Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mradi wa FAO na WFP wawanusuru wakulima walioathirika na mabadiliko ya tabianchi Kenya 

Familia za Turkana zinatumia kilimo cha umwagiliaji kulima mazao ya chakula wakati wa ukame wa muda mrefu nchini Kenya.
UNDP/Ngele Ali
Familia za Turkana zinatumia kilimo cha umwagiliaji kulima mazao ya chakula wakati wa ukame wa muda mrefu nchini Kenya.

Mradi wa FAO na WFP wawanusuru wakulima walioathirika na mabadiliko ya tabianchi Kenya 

Tabianchi na mazingira

Kutana na Agnes mkulima kutoka wilaya ya Lodwar kaunti ya Turkana jimbo la Rift Valley nchini Kenya. Mabadiliko ya tabianchi yanayolikumba eneo la Afrika Mashariki kwa kiasi kikubwa yamemuathiri sana yeye na jamii yake, lakini sasa asante kwa mradi wa pamoja wa mashirika ya Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani WFP na la chakula na kilimo FAO wa kuwasaidia wakulima wadogo kujenga mfereji wa maji kwa ajili ya umwagiliaji na kununua mazao yao, maisha ya Agnes na jamii yake yamebadilika.

 

Huyo ni Agnes mama na mkulima wa muda mrefu katika jamii hii ya Lodwar ambayo imeathirika vibaya na mabadiliko ya tabianchi na baada ya dhiki kweli ni faraja, kwani sasa mrejeji uliojengwa kwa msaada wa FAO na WFP unawaletea maji kutoka mtoni ambayo yanaisaidia jamii hii kufanya kilimo cha umwagiliaji mafanikio. Agnes anakumbuka hali ilivyokuwa mbaya, “Kulikuwa na ukame mkali, mbuzi walianza kukonda na kufa, watu walilala njaa, huu sio mwaka mzuri kabisa kwa sababu hata kupanda ndio tunaanza anza kupanda sasa”

Kabla ya kujengewa mfereji WFP imekuwa ikiisaidia jamii hii kwa msaada mbalimbali wa kujenga mnepo dhidi ya mabadiliko ya tabianchi. “Sasa WFP mara ya kwanza walikuja wakatupatia chakula, kila wakati walikuwa wanakuja kutupa chakula na baada ya hapo wakaanzisha FFS mpango wa chakula kwa samani. Tukaanzisha kikundi na baadaye WFP ikaanza kujenga huo mfereji” 

Leo hii Agnes ni mwenye mafanikio anayeweza kupanda na kuuza mazao mbalimbali ya chakula ,“Hapo awali tulikuwa tunalima mtama, mahindi na kunde na hivi karibuni wametuletea viazi vitamu “ 

Hivyo ni vile viazi vya rangi ya njano ambavyo vinatia nguvu, vina vitamini A,C,K na E. Pia vina vitamin B na madini ya magnesium na Potassium. 

Agnes akaamua kuongeza zao lingine la karanga ambalo linahimili ukame na linahitaji maji kidogo.

Na soko sio mtihani tena kwani WFP na FAO wamewatafutia wakulima hawa masoko na wakati mwingine wananunu mazao yao ili kuyatumia kulisha watoto  wenye utapiamlo,“Mimi nafurahi sana tena sana kwa sababu kama mkulima ninaweza kulima karanga zangu na zinunuliwe na kwenda kusaidia Watoto wetu inanipa furaha sana.”