Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Urusi yakubali UN na ICRC kuhusika katika uhamishaji watu kutoka Mariupol

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres wakati wa mkutano na waziri wa mambo ya nje Sergey Lavrov, Moscow, Urusi.
UN Russia/Yuri Kochin
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres wakati wa mkutano na waziri wa mambo ya nje Sergey Lavrov, Moscow, Urusi.

Urusi yakubali UN na ICRC kuhusika katika uhamishaji watu kutoka Mariupol

Amani na Usalama

Urusi imekubali kuhusika kwa Umoja wa Mataifa katika kuwahamisha raia kutoka eneo la mwisho lililosalia katika mji wa Mariupol wa Ukraine, kufuatia mkutano kati ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres na Rais Vladimir Putin mjini Moscow leo Jumanne. 

Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa ambaye alikuwa katika mji mkuu wa Urusi kwa ajili ya mazungumzo kuhusu vita nchini Ukraine, pia alikutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo, Sergey Lavrov. 

Kwa mujibu wa waraka uliotolewa na Msemaji wa Katibu Mkuu Guterres, wakati wa mkutano wake na Rais Putin, Bwana Guterres amesisitizaa msimamo wa Umoja wa Mataifa kuhusu Ukraine. 

Pia viongozi hao wamejadili mapendekezo ya usaidizi wa kibinadamu na kuondolewa kwa raia kutoka maeneo yenye migogoro, kwa mfano katika mji wa bandari uliozingirwa wa Mariupol, ambako maelfu ya raia na wanajeshi wa Ukraine wamesalia wamejichimbia kwenye kinu cha chuma cha Azovstal. 

"Rais Putin amekubali, kimsingi, kuhusika kwa Umoja wa Mataifa na Kamati ya Kimataifa ya chama cha Msalaba Mwekundu ICRC katika uondoaji wa raia kutoka katika kinu cha Azovstal huko Mariupol." Amesema Msemaji wa Katibu Mkuu, Bwana Dujarric. 

Ameongeza kuwa majadiliano ya ufuatiliaji yatafanywa na ofisi ya Umoja wa Mataifa ya masuala ya kibinadamu, OCHA, na Wizara ya Ulinzi ya Urusi. 

Mapema leo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amezungumza na waandishi wa habari kuhusu pendekezo lake ambalo litashuhudia Umoja wa Mataifa, Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu, na vikosi vya Ukraine na Urusi, kuratibu kazi ya kuwezesha uhamishaji salama wa raia wanaotaka kuondoka Mariupol. 

Ziara ya Katibu Mkuu inafuatia barua za maombi zilizotumwa kwa Urusi na Ukraine wiki iliyopita. 

Bwana Guterres atakuwa mjini Kyiv nchini Ukraine Alhamisi kwa mkutano wa kikazi na Waziri wa Mambo ya Nje Dmytro Kuleba na kisha kupokelewa na Rais Volodymyr Zelenskyy.