Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Zaidi ya watoto milioni 6 wako hatarini kwa utapiamlo Sahel:UN 

Hatua za haraka zinahitajika kwa ajili ya kukabiliana na suala la utapiamlo Afrika Magharibi na Kati.
UNICEF/UN0594520/Dejongh
Hatua za haraka zinahitajika kwa ajili ya kukabiliana na suala la utapiamlo Afrika Magharibi na Kati.

Zaidi ya watoto milioni 6 wako hatarini kwa utapiamlo Sahel:UN 

Afya

Mwaka huu wa 2022, takriban watoto milioni 6.3 wenye umri wa miezi 6 hadi miezi 59 katika nchi 6 za ukanda wa Sahel wataathirika na tatizo la uzito mdogo ikilinganishwa na urefu wao na hivyo kuweka maisha ya watoto wasiopungua 900,000 hatarini, linaonya kundi la wataalamu wa kufuatilia lishe katika nchi zilizoko Afrika Magharibi na Kati.  

Kundi hilo la wataalamu linaloundwa na mashirika ya Umoja wa Mataifa kama vile UNICEF, WFP, WHO na wadau wengine kama Concern na Save the Children, linatoa wito kwa wafadhili na washirika wao kuongeza msaada wao haraka ili kukabiliana na mahitaji ya haraka ya lishe ya watoto walioathiriwa huku wakiimarisha hatua za kuzuia ili kukabiliana na sababu kuu za utapiamlo wa watoto katika eneo hilo.   

Idadi ya watoto chini ya umri wa miaka 5 wanaotarajiwa kukumbwa na utapiamlo duniani mwaka huu haijawahi kuwa kubwa kiasi hicho, ikionesha ongezeko la asilimia 27 ikilinganishwa na mwaka 2021 na asilimia 62 ikilinganishwa na mwaka 2018 na hiki ni kiwango cha juu kwa mwaka wa tano mfululizo. 

UNICEF inataka kukabiliana kiini cha utapiamlo kwa watoto 

Likikabiliwa na ongezeko kubwa la idadi ya watoto wenye utapiamlo katika miaka ya hivi karibuni  katika eneo hilo la Sahel, Umoja wa Mataifa na washirika wake wanasisitiza haja ya kuchukuliwa hatua za haraka sio tu kuokoa maisha, bali pia kuzuia watoto kupata utapiamlo. 

Kwa hivyo, Kikundi kinatoa wito kwa wafadhili na washirika kuongeza msaada wao haraka ili kukidhi mahitaji ya haraka ya lishe ya watoto walioathiriwa na kuongeza hatua za kuzuia ili kushughulikia sababu kuu za utapiamlo wa watoto. 

"Wakati umefika wa kukabiliana na chanzo kikuu cha utapiamlo wa watoto katika eneo hilo, kwa uharaka na dhamira kuu", amesema Bi. Poirier, akibainisha kuimarika kwa juhudi katika kukabiliana na migogoro ya mara kwa mara iliyobainika katika muongo uliopita . 

Baada ya COVID-19, mzozo wa Ukraine waleta hofu 

Ukosefu wa usalama na matukio mabaya ya mabadiliko ya tabianchi yanazidisha hali ambayo tayari ni tete na ya hatari na kusababisha watu wengi kuhama makazi yao.  

Kufikia mwisho wa 2021, zaidi ya watu milioni 2.5 walikuwa wakimbizi wa ndani katikati mwa Sahel imesema taarifa hiyo. 

Pia katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, ongezeko kubwa la mashambulizi ya kutumia silaha dhidi ya jamii, shule, vituo vya afya na taasisi nyingine za umma na miundombinu limetatiza maisha na upatikanaji wa huduma za kijamii. 

Umoja wa Mataifa unasema kana kwamba hayo hayatoshi janga la Covid-19 linaendelea kuwa na athari mbaya kwa maisha ya kaya na pia mifumo ya chakula, afya, elimu, na ulinzi wa kijamii. 

Na sasa mgogoro wa Ukraine unaweza kusababisha kupungua kwa muda mrefu kwa mauzo ya chakula nje ya nchi na kuongeza idadi ya watu wenye lishe duni katika eneo la Afŕika Kusini mwa Jangwa la Sahaŕa, kulingana na makadirio ya shirika la Umoja wa Mataifa la chakula na kilimo FAO

Zaidi ya hayo, takwimu juu ya kuzuia utapiamlo mkali kwa watoto wenye umri wa miezi 6-23 na wanawake wajawazito na wanaonyonyesha kupitia ulishaji wa ziada katika nchi tisa za eneo hilo zinaonyesha kuwa ufadhili wa haraka unahitajika pia ili kuhakikisha mwitikio mzuri na wa haraka. 

Mahitaji ya jumla ya ufadhili ni zaidi ya dola milioni 93, kukiwa na pengo la ufadhili la dola milioni 56, ikijumuisha dola milioni 26 za kugharamia mahitaji wakati wa msimu wa muambo kuanzia Juni hadi Septemba. 

Kwa matibabu ya utapiamlo uliokithiri au unayafuzi , pengo la ufadhili ni dola milioni 35.5 na kwa utapiamlo uliokithiri na wa wastani.  

Ikiwa ni pamoja na nchi kama Nigeria, ambapo upungufu huu ni dola milioni 42 kwa utapiamlo mkali, wa aina mbaya zaidi ya utapiamlo.