Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mtu 1 kati ya 6 ni mkimbizi wa ndani Ukraine:IOM

Mama na mwanae wakiondoka kituo cha treni cha Lvivi nchini Ukraine.
© UNICEF/Giovanni Diffidenti
Mama na mwanae wakiondoka kituo cha treni cha Lvivi nchini Ukraine.

Mtu 1 kati ya 6 ni mkimbizi wa ndani Ukraine:IOM

Wahamiaji na Wakimbizi

Ripoti mpya iliyotolewa leo na shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji IOM inasema mtu 1 kati ya 6 ni mkimbizi wa ndani nchini  Ukraine na hivyo kuifanya idadi ya watu waliokimbia makazi yao na kusalia wakimbizi wa ndani tangu kuanza kwa mzozo wa Ukraine tarehe 24 mwezi Februari mwaka huu kufikia zaidi ya watu milioni 7.7 sawa na asilimia 17 ya watu wote wa taifa hilo.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo iliyotolewa mjini Geneva Uswisi katika siku 17 za mwanzo wa mwezi huu wa Aprili pekee watu wengine zaidi ya 60,000 wamelazimika kuwa wakimbizi wa ndani nchini Ukraine. 

Hili ni ongezeko la asilimia 19 tangu tathimini ya kwanza iliyochapishwa Machi 16 mwaka huu. 

Asilimia 60 ya wakimbizi hao wa ndani, IOM inasema ni wanawake na zaidi ya nusu ya wakimbizi hao wa ndani wako mashariki mwa Ukraine ambako kunaripotiwa uhaba mkubwa wa chakula, huku familia nyingi zenye watoto wa chini ya umri wa miaka 5 zikiripoti matatizo ya kushindwa kupata chakula cha kutosha kwa ajili ya watoto wao. 

Changamoto kubwa zilizobainiwa na IOM kwa watu hawa ni pamoja na fedha, fursa ya kupata msaada wa fedha, madawa na vifaa vingine vya tiba. 

Mkurugenzi mkuu wa IOM António Vitorino amesema “ Wanawake na Watoto, wazee na watu wenye ulemavu ndio waathirika wakubwa wakiwakilisha kundi lililo katika hatari zaidi. Kazi yetu ni kuwasaidia waliolazimika kukimbia nyumba zao na wote walioathirika ambao wako hatarini, lakini usitishaji wa mapigano ni muhimu sana ili kuruhusu ufikishaji wa misaada ya kibinadamu na kuyafikia maeneo ambayo ni vigumu kufika kutokana na usalama mdogo.” 

Tangu kuanza kwa vita takriban watu 150,000 wameshapokea msaada kutoka IOM ikiwemo chakula, vifaa visivyo chakula, vifaa vya usafi , fedha taslimu, huduma ya afya ya akili na msaada wa kisaikolojia, pia taarifa za kuzuia usafirishaji haramu wa binadamu, ukatili wa kingono na ukatili wa kijinsia.