Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Zaidi ya raia 10,000 wa DRC wakimbilia Uganda

Wakimbizi wwa DRC wamewasili wilayani Kisoro nchini Uganda
© UNHCR/Calvin Odur
Wakimbizi wwa DRC wamewasili wilayani Kisoro nchini Uganda

Zaidi ya raia 10,000 wa DRC wakimbilia Uganda

Msaada wa Kibinadamu

Zaidi ya raia 10,000 kutoka Jamhuri ya kidemokrasia Kongo DRC wamekimbilia nchini Uganda kufuatia machafuko yanayoendelea kwenye jimbo la Kivu Kaskazini nchini humo.

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR kwakushirikiana na serikali ya Uganda na wadau wengine wa misaada ya kibinadamu wanawapokea wakimbizi hao walioanza kuingia kwa kasi nchini Uganda tarehe 28 Machi 2022 kupitia mpaka wa Bunagana. 

Assumpta Massoi/UNNewsKiswahili

Mwakilishi wa UNHCR nchini Uganda Joel Boutroue akizungumza katika mkutano wa waandishi wa habari jijini Geneva Uswisi amesema “watu hao waliowasili wameeleza milio ya risasi ilikuwa ikisikika wakiwa mpakani kuashiria mapigano yalikuwa yakiendelea. Watu sita walifika wakiwa na majeraha ya risasi na kupelekwa kwenye matibabu.”

Boutriue ameeleza wakimbizi hao wamesafiri katika mazingira magumu zaidi kutokana na mvua kubwa zinazonyesha na watu waliofika wamebeba vitu vichache tu ambavyo wangeweza kubeba. “Maelfu ya watoto, wanawake na wanaume wamewasili kutoka eneo la Rutchuru nchini DRC, takriban kilomita 8 kutoka kwenye kivuko cha mpaka cha Bunagana katika wilaya ya Kisoro nchini Uganda.”

Shukran kwa serikali ya Uganda 

Mbali na kuwa kwa sasa Uganda imefunga mpaka wa Bunagana kufanya biashara lakini hiyo haikufanya kushindwa kuwaruhusu wanaosaka hifadhi kuingia nchini humo. 

UNHCR na Ofisi ya Waziri Mkuu ya Uganda ambayo ndio yenye jukumu la kusimamia vituo kadhaa vya usafiri kwa wanaotafuta hifadhi kwenye mpaka wa DRC tayari imewahamisha waomba hifadhi wapatao 2,350 katika kituo cha karibu cha Nyakabande.

“Wasaka hifadhi wengine wanatumia njia zisizo rasmi kuvuka mpaka huo lakini pia tumeona watoto wengi wakiingia nchini humu bila ya wazazi au walezi, wazee na walemavu wanaotumia viti vya magurudumu matatu.” Amesema mwakilishi huyo wa UNHCR. 

Wengi wa wakimbizi wapya wanataka kukaa karibu na mpaka ili waweze kupata habari zinazoendelea katika vijiji vyao kwa matumaini kwamba vurugu hizo zitakoma na waweze kurejea nyumbani hivyo wanajihifadhi karibu na soko na pamoja maeneo mengine ya wanajamii. 

Wengine wakimbilia maeneo mengine 

Mbali na kukimbilia nchini Uganda, UNHCR imeeleza kuna wakimbizi wa ndani wapatao 36,000 ambao wamekimbilia maeneo mengine ndani ya DRC. Wengi wao wamepatiwa hifadhi na familia wenyeji wa maeneo hayo, au sokoni na shuleni. 

Hata hivyo hali ya usalama inafanya kuwa vigumu kuwafikia walioathirika, lakini kuna jopo maalum linalofanya kazi ya kujaribu kuwafikia likiongozwa kwa pamoja na UNHCR na Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani WFP ili kuweza kuwapatia msaada wa kibinadamu.

Ufadhili bado ni mdogo Uganda

Mpaka sasa UNHCR imepokea asilimia 9 pekee ya mahitaji ya jumla ya ufadhili ya dola milioni 343.3 kwa ajili ya shughuli zake nchini Uganda, nchi ambayo inahifadhi wakimbizi wengi zaidi kuliko nyingine yoyote barani Afrika.

Zaidi ya hayo, mahitaji ya kibinadamu ya wakimbizi wa ndani zaidi ya milioni 5.6 nchini DRC bado hayajafikiwa kutokana na ukosefu wa fedha.