Ukatili wa kutisha na unyanyasaji wa kingono Leer lazima ukome:UNMISS
Ukatili wa kutisha na unyanyasaji wa kingono Leer lazima ukome:UNMISS
Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini (UNMISS) umelaani vikali unyanyasaji na ukatili wa kingono ulioenea, mauaji ikiwa ni pamoja na watu kukatwa vichwa, kuchomwa moto raia wakiwa hai, na mashambulizi dhidi ya wahudumu wa misaada ya kibinadamu katika kaunti ya Leer.
Matukio haya ni miongoni mwa ukiukaji wa haki za binadamu uliorekodiwa wakati wa ongezeko la ghasia zilizotekelezwa na vijana wenye silaha kutoka kaunti za Koch na Mayendit.
Kwa mujibu wa takwimu za timu ya haki za binadamu ya UNMISS ambayo imefanya ziara ya siku 10 ya uhakiki kati ya Februari 17 na Aprili 7 mwaka huu, raia 72 waliuawa, 11 kujeruhiwa, na kesi 64 za unyanyasaji wa kijinsia zilirekodiwa. Taatifa yao iliyotolewa leo inasema manusura wawili wameeleza kubakwa mara kadhaa na kubakwa na magenge ya watu baada ya kutoka mafichoni kwenda kutafuta chakula cha watoto wao.
Mwanamke mwingine ambaye alikuwa amejifungua hivi karibuni amesimulia kwamba alibakwa na kupigwa vibaya kwa siku tatu mfululizo.
"Nimechukizwa sana na mashambulizi haya ya kutisha kwa raia huko Leer. Ni lazima sote tufanye kila tuwezalo kuhakikisha kuwa waathiriwa na manusura wanapata haki wanayostahili na kupata matunzo na usaidizi wanaohitaji,” amesema mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu Sudan Kusini na mkuu wa UNMISS Nicholas Haysom.
Watu 40,000 wafungasha virago kukimbia machafuko
Kulingana na ripoti za awali, za UNMISS takriban watu 40,000 wamekimbia ghasia huko Leer, huku maelfu wakiripotiwa kuvuka mto Nile hadi Fangak katika jimbo la Jonglei. Maelfu ya ng'ombe walivamiwa, na masoko, nyumba, na vifaa vya misaada ya kibinadamu na maghala kuporwa na kuteketezwa.
Msimu wa mvua tayari umeanza, na Umoja wa Mataifa unahofia kuwa pamoja na hatari ya mafuriko, pia hali hiyo itasababisha hatari kwa maelfu ya familia zilizokimbia makazi yao.
Ghasia katika kaunti za Mayendit na Koch, ikiwemo Mirmir Payam, pia zinachunguzwa.
UNMISS imetuma askari wa ziada wa kulinda amani kufanya doria za mara kwa mara, ikiwa ni pamoja na doria za usiku katika mji wa Leer ili kuzuia hasara zaidi za kupoteza maisha.
Walinda amani wanatoa ulinzi kwa watu waliokimbia makazi yao na wasaidizi wa misaada ya kibinadamu wanafika kukidhi mahitaji ya manusura.
Hata hivyo, ulinzi wa raia ni jukumu la kwanza kabisa la Serikali. Na UNMISS imekaribisha hatua za awali zilizochukuliwa katika uundaji wa kamati ya uchunguzi na kutumwa kwa SSPDF kurejesha usalama.
Hatua zichukuliwe haraka kuzuia mashambulizi zaidi
UNMISS inazitaka mamlaka za kitaifa na za kijimbo kuchukua hatua za haraka ili kupunguza mivutano na kuzuia kuongezeka zaidi kwa mashambulizi ya kulipiza kisasi.
Bwana Haysom amesema “Kitendo cha watu kutoadhibiwa kwa ukiukaji wa haki za binadamu lazima kikomeshwe na wahalifu wawajibishwe kwa uhalifu huu wa kutisha,”.
UNMISS pia inashirikiana na uongozi katika ngazi ya mji mkuu na serikali ili kupunguza ghasia wakati timu za masuala ya kiraia zinakutana na jumuiya ili kufanya majadiliano na vikundi mbalimbali katika maeneo yaliyoathiriwa na migogoro.
Akiongeza sauti yake kufuatia machafuko na ukatili huo mratibu wa masuala ya kibinadamu wa Sudan Kusini , Bi.Sara Beysolow Nyanti amesema "Ninalaani vikali ghasia zinazoendelea katika Kaunti ya Leer katika jimbo la Unity, na mizozo na migogoro kote Sudan Kusini. Kuongezeka kwa mapigano mwezi Aprili kumesababisha uharibifu mkubwa, huku watu wengi wakiripotiwa kuuawa, kujeruhiwa, wanawake kutekwa nyara na kubakwa, nyumba kuchomwa moto, na mali kuporwa. Ukatili huu ulitokea wakati wasaidizi wa kibinadamu wakichukua hatua ili kupunguza mateso kutokana na mvua na athari za mafuriko ya 2021 pamoja na shughuli za maandalizi ya kukabiliana na athari za mvua zinazokuja na mafuriko yanayotarajiwa, si haki na lazima vitendo hivyo vikomeshwe".
Tarehe 22 Aprili na 23 Aprili, Bibi Nyanti aliongoza ujumbe wa ngazi ya juu kwenda Bentiu, jimbo la Unity, na Malakal, jimbo la Upper Nile, ili kutathmini hali ya kibinadamu ya watu mashinani na kukutana na watu walioathiriwa na ghasia na majanga ya asili yanayoendelea.
Wajumbe hao wa ngazi ya juu waliwasikiliza wanawake wakielezea uzoefu wao wa kutisha wa ukatili wa kijinsia, masuala ya afya na ukosefu wa elimu.
Baadhi ya wanawake waliokimbia makazi yao na kuathirika na machafuko na mafuriko walisema "Tunabakwa, tunanyanyaswa, hatuna riziki, hatuna fursa, wasichana hawawezi kwenda shule. Machozi yetu ni ya amani. Haya si maisha tuliyochagua”.