Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ajenda Mpya ya Miji ni jawabu la Ajenda 2030- Amina

Huduma za usafiri wa mwendokasi jijini Dar es salaam nchini Tanzania ni miongoni mwa mipango ya miji ya kuimarisha huduma kwa wakazi kadri inavyozidi kukua
World Bank/Hendri Lombard
Huduma za usafiri wa mwendokasi jijini Dar es salaam nchini Tanzania ni miongoni mwa mipango ya miji ya kuimarisha huduma kwa wakazi kadri inavyozidi kukua

Ajenda Mpya ya Miji ni jawabu la Ajenda 2030- Amina

Masuala ya UM

Umoja wa Mataifa umetaja mambo makuu mawili ambayo itazingatia katika kuwezesha nchi wanachama kutekeleza kwa ufanisi Ajenda Mpya ya Miji yenye lengo la kuhakikisha kuwa kila mtu anapata haki sawa na kunufaika na fursa zitokanazo na ukuaji wa miji kiendelevu.

Akizungumza jijini New York, Marekani katika kikao cha ngazi ya juu cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuhusu utekelezaji wa ajenda hiyo, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bi. Amina J. Mohammed ametaja mambo hayo kuwa ni pamoja na waratibu wakazi wa Umoja wa Mataifa na timu zao kuongeza juhudi za kujumuisha katika program zao mipango ya ukuaji wa miji na kushirikiana na nchi husika katika utekelezaji.

“Wakiongozwa na mbinu za kimsingi katika ngazi ya kitaifa, mfumo wa Umoja wa Mataifa utatoa usaidizi wa kuandaa sera za kitaifa za miji sambamba na mipango miji kulingana na mahitaji ya taifa husika,” amesema Naibu Katibu Mkuu.

Amesema marekebisho ya hivi karibuni ya mfumo wa maendeleo wa Umoja wa Mataifa unawezesha timu za Umoja wa Mataifa mashinani kutoa misaada mahsusi kwa nchi husika kulingana na mahitaji.

Bi. Mohammed ametaja jambo la pili kuwa ni ubia wa kitaifa kwa ajenda 2030 au Local2030 Coalition unaoongozwa na shirika la Umoja wa Mataifa la makazi, UN-Habitat na lile la mpango wa maendeleo, UNDP utahamasisha na kuleta pamoja harakati za serikali za kitaifa na mitaa pamoja na sekta za biashara, mashirika ya kirai na mitandao mingine bila kusahau wajasiriamali.

Watoto wakisikiliza kwa makini wakati wa ufunguzi wa kituo chao kwenye kitongoji cha hali duni cha Mathare kilichopo katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi
UN-Habitat/Kirsten Milhahn
Watoto wakisikiliza kwa makini wakati wa ufunguzi wa kituo chao kwenye kitongoji cha hali duni cha Mathare kilichopo katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi

“Mfumo huu wa ushirikiano ni msing iwa ripoti ya Ajenda Yetu ya Pamoja ya Katibu Mkuu wa UN ambayo inatambua dhima adhimu ya wadau katika mchakato wa maendeleo,” amesema Bi. Mohammed.

Ajenda ya Miji ni msingi wa kufanikisha SDGs.

Naibu Katibu Mkuu amesema tayari “tumeingia mwaka wa pili wa muongo wa kufanikisha SDGs, na ajenda hii mpya ya miji ni msingi wa mafanikio ya malengo ya maendeleo endelevu.”

Amekumbusha kuwa ukuaji wa miji ni jambo linaloainisha karne ya 21 na ni mbinu thabiti ya kufikia maendeleo endelevu iwapo itapangwa na kusimami vizuri.

“Tayari zaidi ya asilimia 50 ya wakazi wa Dunia wanaishi mijini. Idadi hii itaongezeka hadi takribani asilimia 70 mwaka 2050,” amesema Naibu Katibu Mkuu.

Baadhi ya miji itapanuka na kuwa na idadi kubwa ya watu, “ni injini za ukuaji, ubunifu, utamaduni na ufahamu. Lakini pia imegubikwa na mashinikizo ya mazingira, rasilimali, maji na nishati,”

Ajenda Mpya ya Miji kumaliza changamoto mijini

Bi. Mohammed amesema ni kwa kuzingatia changamoto zinazokumba miji sasa na changamoto za siku za usoni ndio  maana Ajenda Mpya ya Mijini muhimu.

Familia zinazoishi kwenye makazi duni katika mji mkuu wa Bangladesh, Dhaka zinapatiwa huduma za dharura wakati wa janga la COVID-19
UNDP/Fahad Kaizer
Familia zinazoishi kwenye makazi duni katika mji mkuu wa Bangladesh, Dhaka zinapatiwa huduma za dharura wakati wa janga la COVID-19

“Inaweka njia ya wazi kabisa ya nchi kuendeleza kwa dhati miji yake kiendelevu kwa kuwa na uchumi wenye mnepo,” amesema Naibu Katibu Mkuu akikumbusha hata hivyo ukuaji wa miji usije ukapatiwa kipaumbele zaidi na kusahau maeneo ya vijijini.

Ajenda Mpya ya Miji inataka nchi wanachama kuwa na será zinazotazamia kubadilika kwa aina ya makundi mijini na zihakikishe kuna mizania kwenye maendeleo katika maeneo yote ili asiweko mtu yeyote anayeachwa nyuma.