Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wiki ya chanjo duniani ikianza WHO yachagiza maisha marefu kwa wote 

Chanjo kwa jamii zinazohifadhi wakimbizi Uganda.
© UNICEF/Maria Wamala
Chanjo kwa jamii zinazohifadhi wakimbizi Uganda.

Wiki ya chanjo duniani ikianza WHO yachagiza maisha marefu kwa wote 

Afya

Wiki ya chanjo duniani imeanza leo jumapili aprili 24 na itaenda hadi Aprili 30 huku shirika la afya duniani WHO likichagiza maisha marefu kwa wote ikiwa ndio kaulimbiu ya wiki hiyo kwa mwaka huu. 

WHO inasema lengo kuu la wiki ya chanjo ni kutanabaisha hatua za pamoja zinazohitajika na kupigia upatu matumizi ya chanjo ili kulinda watu wa rika zote dhidi ya magonjwa.WHO inashirikiana nan chi kote duniani kuelimisha thamani ya chanjo na kupata chanjo hizo lakini pia kuhakikisha serikali zinapata muongozo na msaada wa kiufundi kutekeleza programu za chanjo. 

Na nia hasa ya wiki ya chanjo ni kuhakikisha watu wengi zaidi na jamii zao wanalindwa dhidi ya magonjwa yanayoweza kukingwa na kuepukwa kwa kupata chanjo. 

Umuhimu na thamani ya chanjo 

Kwa mujibu wa WHO maisha marefu kwa wote sio ahadi, ni matamanio kwa sababu kila mtu anastahili nafasi ya maisha bora. “Maisha ambayo mtu yuko huru kutafuta furaha na kuangalia nyuma bila kujiuliza je kama ningefanya hivi”. 

WHO inasema chanjo zimekuwa zikiokoa maisha ya mamilioni ya watu tangu mwaka 1796. 

Chanjo ya kwanza ya ndui ilikuwa ni ya mapambano dhidi ya magonjwa na kwa mara ya kwanza, ilimpa kila mtu nafasi ya kuishi na kisha mamia ya chanjo zingine baadaye. 

“Katika karne mbili na robo mabilioni ya watu wameishi maisha marefu zaidi. Wamekuwa na kuwa askari wa zimamoto, madaktari, wanamuziki, akina baba. akina mama, ndugu na kina dada.” 

Shirika hilo linasema huenda “chanjo zisipate sifa kwa busu hilo ya kwanza, kwa goli hilo la ushindi, kwa siku hiyo maalum, kwa kumbatio hilo la mwisho, lakini thamani yake haipimwi tu katika dozi zilizotolewa, ni kwa dakika mtu alizorejeshewa katika maisha na maisha marefu mtu anayoweza kuishi.” 

Kwa mujibu wa shirika hilo la afya, “chanjo hutoa fursa na matumaini kwa sisi sote kufurahia maisha kamilifu zaidi. Na hilo ndilo jambo ambalo sote tunapaswa kulipigania. Chanjo, katika kutafuta maisha marefu tunayoweza kuishi vizuri na maisha marefu kwa wote.”