Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chonde chonde viongozi wa Ukraine na Urusi nipokeeni nakuja tujadili kumaliza vita- Guterres

Majengo yaliyoharibikwa kwa makombora kwenye mji wa Borodianka jimbo la Kyiv nchini Ukraine
© UNDP/Oleksandr Ratushniak
Majengo yaliyoharibikwa kwa makombora kwenye mji wa Borodianka jimbo la Kyiv nchini Ukraine

Chonde chonde viongozi wa Ukraine na Urusi nipokeeni nakuja tujadili kumaliza vita- Guterres

Amani na Usalama

Katika harakati za kusaka suluhu kwenye vita vinavyoendelea nchini Ukraine, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametuma barua kwa viongozi wa Urusi na Ukraine ili aweze kufanya ziara katika nchi mbili hizo.

Taarifa iliyotolewa leo jijini New York, Marekani na msemaji wa Umoja wa Mataifa, Stephane Dujarric, inasema barua hizo ziliwasilishwa jana kwenye ofisi za uwakilishi wa kudumu wa Urusi na Ukraine kwenye Umoja wa Mataifa.

“Katika barua hizo, Katibu Mkuu amemwaomba Rais Vladmir Putin wa Urusi ampokee kwenye mji mkuu wa Urusi, Moscow, na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy ampokee kwenye mji mkuu Ukraine.

Katibu Mkuu amesema katika wakati huu wa kitisho kikubwa na madhara, angelipenda kujadili hatua za haraka za kuleta amani Ukraine na mustakabali wa ushirikiano wa kimataifa kwa kuzingatia misingi ya Chata ya Umoja wa Mataifa na sheria za kimataifa.

Ameeleza kuwa Ukraine na Urusi, zote ni wanachama waasisi wa Umoja wa Mataifa na siku zote wamekuwa waungani thabiti wa taasisi hiyo.

Mapema jana Katibu Mkuu alisihi sitisho la siku nne za mapigano nchini Ukraine ili kutoa fursa siyo tu ya maandalizi ya Pasaka ya waothodoksi bali pia kutoa fursa ya kuzingatia maana ya sherehe ya Pasaka.