Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Je wafahamu mbu walao mbu wenzao?

Mbu aina ya Anopheles akiwa kwenye chandarua. Mbu huyu ndiye aenezaye ugonjwa wa Malaria.
© WHO/S. Torfinn
Mbu aina ya Anopheles akiwa kwenye chandarua. Mbu huyu ndiye aenezaye ugonjwa wa Malaria.

Je wafahamu mbu walao mbu wenzao?

Afya

Hii leo ikiwa ni siku ya kimataifa ya kutokomeza ugonjwa wa Malaria duniani, tunamulika Toxorhynchites aina ya mbu ambaye anakula mbu wengine hususan mbu aina ya Anopheles ambaye anaeneza ugonjwa wa Malaria.

Dokta Jovin Kitau kutoka shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni, WHO nchini Tanzania, ambaye ni mtaalamu wa kudhibiti na kufuatilia ugonjwa Malaria anasema Toxorhynchites wamebainika katika tafiti kuwa wanakula mbu wengine.

“Tafiti zinaonesha kuwa mbu hao wanapokuwa bado ni viluilui wana uwezo wa kula viluilui wa mbu wengine akiwemo aina ya Anopheles ambayo ndio inaambukiza Malaria. Kwa hiyo hizi ni tafiti ambazo zimeweza kuthibitisha kuwa aina hii ya mbu inaweza kuongezwa kama sehemu ya mkakati ya kuzuia mbu waenezao Malaria,” amesema Dokta Kitau akihojiwa na Filbert Alexander wa kituo cha habari cha Umoja wa Mataifa, UNIC jijini Dar es salaam, nchini Tanzania.

Hata hivyo mtaalamu huyo amesema “hakujawa na majaribio ya kutosha ya kuwezesha kutambua kama kweli mbinu hii ya kutumia mbu kula mbu wengine inaweza ikaleta manufaa kwenye kupunguza maambukizi  ya vimelea vya Malaria kutoka kwa mtu mmoja kwenda mwingine kupitia mbu.”

Amesema ni kwa sababu ya kukosekana kwa taarifa na takwimu zinazoweza kuhusianisha moja kwa moja, “kwa maana ya kwamba kupunguza mbu waenezao Malaria kwa kutumia mbu wengine, hii inaifanya kuwa ni mbinu inayoweza kutumika lakini haijafanikiwa kutangazwa sana kama mbinu za kutumia vyandarua na kupulizia dawa za ukoko na kadhalika.”

Je inawezekana kutokomeza Malaria Kiafya, Kisiasa na Kiuchumi?

Alipoulizwa kuhusu harakati za kutokomeza Malaria, Dokta Kitau amegawa hoja hiyo katika maeneo matatu; Kiafya, Kiuchumi na Kijamii.

Kuhusu kiafya, amesema hilo linawezekana kwa kuwa na takwimu sahihi kwani inawezesha serikali kupeleka mbinu za kukabiliana na ugonjwa huo kama vile vyandarua, tiba sahihi na kupuliza dawa za ukoko.

Dkt. Jovin Kitau, mtaalamu wa masuala ya Malaria, WHO Tanzania.
UNIC Dar es salaam
Dkt. Jovin Kitau, mtaalamu wa masuala ya Malaria, WHO Tanzania.

Kutokomeza kisiasa, amesema ni jambo linaweza kuzungumzwa na kubishaniwa, “kwa sababu kutokomeza maambukizi kiafya, hakuna maana ya kwamba kisiasa usilizungumzie kabisa, kwa sababu malaria ni ni ugonjwa unaoambukiza na huwezi kujua ni wakati gani unao kwenye nchi. na kwa hiyo ule mwamko wa kisiasa juu ya utokomezaji wa Malaria na maambukizi yake ni muhimu ukaendelea ukawepo.”

Dokta Kitau amesema “ni kweli unaweza kutokomeza kiafya lakini kutokomeza kisiasa inaweza kuwa si jambo zuri sana kwa kuwa unaondoa kabisa kwenye mazungumzo ya watu na unaondoa kabisa kufanya watu waendelee kulifanya kuwa tatizo linalofahamika.”

Kutokomeza kiuchumi amesema ni jambo linawezekana kwa maana moja “kiuchumi unafanya Malaria lisiwe jambo linalogharimu sekta ya afya au uchumi wa nchi na hiyo ndio maana halisi ya kutokomeza.”

Hata hivyo amesema “bado kiuchumi unaweza kuwa na shughuli kadhaa unafanya ili nchi iwe na uwezo wa kujikinga yasije yakatokea maambukizi ambayo yatashtusha nchi.”