24 Aprili 2022
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametuma salamu za rambirambi kwa familia, serikali na wananchi wa Kenya kufuatia kifo cha Rais wa zamani wa taifa hilo la Afrika Mashariki Mwai Kibaki.
Kupitia taarifa fupi iliyotolewa na msemaji wake Jumamosi mjini New York Marekani, Katuibu Mkuu amesema amesikitishwa na taarifa za kifo hicho.
Ameongeza kuwa Rais huyo wa zamani Kibaki atakumbukwa kama kiongozi aliyetoa mchango muhimu katika maendeleo ya Kenya.
Akishikamana na watu wa Kenya Guterres amesema Umoja wa Mataifa utaendelea kufanya kazi kwa karibu na Kenya kuendeleza amani, usalama na maendeleo endelevu katika eneo la Afrika Mashariki na kwingineko.