Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mabilioni ya watu wanaendelea kuvuta hewa isiyo salama kwa afya zao:WHO 

Uchafuzi wa hali ya hewa unaosababisha madhara ya kiafya kote ulimwenguni ikiwemo, New Delhi India
UN india
Uchafuzi wa hali ya hewa unaosababisha madhara ya kiafya kote ulimwenguni ikiwemo, New Delhi India

Mabilioni ya watu wanaendelea kuvuta hewa isiyo salama kwa afya zao:WHO 

Afya

Karibu watu wote duniani, asilimia 99 wanavuta hewa isiyo salama iliyopita viwango vya ubora wa hewa vilivyowekwa na shirika la afya la Umoja wa Mataifa WHO na hivyo kutishia afya zao.  

Hii ni kwa mujibu wa takwimu mpya zilizotolewa leo na shirika hilo ambazo pia zinasema zaidi ya miji 6,000 katika nchi 117 duniani sasa inafuatilia ubora wa hewa, lakini watu wanaoishi katika miji hiyo bado wanavuta hewa isiyo na ubora unaotakiwa ikiwa na chembechembe za uchafu na hewa ya nitrogen dioxide, huku wale wanaoishi katika nchi za kipato cha chini na cha kati wakiathirika zaidi.   

Takwimu hizo za utafiti mpya zimelifanya shirika la WHO kuelezea umuhimu wa kukabililiana na matumizi ya mafuta kisukuku na kuchukua hatua zingine madhubuti za kupunguza viwango vya uchafuzi wa hewa.  

Kwa mujibu wa shirika hilo la afya duniani twakimu hizi mpya lazima zitie shinikizo ya kuelekea mabadiliko ya nishati. 

“Bei ya juu ya mafuta kisukuku, usalama wa nishati na udharura wa kushughulikia changamoto mbili za afya za uchafuzi wa hewa na mabadiliko ya tabianchi unasisitiza haja ya haraka ya maendeleo ya haraka kuelekea ulimwengu usiotegemea sana nishati ya mafuta kisukuku.” Amesema Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus, mkurugenzi mkuu wa WHO. 

Nchi zinazoendelea ndio wanaathiriwa zaidi na uchafuzi wa hewa 

Katika nchi 117 ambazo zinafuatilia ubora wa hewa WHO imegundua kwamba ubora wa hewa katika asilimia 17% ya miji katika nchi za kipato cha juu uko chini ya miongozo ya ubora wa hewa ya WHO ambao ni hewa kwa chembe nzuri (PM2.5 au PM10).  

Na nchi za kipato cha chini na cha kati bado zinakabiliwa na viwango hatari vya chembe chembe chafu za hewa kuliko wastani wa kimataifa. 

Hata hivyo, mifumo ya hewa ya nitrogen dioxide ni tofauti, ikionyesha pengo ndogo kati ya nchi za kipato cha juu na nchi za kipato cha chini na cha kati.  

Katika nchi za kipato cha chini na cha kati, chini ya 1% ya miji ndio ina hewa ambayo ina viwango vinavyopendekezwa na WHO. 

Kwa ujumla, watu katika nchi zinazoendelea ndio wanaokabiliwa zaidi na uchafuzi wa hewa.  

Pia ni asilimia ndogo tu ya watu ndio walio na ulinzi linapokuja suala la kipimo cha ubora wa hewa, japo hali inaboreka. 

Zaidi ya hayo, ushahidi kuhusu madhara ya uchafuzi wa hewa kwa mwili wa binadamu umeongezeka kwa kasi na kudhihirisha madhara makubwa yanayotokana na hata viwango vya chini vya vichafuzi vingi vya hewa. 

Uchafuzi wa hewa kutoka kwa viwanda unachangia katika kuongeza nyuzi joto.
Unsplash/Maxim Tolchinskiy
Uchafuzi wa hewa kutoka kwa viwanda unachangia katika kuongeza nyuzi joto.

Zaidi ya vifo milioni 13 hutokana na sababu zinazoweza kuzuilika za mazingira 

Twakwimu hizo mpya za WHO zinasema chembe chembe, hasa PM2.5, zinaweza kupenya ndani kabisa ya mapafu na kwenye mkondo wa damu, na kusababisha magonjwa ya moyo na mishipa, kiarusi na matatizo ya kupumua. 

Wakati huo huo, hewa ya nitrogen dioxide inahusishwa na magonjwa ya kupumua, hasa pumu au athma.  

Pia husababisha dalili za matatizo mengine ya upumuaji kama vile kukohoa, kuhema, au kupumua kwa shida, kulazwa hospitalini, na kupelekwa katika chumba cha huduma za dharura. 

Kwa mujibu wa WHO, zaidi ya vifo milioni 13 duniani kote kila mwaka vinatokana na sababu zinazoweza kuzuilika, ikiwa ni pamoja na vifo milioni 7 vinavyohusiana na uchafuzi wa hewa. 

"Baada ya kunusurika na janga la COVID-19, haikubaliki kuendelea kuorodhesha vifo milioni 7 vinavyoweza kuzuilika na miaka mingi ya madhara ya kiafya inayoweza kuepukika kutokana na uchafuzi wa hewa. Uwekezaji mwingi bado unatolewa kwa mazingira machafu badala ya hewa safi na yenye afya,” amesema katika taarifa yake Dkt. Maria Neira, mkurugenzi wa mazingira, mabadiliko ya tabianchi na afya katika  shirika la WHO. 

Mapendekezo ya WHO kuboresha ubora wa hewa na afya 

WHO inatoa wito wa kuimarishwa haraka hatua kwa vitendo ili kuboresha ubora wa hewa.  

Lengo ni kubainisha vyanzo vya uchafuzi wa hewa angani. WHO pia inapendekeza kuunga mkono hatua za kuhamia kwenye matumizi ya kipekee ya nishati safi majumbani kwa ajili ya kupikia, kupasha joto nyumba na taa. 

Shirika hilo la Umoja wa Mataifa linataka kuanzishwa kwa mifumo salama na nafuu ya usafiri wa umma na mitandao inayofaa kwa watembea kwa miguu na waendesha baiskeli.  

Hii ni pamoja na kuhakikisha masharti makali katika suala la ufanmisi na usimamizi wa uzalishashi wa hewa chafuzi itokanayo na magari 

Hii pia inahusisha kuwekeza katika nyumba zinazotumia nishati na mitambo  safi na salama ya kuzalisha umeme.  

WHO pia inapendekeza kuboresha usimamizi wa taka za viwandani na manispaa, lakini pia kupunguza uzalishaji wa taka za kilimo, uchomaji moto misitu na baadhi ya shughuli za kilimo mseto kama vile uzalishaji wa mkaa.