kibinadamu, umasikini uliopitiliza na viwango vya juu vya vifo.”

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, hatari ya LDCs kutumbukia kwenye matatizo ni matokeo ya udhaifu katika tija unaohusishwa na ukosefu wa uwezo wa wananchi wake, ukosefu wa miundombinu na fursa ndogo ya kunufaika na teknolojia. “Ni matokeo pia ya taasisi dhaifu, ikiwemo taasisi za kazi na mifumo ya hifadhi ya jamii.”

Ajira isiyo rasmi ni asilimia 90 katika nchi maskini

Katika nchi hizo, ajira zisizo rasmi zimesheheni na huwasilisha takribani asilimia 90 ya ajira zote kwenye mataifa hayo yanayoendele.

Halikadhalika kuna tofauti kubwa kati ya utendaji wa mashirika kwa upande wa uwezo na tija.

Mwendesha bodaboda salama na mchuuzi wanatumia boda salama, app ya simu kwa ajili ya kusafirisha chakula wakati wa vikwazo kwa ajili ya kuzuia COVID-19.
UNCDF
Mwendesha bodaboda salama na mchuuzi wanatumia boda salama, app ya simu kwa ajili ya kusafirisha chakula wakati wa vikwazo kwa ajili ya kuzuia COVID-19.

Teknolojia ni jawabu kunusuru LDCs.

Ripoti imetathmini ni kwa vipi teknolojia za kidijitali zinaweza kuleta mafanikio makubwa hususan kwenye nchi zenye idadi kubwa ya vijana, “lakini kuwepo na uwekezaji mkubwa kwenye mitaji, stadi na ufahamu ili kusaidia ajira jumuishi na zenye utu.”

Nini kifanyike?

Ripoti ina mapendekezo kadhaa ikiwemo kupanua wito wa misaada rasmi ya maendeleo ili kuimarisha huduma za afya, chanjo na kuepusha vidhibiti visivyo rasmi vya uhamiaji na biashara.

Halikadhalika kuimarisha taasisi za ajira na sera za ajira kwa aijli ya kazi zeny eutu na kuimarisha sera zinazochukua hatua kwa tabianchi ili kuwa na uchumi usioharibu mazingira.

Akizungumzia ripoti hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa ILO, Guy Rider amesema, “mitikisiko lukuki imeweka LDCs katika shinikizo kubwa, lakini kama kuna sera sahihi za ajira na sera sahihi za uchumi mkubwa, ajira mpya zinaweza kuanzishwa sambamba na zilizoko bila kusahau ubunifu unaochochewa na uwekezaji katika ajira zisizoharibu mazingira na kufungua fursa za uchumi wa kidijitali.