Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu
Katibu Mkuu António Guterres akiongoza mkutano wa hafla ya kutoa ahadi za kusaidia  msaada wa kibinadamu nchini Afghanistan.

Tusipoipa kisogo tunaweza kuinusuru Afghanistan na mahitaji yake ya kibinadamu:UN

UN Photo/Eskinder Debebe
Katibu Mkuu António Guterres akiongoza mkutano wa hafla ya kutoa ahadi za kusaidia msaada wa kibinadamu nchini Afghanistan.

Tusipoipa kisogo tunaweza kuinusuru Afghanistan na mahitaji yake ya kibinadamu:UN

Msaada wa Kibinadamu

Wakati dunia inaelekeza nguvu zake katika vita vinavyoendelea nchini Ukraine, Umoja wa Mataifa hii leo umeikumbusha jumuiya ya kimataifa kuikumbuka Afghanistan wakati ukizindua mkutano wa ahadi za msaada wa kuokoa maisha ya mamilioni ya watu wa taifa hilo lisilo na bandari. 

Licha ya mahitaji ya kibinadamu yanayoendelea kuchochewa na mzozo wa miaka mingi na ukame wa mara kwa mara, hali ya sasa nchini Afghanistan ni mbaya, ambapo zaidi ya watu milioni 24.4 wanahitaji msaada wa kibinadamu ili kuendelea kuishi, kulingana na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu masuala ya kibinadamu OCHA

Viwango vya uhakika wa chakula vimeshuka kwa kasi ya kutisha, na kuacha nusu ya watu wakikabiliwa na njaa kali, ikiwa ni pamoja na milioni 9 katika hali ya dharura ya uhaba wa chakula ikiwa ni idadi kubwa zaidi duniani. 

Isitoshe, utapiamlo unaongezeka, na uwezo wa watu kupata riziki umesambaratishwa. 

Mtoto wa miezi 18 nchini Afghanistan akiwa anaugua utapiamlo mkali na maradhi mengine
© UNICEF/Hasinullah Qayoumi
Mtoto wa miezi 18 nchini Afghanistan akiwa anaugua utapiamlo mkali na maradhi mengine

Ombi la msaada  

Ili kusaidia kukabiliana na hali hiyo, Katibu Mkuu António Guterres leo amezindua mtandaoni tukio la ngazi ya juu la ombi la ahadi za kuunga mkono hatua za msaada wa kibinadamu nchini Afghanistan lililoandaliwa kwa pamoja na serikali za Uingereza, Ujerumani na Qatar. 

Mwaka jana, wakati nchi ilipokabiliwa na msukosuko mkubwa na kutengwa kimataifa, wafadhili walionyesha ukarimu wa ajabu kwa Waafghanistan.Walitoa ufadhili wa dola bilioni 1.8 kwa mashirika ya misaada na uliweza kusaidia watu milioni 20 kwa chakula cha kuokoa maisha, maji safi, huduma za afya, malazi na elimu. 
Wafadhili wa kimataifa wanaombwa kuendelea kutoa fedha hizo na kuziongeza tena mwaka huu. 

Operesheni ya misaada inayoratibiwa na Umoja wa Mataifa ni kubwa zaidi lakini sio pekee nchini Afghanistan na inaomba dola bilioni 4.4, ikiwa ni mara tatu ya kiasi kilichoombwa mwaka 2021. 

"Tuna uwezo wa kukomesha kuendelea kudorora kwa hali ya kibinadamu nchini Afghanistan na ni wajibu wetu wa kimaadili kutumia uwezo huu kwa ukarimu wa leo kuahidi ufadhili, unaobadilika na usio na masharti” amesema mkuu wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya kibinadamu Martin Griffiths. 

Watoto wakifanya kazi ya kubeba mizigo ya wasafiri katika mpaka wa Pakistan na Afghanistan huko Kandahar
© UNOCHA / Sayed Habib BIDEL
Watoto wakifanya kazi ya kubeba mizigo ya wasafiri katika mpaka wa Pakistan na Afghanistan huko Kandahar

Kuleta mabadiliko 

OCHA inasema kwa vile uchangishaji wa fedha hadi sasa umepata asilimia 13 pekee ya mahitaji ya mpango wa hatua za kibinadamu wa mwaka 2022, ahadi za usaidizi ambazo zitaendelea kwa muda uliosalia wa mwaka huu  zinahitajika kwa haraka ili kuongeza utoaji wa misaada. 

Katika wiki nane za kwanza za mwaka 2022, washirika wa kibinadamu walifikia watu milioni 12.7 kwa msaada wa kuokoa maisha, wakitoa kipaumbele kwa wanawake, wasichana na makundi ya wachache. 

Usambazaji wa misaada umejumuisha chakula chenye lishe kwa mamia ya maelfu ya watoto wenye utapiamlo na wanawake wajawazito na wanaonyonyesha; chakula cha afya kwa watoto wa shule, mbegu na pembejeo kwa wakulima, na matibabu ya majeraha na afya ya uzazi. 

Washiriki wa mkutano huo wanahimizwa kuahidi kwa ukarimu kuonyesha ishara kubwa ya mshikamano kwamba ulimwengu unasimama na watu wa Afghanistan. 

Mtoto wa kiume akiwa darasani huo Herat,Afghanistan
© UNOCHA/Sayed Habib Bidel
Mtoto wa kiume akiwa darasani huo Herat,Afghanistan

Kujadili makosa yanayotendeka 

Kabla ya mkutano huo, mkuu wa shirika la mpango wa maendeleo la Umoja wa Mataifa UNDP, Achim Steiner, alifanya safari ya siku mbili nchini humo, ambapo alisisitiza umuhimu wa haki za wasichana na wanawake nchini Afghanistan. 

Maamuzi ya hivi majuzi ya kuwazuia wasichana kwenda shule ya sekondari kuanzia darasa la 6 na kuendelea yanatia wasiwasi mkubwa, alisema, akisisitiza kwamba UNDP imejitolea kufanya kazi na mashirika ya Umoja wa Mataifa kutetea na kukuza upatikanaji wao wa elimu na kazi. 

"Ushirikiano wa UNDP mara nyingi huwa wa pande nyingi, na wakati mwingine tunakabiliwa na changamoto kama vile kukosa elimu ya wasichana nchini Afghanistan, kunaweza kuwa makosa makubwa ya kujadiliwa”. 
Ameongeza kuwa "Wote wavulana na wasichana lazima waruhusiwe kuingia madarasani kwa sababu mustakabali wa Afghanistan lazima uwe wa Waafghanistan wote, sio tu wachache waliochaguliwa".

Kuongezeka kwa umaskini 

Mkuu huyo wa UNDP pia ameelezea hitaji la dharura la kuchukuliwa hatua ili kuzuia umaskini unaoongezeka kwa kasi na kuyumba kwa uchumi. 

"Tuliripoti mwishoni mwa mwaka jana kwamba inakadiriwa kuwa asilimia 97 ya Waafghan wanaweza kuwa wanaishi katika umaskini ifikapo katikati ya 2022, na cha kusikitisha ni kwamba, idadi hiyo inafikiwa haraka kuliko ilivyotarajiwa," amesema. 

Ameongeza kuwa "Na kutokana na kupanda kwa bei za bidhaa duniani kote, tunajua kwamba watu hapa hawawezi kumudu mahitaji yao ya msingi ya kibinadamu kama vile chakula, huduma za afya na elimu". 

Mwanamke anamleta mpwa wake aliye na utapiamlo mkali kupatiwa atibabu katika kliniki huko Kandahar, Afghanistan.
© UNICEF/Alessio Romenzi
Mwanamke anamleta mpwa wake aliye na utapiamlo mkali kupatiwa atibabu katika kliniki huko Kandahar, Afghanistan.

Msaada kwa wanawake wamiliki wa biashara 

Huko Mazar-e-Sharif, Bw. Steiner alikutana na wanawake wamiliki wa biashara na wanachama wa chama cha wafanyabiashara ambao walizungumza kuhusu jitihada zao za kuweka biashara sawa. 

"Wanawake wafanyabiashara wadogo niliozungumza nao ni wastahimilivu katika azma yao ya kuendelea kupata mapato na kuhudumia familia na jamii zao dhidi ya matatizo yote," Amesema Bwana. Steiner, huku akiisukuma jumuiya ya kimataifa kusaidia kuzuia matatizo zaidi ya kiuchumi kwao. 

Ameendelea kusema kuwa "Mwaka huu pekee, tunalenga kusaidia zaidi ya wafanyabiashara 50,000 wadogo na wa kati, wengi wao wakiongozwa na wanawake." 

Kandahar, Afghanistan
Picha: UNAMA
Kandahar, Afghanistan


Mzigo mkubwa wa madeni 

UNDP imeonya kuwa kufuatia unyakuzi wa madaraka uliofanywa na Taliban mwezi Agosti, mwaka jana Afghanistan inakabiliwa na anguko la kiuchumi ambalo haliwezi kubadilika, mfumo wa benki uliogandishwa na ukwasi ambao unaweza kuwaacha takriban asilimia 80 ya watu nchini humo kwenye mzigo mkubwa wa madeni. 

"Lazima tuurudishe uchumi wa taifa hilo kwenye msitari na kupanda kutoka chini kwenda juu, na hiyo inamaanisha msaada kwa watu binafsi, familia zao na biashara zao," alisema mkuu wa UNDP, akitetea ukarimu katika mkutano huo wa ahadi ya msaada. 

"Wakati tahadhari ya dunia inaelekezwa nchini Ukraine na athari mbaya za vita hivyo, lazima pia tusimame kwa mshikamano na watu wa Afghanistan".