UN yazindua mpango wa kuijengea mnepo Ukraine na watu wake

11 Aprili 2022

Mpango wa maendeleo unaoongozwa na Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Ukraine umezinduliwa leo Jumatatu, ili kutoa msaada wa haraka wa kiuchumi na usaidizi wa muda mrefu kwa mamilioni ya watu walioachwa wakihangaika kukidhi mahitaji ya msingi, kutokana na uvamizi wa Urusi. 

Shirika la mpango wa maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) linalenga kukabiliana na uharibifu ambao umesababishwa na mashambulizi ya makombora katika miji mbalimbali na makadirio ya mapema kwamba maendeleo ya kiuchumi katika miongo miwili ijayo yanaweza kupotea, ikiwa vita vitaendelea. 

Tangazo hilo limekuja wakati Benki ya Dunia imetoa tahadhari kwamba uchumi wa Ukraine unatazamiwa kushuka kwa asilimia 45 mwaka huu, kwa sababu ya vita. 

Kwa kuathiriwa na vikwazo ambavyo havijawahi kushuhudiwa, uchumi wa Urusi tayari umeingia katika mdororo mkubwa na matokeo yanatarajiwa kuupunguuza kwa asilimia 11.2 mnamo 2022, imesema Benki ya Dunia. 

UN itaendelea kuisaidia Ukraine 

"Vita vya Ukraine vinaendelea kusababisha mateso makubwa kwa binadamu huku watu tisa kati ya 10 wakiwa katika hatari ya kutumbukia katika umaskini," amesema Achim Steiner, mkuu wa UNDP na kuongeza kuwa "Kama sehemu ya hatua zilizoratibiwa na Umoja wa Mataifa, UNDP ina dhamira ya kuendeleakusalia Ukraine na kutoa msaada kwa ajili ya watu wa taifa hilo”. 

Ingawa hakuna ubishi dhidi ya mateso makubwa ya kibinadamu ambayo uvamizi wa Urusi umesababisha Ukraine, mkuu wa UNDP, Achim Steiner, amesisitiza kuwa ni muhimu kuhakikisha kuwa uchumi wa ndani unaendelea kufanya kazi na kwamba maisha ya watu yanalindwa. 

Shukrani kwa uwepo wa muda mrefu wa UNDP kote nchini Ukraine, ina miundombinu ya kusaidia hatua za dharura za Serikali na utoaji wa huduma muhimu za umma. 

Kuna mkazo mahususi katika kuwasaidia watu walio katika mazingira magumu zaidi nchini Ukraine katika ngazi ya jamii, hasa wanawake wote walio katika hatari ya kubwa ya unyanyasaji, ikiwa ni pamoja na unyanyasaji wa kingono unaohusiana na migogoro. 

Ili kusaidia kuwawezesha wanawake na wasichana, UNDP inasisitiza kwamba lazima wawe na haki ya kupata mahitaji ya msingi na usaidizi wa kimaisha ikiwa ni pamoja na usaidizi wa kibiashara na upatikanaji wa fedha, mitandao na masoko. 

Mpango wa shirika hilo pia unalenga kukidhi mahitaji ya haraka ya kibinadamu kwa kutumia "mtaji wa binadamu, uwezo wa kiuchumi na maliasili" wa Ukraine, na kuimarisha jumuiya ya kiraia kusaidia kutetea haki za binadamu kwa "ushirikishwaji, ulinzi na uwezeshaji" wa watu katika kujikwamua, limesema shirika hilo la maendeleo la UNDP. 

Changamoto ya kikanda 

Nje ya Ukraine, athari za uvamizi wa Urusi tayari zimetafsiriwa kwa wasiwasi mkubwa miongoni mwa wahudumu wa kibinadamu kuhusu uhaba wa chakula duniani, kwani uzalishaji wa nafaka nyingi na vyakula vingine vikuu nchini Ukraine umeathiriwa. 

Vikwazo kwa Moscow pia vimeathiri uchumi duniani kote, kulingana na Benki ya Dunia, ambayo imesema kuwa masoko yanayoibukia na nchi zinazoendelea barani Ulaya na Asia ya Kati yanatarajiwa kubeba mzigo mkubwa. 

Katika taarifa yake ya hivi karibuni ya kiuchumi, Benki ya Dunia ilitabiri kuwa uchumi wa eneo hilo ulitarajiwa kushuka kwa asilimia 4.1 mwaka huu, ikilinganishwa na utabiri wa kabla ya vita wa asilimia tatu ya ukuaji. 

"Huku kunawez kuwa ni kusinyaa kwa mara ya pili kwa uchumi katika miaka mingi, na kukubwa mara mbili ya kuporomokoka kwa uchumi kulikosababishwa na janga la COVID-19 mwaka 2020,"  

TAGS:UNDP, Benki ya Dunia, Ukraine, uchumi, vita, COVID-19 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter