Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Upimaji na matibabu ni muhimu kuzuia maambukizi ya Chagas toka kwa mama kwenda kwa mtoto:UN

Wadudu wanaopatikana Amerika kusini wanaoaminika kusababisha ugonjwa wa chagas.
CDC/David Snyder
Wadudu wanaopatikana Amerika kusini wanaoaminika kusababisha ugonjwa wa chagas.

Upimaji na matibabu ni muhimu kuzuia maambukizi ya Chagas toka kwa mama kwenda kwa mtoto:UN

Afya

Ikiwa leo ni siku ya ugonjwa wa Chaga, shirika la afya la Umoja wa Mataifa WHO linasema duniani kote inakadiriwa kuwa hadi watu milioni 7 wameambukizwa ugonjwa huu ambao mara nyingi hauna dalili lakini ni tishio kwa maisha ya binadamu endapo hautotibiwa.

Siku hii ambayo huadhimishwa kila mwaka Aprili 14 lengo lake ni kuelimisha kuhusu ugonjwa huu uliopuuzwa ambapo watu zaidi ya asilimia 10% tu walioathirika ndio waliopimwa na asilimia 1% pekee ndio waliopata matibabu yanayostahili.

Kwa mujibu wa WHO mara nyingi hujulikana kama "ugonjwa wa kimyakimya" kwa sababu hauonyeshi dalili au una dalili chache sana.

Shirika hilo limesisitiza haja muhimu ya kuongezeka kwa uchunguzi, ambao ukosefu wake unaleta kikwazo kikubwa cha kuwatunza  na kuwahudumia watu milioni 75 wanaokadiriwa kuwa katika hatari ya kuambukizwa.

Maeneo yaliyoathirika zaidi

Katika ukanda wa Amerika ya Kusini, ambako ni janga, ugonjwa wa Chagas husababisha vifo vingi kila mwaka kuliko ugonjwa wowote wa vimelea ikiwa ni pamoja na malaria.

WHO imeongeza kuwa watu wengi walio katika hatari kubwa ya kuambukizwa ni miongoni mwa jamii za watu maskini zaidi na waliotengwa.

Ugonjwa wa Chagas husababishwa na vimelea vya Trypanosoma crusi, ambavyo huingia kwa binadamu kupitia kuumwa na mdudu wa triatomine, anayejulikana pia kama mdudu anayebusu.

Pia unaweza kuambukizwa  wakati wa kuzaliwa kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto, kwa kuongezewa damu na au kwa kupewa viungo vya mwili vya mtu mwingine aliye na maambukizi.

Waathirika wakubwa

Shirika la Umoja wa Mataifa la kufanikisha upatikanaji wa dawa za tiba kwa gharama nafuu UNITAID limesema, wakati zaidi ya wanawake milioni moja walio katika umri wa kuzaa wakikadiriwa kuambukizwa ugonjwa wa Chagas, kuzuia maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto ni muhimu ili kupunguza kasi ya kuenea kwa magonjwa na kuzuia magonjwa hayo.

Mathalani nchini Brazili Unitaid, inashirikiana na wizara ya afya na wamejitolea kuboresha upatikanaji wa huduma ya vipimo vya bei nafuu, matibabu bora na huduma ya kina kwa wanawake na watoto wao wachanga.

Shirika hilo limeongeza kuwa kwa uchunguzi wa kina na wa mpangilio maalum kwa wanawake na watoto, kazi hii inaweza kupunguza kwa kiasi kikubwa maambukizi na kupunguza idadi ya maambukizi mapya kila mwaka, na hivyo kusaidia kuepusha madhara makubwa na ya gharama kubwa ya afya baadaye maishani.

Katika asilimia 30 ya watu wote walioambukizwa kwa muda mrefu, ugonjwa wa Chagas husababisha matatizo makubwa ya moyo na utumbo ikiwa ni pamoja na kiharusi, mshtuko wa moyo na kifo cha ghafla ikiwa haujatibiwa.

Shirika la afya la nchi za Amerika (PAHO) linakadiria kuwa ugonjwa wa Chagas unachangia zaidi ya dola za Marekani milioni 600 katika gharama zinazohusiana na huduma za afya kila mwaka.

Juhudi za Unitaid, zinazoendelea nchini Brazil, Bolivia, Colombia na Paraguay, zinalenga kuonyesha mbinu mpya za upimaji, matibabu na huduma kwa wagonjwa wa Chagas ambazo zitatoa ushahidi muhimu kuwezesha kupitishwa kwa mikakati ya kiafya inayowezekana na ya gharama nafuu ya kukabiliana na ugonjwa wa Chagas kote nchini, kikanda na kimataifa.

Wakati wagonjwa wengi wanapatikana Amerika ya Kusini , ugonjwa huo unaendelea kusambaa katika maeneo mengine duniani.

Hivi sasa kwa takwimu za WHO watu wamebainika na ugonjwa wa Chagas katika nchi 44 kwenye bara la Amerika, Afrika, Asia, Ulaya na Ocenia ambalo pia hujulikana kama Australia.