Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu
Mfanayakazi katika kampuni ya Africa Collext Textiles.

Kampuni ya Kenya na namna inavyosaidia kukabiliana na taka za nguo

UNEP/Ahmed Nayim Yussuf
Mfanayakazi katika kampuni ya Africa Collext Textiles.

Kampuni ya Kenya na namna inavyosaidia kukabiliana na taka za nguo

Tabianchi na mazingira

Sekta ya nguo inachangia kati ya asilimia 2 na 8 ya gesi chafuzi duniani. Uzalishaji wa kilo moja ya vitambaa unatumia zaidi ya nusu kilo ya kemikali na hutumia maji safi mengi.

Duniani kote dola bilioni 460 hupotea kila mwaka kwa ajili ya utupaji wa nguo ambazo bado zinaweza kuvaliwa. 

Ili kukabiliana na changamoto hiyo Shirika la Umoja wa Mataifa la mazingira, UNEP linatekeleza mradi wa miaka mitatu unaofadhiliwa na muungano wa Ulaya kwa ajili ya kuinua utaratibu wa biashara bunifu katika mnyororo wa nguo kwa lengo la kusaidia katika kudhibiti uchafuzi wa mazingira na kuinua maisha ya watu. 

Moja ya kampuni inayoshiriki katika mradi huo ni Africa Collect Textiles ambayo imeunda mfumo wa biashara, na kupima athari za kimazingira wanazosababisha na kubuni mbinu za kutumia taka za nguo kutengeneza bidhaa nyingine ikiwemo mikeka na midoli. 

Alex Musembi ni mwanzilishi mwenza wa kampuni ya Africa Collect Textiles, “Watu wanaotoa msaada wa nguo Ulaya nadhani wanafikiri kwamba nguo hizo zinatolewa kwa Afrika bila malipo yoyote. Nguo hizo hukaguliwa Ulaya kwa viwango na viwango vya chini kabisa hutumwa Afrika na mwisho wa siku nguo hizo huishia kwenye majalala na pia kwenye mito na baharí. Fursa ya kuokota taka za nguo ni kwa ajili ya kuzichakata tena.” 

Kampuni hiyo ya Africa Collect Textiles imeweka vibada ambavyo watu wanaweza kutupa nguo ambazo wamekwishatumia na kisha baada ya kujaa zinapelekwa kwenye kiwanda ambapo wanatengeneza vitu ikiwemo mikeka na pia wanazitumia kutengeneza nyuzi na bidhaa mpya ambazo zinarejeshwa kwenye soko.

Profesa Josephat Igadwa Mwasiaga ni mpelelezi mkuu wa mradi wa UNEP wa inTex chuo kikuu cha Moi, Kenya. “Sekta ya nguo ni moja ya sekta ambazo zinachangia uchafuzi, huenda pamba inakuzwa barani Afrika, inachakatwa Asia na nguo zinatengenezwa na kutumwa barani Ulaya. Baada ya kutumiwa bara Ulaya zinatumwa barani Afrika kwa matumizi ya mara ya pili ambapo baada ya hapo zinachomwa au kurundikwa kwenye majalala”.

Kwa upande wake bwana Musembi anasema bidhaa  zao ni zaidi ya bidhaa kwani. “Wakati mteja ananunua bidhaa zetu, sio tu kwamba ananunua bidhaa nzuri lakini pia ananunua hadithi ya mashirika kama vile UNEP, muungano wa Ulaya. Taasisi za mitaa na serikali ni lazima wamulike suala la taka za nguo kwa sababu ni changamoto ya dunia nzima kwa hiyo ni lazima tuwe na mtazamo wa kimataifa na suluhu za kimataifa.”