Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tunazifuatilia taarifa kuwa Uingereza inataka kuwahamishia nchini Rwanda wasaka hifadhi  

Moja ya mitaa ya mji mkuu wa Rwanda, Kigali
UN/Rick Bajornas
Moja ya mitaa ya mji mkuu wa Rwanda, Kigali

Tunazifuatilia taarifa kuwa Uingereza inataka kuwahamishia nchini Rwanda wasaka hifadhi  

Wahamiaji na Wakimbizi

Kufuatia uwepo wa taarifa za kuwa Uingereza imeingia makubaliano na Rwanda ya kuwahamisha wasaka hifadhi nchini Uingereza na kuwapeleka Rwanda, Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR limesema linaelewa kuwa serikali ya Uingereza inatangaza ushirikiano wa uhamiaji na maendeleo ya kiuchumi na nchi ya Rwanda lakini linahitaji kuyaona makubaliano hayo kwanza kabla ya kutoa maoni.

UNHCR imesema inafuatilia kupata undani wa makubaliano hayo kati ya Uingereza na Rwanda lakini hata kwa kuweka kando suala hili la sasa, kwa kuwa asili ya makubaliano haijafahamika, msimamo wa shirika hilo ni kuwa haliungi mkono taifa moja kuhamishia majukumu yake ya kutunza wasaka hifadhi kwenda katika taifa jingine. 

Hii ni pamoja na hatua zinazochukuliwa na Mataifa kuhamisha wanaotafuta hifadhi na wakimbizi hadi nchi nyingine zenye ulinzi duni wa kulinda haki zao au ambapo hali hii inasababisha kuhamisha majukumu badala ya kushirikiana katika majukumu hayo.   

“Kwa hivyo tunazihimiza serikali kujiepusha na kuanzisha mazoea ambayo yanaweza kuhamishia nje wajibu wao wa kutoa hifadhi.” Imesema taarifa ya UNHCR iliyotolewa leo na msemaji wa shirika hilo Matthew Saltmarsh, kufuatia kuenea kwa taarifa za makubaliano haya kati ya Uingereza na Rwanda.