Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Janga la njaa lanyemelea Somalia- UN

Mtoto mwenye umri wa miezi 7 akichnguzwa utapiamlo unaochochewa na ukame mkali nchiin Somalia.
© UNICEF/Sebastian Rich
Mtoto mwenye umri wa miezi 7 akichnguzwa utapiamlo unaochochewa na ukame mkali nchiin Somalia.

Janga la njaa lanyemelea Somalia- UN

Msaada wa Kibinadamu

Mashirika ya Umoja wa Mataifa yameonya kuwa janga lingine la njaa kama la mwaka 2011 linanyemelea Somalia iwapo wahisani hawataongeza ufadhili wao kwa ombi la usaidizi wa kibinadamu kwa taifa hilo la pembe ya Afrika kwa kuwa ukame wa muda mrefu sambamba na ongezeko la bei za vyakula vimeongeza idadi ya wasio na uhakika wa chakula kufikia watu milioni 6, sawa na asilimia 40 ya wananchi wote. 

Mashirika hayo ya Umoja wa Mataifa, lile la chakula na kilimo, FAO, Mpango wa chakula duniani, WFP na la kuhudumia watoto, UNICEF yametoa onyo hilo kupitia taarifa iliyotolewa leo mjini Mogadishu, Somalia.

Ukame wa muda mrefu unaendelea kuvuruga maisha ya jamii na mbinu zao za kujipatia kipato huku kasi ya mahitaji ikizidi ile ya upatikanaji wa misaada ya kibinadamu.

Takwimu za leo za watu milioni 6 kuwa kwenye viwango vya juu vya ukosefu wa chakula zinatokana na ripoti mpya ya tathmini ya uhakika wa kupata chakula, IPC ambapo inasema hali inaweza kuwa mbaya zaidi katika maeneo sita ya Somalia.

Kiwango hicho ni ongezeko maradufu ikilinganishwa na takwimu za mwanzo wa mwaka huu.
Mratibu wa masuala ya kibinadamu Somalia, Adam Abdemoula anasema “kiwango hicho kinatia sana shaka na kinapaswa kuwa onyo kuu kuona iwapo ni kweli tuliposema mwaka 2011 janga hili lisitokee tena tulimaanisha au la!”

Ombi la usaidizi kwa Somalia kwa mwaka huu n idola bilioni 1.5 lakini hadi sasa kilichopatikana ni asilimia 4.4 pekee.

Bila fedha hizo kupatikana, takribani watoto milioni 1.4 watakabiliwa na utapiamlo mkali hadi mwisho wa mwaka huu, huku robo yao au 330,000 wakitabiriwa kupata unyafuzi au utapiamlo uliopitiliza.
Mwakilishi wa WFP nchini Somalia, El-Khidir Daloum anasema wanachosubiri kuanza kufanya ni kuhamisha chakula kutoka kwa wenye njaa na kupelekea wale walio hatarini kufa kwa njaa.

Mwezi Julai mwaka 2011 Umoja wa Mataifa ulitangaza janga la njaa katika majimbo mawili nchini Somalia, janga ambalo kwa kiasi kikubwa lilisababishwa na ukame.