Nimeacha kazi ili nimhudumie mwanangu: Simulizi ya mama mwenye mtoto aliye na usonji

Kutana na Elly Kitali, mama wa watoto wawili, ambaye ameamua kuweka kando taaluma yaka ili kumleta mtoto wake wa kiume aitwaye Chadron. Chadron ana changamoto zaidi ya moja ya kiafya; usonji na ugonjwa unaoathiri uwezo wa mtu kujifunza au Down Syndrome.
“Kwa mara ya kwanza nilitambua Chadron ana usonji, alipokuwa na umri wa miaka mitatu na tulitegemea Chadron atakuwa na uwezo wa kuzungumza maneno machache hata mama au baba, yaani awe na mawasiliano, lakini haikuwa hivyo,” anasema Bi. Kitali.
Shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni, WHO linasema Watoto wa kiume huathirika zaidi kuliko watoto wa kike na kwamba 1 kati ya watoto 44 anaishi na hali ya usonji, hivyo basi mtoto 1 wa kiume kati ya watoto 127 wa kiume ana usonji.
Wazazi hugundua mtoto ana usonji baada ya kuonyesha tabia zisizo za kawaida ndani ya miezi 18. Tabia hizo ni pamoja na kushindwa kutamka neno lolote anapotimiza umri wa miaka 16, kupiga piga mikono, kung’ang’ania vitu, kutikisa kichwa mara kwa mara, kutotamka maneno ya kitoto anapotimiza umri wa mwaka mmoja, kutumia nguvu sana, kuparua wengine, kujiumiza mwenyewe kwa kujing’ata, kujikwaruza na kurusha vitu.
Tabia ya Chadron kwa ujumla ni ngumu kwa sisi wazazi kuelewa kwa mfano ana tabia ya kutumia nguvu sana, kupiga kelele, kuparua hasa akiwa anaumwa au akiwa amekasirika, lakini pia ana tabia ya kujitenga, iwapo utamuweka eneo lenye watoto wengi, pia ana tabia ya kurusha vitu.
Usonji umeathiri watoto duniani kote, wazazi hupitia mambo mengi tangu mtoto anapotimiza miezi 18 hadi umri wa miaka 12.
Wazazi huathirika kisaikolojia na kijamii ambapo Mtaalam wa Mazoezi Tiba kwa Vitendo katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili nchini Tanzania, Godfrey Kimathy amesema maara nyingi tunakaa na wazazi na kuwaeleza hali ya usonji kwa mtoto kwa sababu tunatamani mzazi ajue hali ya usonji kwa mwanae hasa ni nini ili awe katika nafasi nzuri ya kumsaidia.
Hamasa nyingi kutolewa kwa wazazi wenye watoto wa hali ya Usonji, ikiwemo kujiunga katika makundi ya kusaidiana ambayo husaidia wazazi kwa wazazi kupeana uzoefu ambao wamepitia, mzazi na mtaalam kukaa pamoja kwaajili yakumpa mzazi msaada wa kisaikolojia, familia huhamasishwa sana kutoa ushirikiano kwa kumjumuisha, kumjengea ujuzi na ushiriki mtoto mwenye hali ya usonji katika familia.
Bi. Kitali anasema anapata ushirikiano kutoka kwa mume wake, ndugu na marafiki ana anatoa ushauri akisema, “wazazi wa kiume wasikimbie wake zao na watoto wenye usonji. Katika harakati zangu za kusaidia wazazi wenye watoto wenye usonji kama mimi nimekutana na wanawake wengi ambao wamekimbiwa na waume zao. Hii tabia si nzuri na inawasababishia maisha ya shida hasa mtoto mwenye usonji.