Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu
Msaada wa chakula ukisafirishwa hadi jimbo la Jonglei kupitia mto Nile nchini Sudan Kusini.

UNMISS kubadili mbinu za utoaji wa misaada ya kibinadamu Malakal

© WFP/Gabriela Vivacqua
Msaada wa chakula ukisafirishwa hadi jimbo la Jonglei kupitia mto Nile nchini Sudan Kusini.

UNMISS kubadili mbinu za utoaji wa misaada ya kibinadamu Malakal

Msaada wa Kibinadamu

Ziara maalum iliyofanywa na Mratibu wa Umoja wa Mataifa wa misaada ya Kibinadamu nchini Sudan Kusini, Sara Beysolow Nyanti, katika eneo la Malakal, nchini humo imebadili mtazamo wa aina ya misaada inayohitajika na wananchi  walioathiriwa na ghasia na majanga ya asili.

Mratibu huyo wa Umoja wa Mataifa wa misaada ya kibinadamu nchini Sudan Kusini  Sara Beysolow Nyanti, ambaye pia ni Naibu Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu katika Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini humo, UNMISS akiongoza ujumbe wa ngazi ya juu ulifika  Malakal, kujionea hali halisi na kuzungumza na wananchi. 
 
Malakal ni eneo maalum ambalo limepewa ulinzi kwa kuwa linahifadhi wakimbizi wa ndani wanaokimbia machafuko katika jimbo la Upper Nile na linaendelea kupokea wakimbizi wapya kila uchao wanaokimbia ghasia na majanga ya asili hali inayozidisha mahitaji ya kibinadamu katika eneo hili. 
  
Akiwa katika eneo hilo alipata maoni ya Martha Steven ambaye ni mwakilishi wa wanawake wakimbizi wa ndani. "Sisi wanawake hatuna kazi za kutuwezesha kupata fedha. Tunakumbana na changamoto nyingi zinazotufanya tukatafute kuni angalau za kutumia na kuuza. Wakati fulani unapokutana na askari mlevi, anaweza kukupiga au kukubaka.” 
 
Mwakilishi wa vijana, kijana Kadila Mayongo akagusia suala la elimu. “Tangu mwaka 2013 hadi sasa vijana wengi, hawajapata fursa ya kwenda Chuo Kikuu au taasisi yoyote ya elimu ya juu. Familia zao hazina uwezo wa kulipa ada. Tunaomba mashirika yaanzishe angalau kituo cha mafunzo ya ufundi stadi, hiyo itakuwa nzuri kwa sisi vijana.” 
 
Pamoja na kuzungukia maeneo kadhaa ya Malakal Ujumbe huo wa Umoja wa Mataifa ulikuwa na vikao kadhaa na makundi mbalimbali yakiwemo ya viongozi wa serikali, asasi za kiraia na makundi maalum na mwisho wa safari yao Bi. Beysolow akazungumza. 
 
Anasema “ninachokiona tunakoelekea huko baadaye ni lazima tubadilishe baadhi ya mambo tunayofanya. Nataka kuona tunafanya kazi zaidi na asasi za kiraia katika eneo hili lakini pia mabadiliko katika utoaji wa fedha taslimu, pamoja na harakati nyingine zihusianazo na utoaji wa fedha taslimu.” 

Mlinda Amani mwanamke akiwa mazoezini huko Malakal, Sudani Kusini
UNMISS\Janet Adongo
Mlinda Amani mwanamke akiwa mazoezini huko Malakal, Sudani Kusini