Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ni wakati wa kutokomeza jinamizi la mabomu ya kutegwa ardhini:Guterres 

Mfanyakazi wa UNMAS akichunguza mabomu ya kutegwa ardhini, jimbo la Equatoria kati, Sudan Kusini.
© UN Photo/Isaac Billy
Mfanyakazi wa UNMAS akichunguza mabomu ya kutegwa ardhini, jimbo la Equatoria kati, Sudan Kusini.

Ni wakati wa kutokomeza jinamizi la mabomu ya kutegwa ardhini:Guterres 

Amani na Usalama

Ingawa zaidi ya mataifa 160 yametia saini mkataba wa kihistoria wa kupiga marufuku mabomu ya ardhini, hatua zaidi bado zinahitajika ili kuwalinda watu dhidi ya silaha hizi zenye athari kubwa amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres. 

Katika ujumbe wake wa siku ya kimataifa ya uelimishaji na usaidizi wa hatua dhidi ya mabomu ya kutegwa ardhini inayoadhimishwa leo Aprili 4 Katibu Mkuu, amezihimiza nchi zote kujiunga na mkataba huo wa mwaka 1997. 

Amesema "Mabomu ya kutegwa ardhini, mabaki ya silaha za vita na vilipuzi vinaendelea kuua au kujeruhi maelfu ya watu kila mwaka ambapo wengi wao ni Watoto."  

Mwishoni mwa wiki, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF, liliripoti kwamba watoto watano msichana mmoja na wavulana wanne waliuawa siku ya Ijumaa wakati vilipuzi vya mabaki ya silaha za vita yalipolipuka katika wilaya ya Marjah, mkoa wa Helmand nchini Afghanistan.  

Mvulana na msichana mwingine pia walijeruhiwa. 

Mohamed Ag Ayoya, mwakilishi wa UNICEF nchini Afghanistan, ameonya kwamba hii ni mbali na kuwa kesi ya pekee. 

"Nchini Afghanistan, katika kipindi cha miezi saba iliyopita, watoto 301 ama waliuawa au kujeruhiwa na mabaki ya milipuko ya silaha za vita na mabomu ya kutegwa ardhini. Idadi halisi inadhaniwa kuwa kubwa zaidi," amesema. 

Kazi ya kugundua mabomu ya kutegwa ardhini Syria.
© UNMAS/Asso Sabahaddin
Kazi ya kugundua mabomu ya kutegwa ardhini Syria.

Mamilioni yako katika hifadhi 

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mastaifa Antonio Guterres amekariri kwamba miaka 30 iliyopita, wanaharakati waliungana kuzindua kampeni ya kimataifa ya kupiga marufuku mabomu ya kutegwa ardhini na ndani ya miaka mitano, mkataba wa kupiga marufuku mabomu ya kutegwa ardhini ulizunduliwa na kuanza kutiwa saini. 

Tangu wakati huo, zaidi ya mabomu ya kutegwa ardhini milioni 55 yameharibiwa, na zaidi ya nchi 30 ulimwenguni kote zimetangazwa kuwa hazina tena mabomu ya kutgwa ardhini,  na majeruhi pia wamepungua kwa kiasi kikubwa. 

"Lakini dunia bado imejaa mamilioni ya mabomu ya ardhini yaliyorundikwa na zaidi ya nchi 50 bado zinathiriwa na silaha hizi za hatari” amesema katibu mkuu. 

Kuchelewesha misaada Ukraine 

Bwana Guterres amesisitiza haja ya ulinzi zaidi kwa "watu wanaoishi chini ya kivuli cha vifaa vya milipuko" katika nchi zmbalimbali zikiwemo Syria, Somalia, Afghanistan, Myanmar, na kwingineko. 

"Nchini Ukraine, ndani ya mwezi mmoja wa vita katika mfumo wa silaha ambazo hazijalipuka, mabomu ya kutegwa ardhini, na mabomu mengine itachukua miongo kadhaa kuyakabili, na hivyo tyatakuwa yanatishia maisha muda mrefu baada ya mitutu ya bunduki kunyamaza," ameongeza Katibu Mkuu. 

"Tayari leo, wanazuia utoaji wa msaada wa dharura wa kibinadamu na kuzuia watu kukimbilia usalama." 

Uwekezaji katika ubinadamu 

Katibu Mkuu aliita hatua ya kukabiliana na mabomu ya kutegwa ardhini kama "uwekezaji kwa ubinadamu. Ni sharti la juhudi za misaada ya kibinadamu na msingi wa amani ya kudumu na maendeleo endelevu." 

Ametoa wito kwa mataifa yote kukubaliana na mkataba huo bila kuchelewa, akiongeza kuwa wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hasa, wana wajibu maalum. 

Nchi tano zilizo na hadhi ya kudumu ni China, Ufaransa, Urusi, Uingereza na Marekani. 

"Katika Siku hii ya kimataifa, hebu tuendeleze maendeleo yaliyopatikana na kuondokana na janga la mabomu ya kutegwa ardhini mara moja na kwa wote,"  

Uwanja Salama, Hatua Salama, nyumbani Salama 

Siku ya uhamasishaji kuhusu mabomu ya kutegwa ardhini mwaka 2022 inaadhimishwa chini ya kaulimbiu “Uwanja Salama, Hatua Salama, nyumbani Salama’. Huduma ya Umoja wa Mataifa ya Kushughulikia mabomu ya kureghwa ardhini na vifaa vingine vya milipuko ambayo ni mabaki ya silaha za kivita (UNMAS) imeeleza umuhimu. 

‘Uwanja Salama’ inarejelea dhana ya kusafisha mabomu kutoka ardhini ili kuifanya kuwa salama kwa maendeleo, huku ‘Hatua Salama’ ikiwa na maana mbili. Inaangazia woga ambao watu wanahisi kusogea na bila kujua kama watalipua moja ya silaha hizi, pamoja na taratibu zinazotumiwa na wateguzi wa mabomu ya kutegwa ardhini wanapokaribia maeneo yaliyochafuliwa. 

Kipengele cha mwisho, ‘Nyumbani Salama’, kinalenga katika kurejesha usalama wa kibinafsi wa watu na jumuiya, katika mipangilio ya baada ya migogoro. 

"Hakuna mahali kama nyumbani, na ni vigumu kujisikia nyumbani bila usalama na jamii," imesema UNMAS. 

Hatari bado ipo Somalia 

Na mpango wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia UNSOM umesema mabaki ya vilipuzi vya silaha za vita na mabomu ya kutegwa ardhini yameendelea kuleta athari kubwa kwa raia wa Somalia na hivyo umeahidi msaada wake kwa taifa hilo la Pembe ya afrika kuhakikisha linakuwa huru na mabomu hayo ya ardhjini na vilipuzi vingine.  

Katika ujumbe wake wa siku hii mkuu wa UNSOM James Swan amesema mwaka 2021 pekee watu 669 waliuawa na kujeruhiwa kutokana na mabaki ya silaha za kivita ikiwemo mabomu ya kutegwa ardhini. Pia amesema mabomu hayo ni tishio kubwa la usalama, na yanaathiri shughuli za maendeleo.