Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu
Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Ulimwenguni limezitaka nchi kujenga ulimwengu mzuri na wenye afya zaidi baada ya COVID-19.

Mabadiliko yanahitajika ili kulinda afya ya sayari ambayo afya ya binadamu inategemea-WHO

WHO/L. Pezzoli
Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Ulimwenguni limezitaka nchi kujenga ulimwengu mzuri na wenye afya zaidi baada ya COVID-19.

Mabadiliko yanahitajika ili kulinda afya ya sayari ambayo afya ya binadamu inategemea-WHO

Afya

Shirika la afya  la Umoja wa Mataifa  WHO limetoa wito wa dharura wa hatua za haraka za viongozi na watu wote kuhifadhi na kulinda afya na kupunguza janga la mabadiliko ya tabianchi kama sehemu ya kampeni ya "Sayari yetu, afya yetu" kuadhimisha siku ya afya, ambayo inafanyika wakati kukishuhudiwa mzozo mkubwa na udhaifu.

Katika wito wake wa kuchukua hatua, WHO imetanabaisha kuwa asilimia 99 ya watu hupumua hewa isiyofaa hasa inayotokana na kuchomwa kwa mafuta ya kisukuku. 

Ulimwengu ulioghubikwa na joto unashuhudia mbu wakieneza magonjwa zaidi na haraka kuliko hapo awali. Matukio makubwa ya mabadiliko ya tabianchi, upotevu wa bayoanuai, uharibifu wa ardhi na uhaba wa maji vinasababisha watu kuhama makwao na kuathiri afya zao. 

Pia shirika hilo linasema uchafuzi wa mazingira na plastiki hupatikana chini kabisa ya bahari zetu, na kwenye milima mirefu zaidi, na zimeingia kwenye mnyororo wa chakula na mkondo wa damu.

Mifumo inayozalisha vyakula na vinywaji vilivyosindikwa na, visivyo na afya na vinywaji vinavyosababisha wimbi la utipwatipwa, vinaongeza visa vya magonjwa ya saratani na magonjwa ya moyo huku ikizalisha hadi theluthi moja ya utoaji wa gesi chafuzi duniani.

Janga la kiafya na kijamii vinahatarisha uwezo wa watu kuchukua udhibiti wa afya na maisha yao. 

Taarifa hiyo  imemnukuu Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt. Tedros ASdhanom Ghebreyesus akisema, “Janga la mabadiliko ya tabianchi ni janga la kiafya: chaguo zisizo endelevu ambazo zinaua sayari yetu zinaua watu". Ameongeza kwamba, "tunahitaji suluhu za mageuzi ili kuufanya ulimwengu kuachana na uraibu wa nishati ya mafuta, kufikiria upya uchumi na jamii zinazozingatia ustawi, na kulinda afya ya sayari ambayo afya ya binadamu inategemea." 

Janga la COVID-19 limeweka bayana ukosefu wa usawa ulimwenguni kote, imesem taarifa hiyo ikisisitiza udharura wa kuunda jamii endelevu, zenye ustawi ambazo hazikiuki mipaka ya kiikolojia na ambazo zinahakikisha kuwa watu wote wanapata vifaa vya kuokoa maisha na kuboresha maisha, mifumo, sera na mazingira. 

Muongozo wa WHO wa kuhakikisha urejeshaji wa afya na ulinzi wa mazingira kutoka kwenye janga la COVID-19 unapendekeza kulinda na kuhifadhi mazingira kama chanzo cha afya ya binadamu; kuwekeza katika huduma muhimu kama vile maji, huduma za kujisafi mpaka nishati safi katika vituo vya afya; kuhakikisha mpito wa nishati yenye kuzingatia afya; kukuza mifumo ya chakula yenye afya na endelevu; kujenga miji yenye afya na ambayo watu wanaweza kuishi; na kusitisha matumizi ya pesa za walipa ushuru kufadhili uchafuzi wa mazingira. 

Mkataba wa Geneva wa ustawi umetanbaaisha ni ahadi gani za kimataifa zinahitajika ili kufikia matokeo sawa ya afya na ya kijamii sasa na kwa vizazi vijavyo, bila kuharibu afya ya sayari yetu. 

Kupitia kampeni yake ya Siku ya Afya Duniani, WHO inatoa wito kwa serikali, mashirika na raia kushirikiana katika hatua wanazochukua kulinda sayari na afya ya binadamu.