Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO yazindua mpango wa kuzuia janga jipya la kimataifa la kiafya

 Aina za kawaida za magonjwa yanayoenezwa na mbu ni pamoja na Kidingapopo, Homa ya Manjano, Chikungunya na Zika.
Unsplash/Shardar Tarikul Islam
Aina za kawaida za magonjwa yanayoenezwa na mbu ni pamoja na Kidingapopo, Homa ya Manjano, Chikungunya na Zika.

WHO yazindua mpango wa kuzuia janga jipya la kimataifa la kiafya

Afya

Virusi vya Arbo inaweza isiwe ni kitu ambacho watu wengi wanakifahamu, lakini ni tishio kubwa kwa karibu watu bilioni nne, ndiyo maana leo shirika la afya la Umoja wa Mataifa WHO , limezindua mpango wa kuzuia virusi hivyo kusababisha janga jipya la kimataifa .

Virusi vya arbo vinavyojulikana zaidi ni vya baadhi ya magonjwa hatari zaidi duniani yanayoenezwa na mbu, kama vile homa ya kidingapopo, homa ya manjano, Chikungunya na Zika. 

Magonjwa haya yanawakilisha tishio la kila wakati na kubwa la kiafya katika sehemu za tropiki duniani ingawa kuna idadi inayoongezeka ya milipuko ya virusi vya magonjwa hayo ulimwenguni, kwa mujibu wa WHO

Mbu aina ya aedes aegypti ambaye anaeneza ugonjwa wa zika, bila kusahau dengue na chikungunya
IAEA
Mbu aina ya aedes aegypti ambaye anaeneza ugonjwa wa zika, bila kusahau dengue na chikungunya

Kushikamana kudhibiti virusi hivyo 

Akikaribisha hatua hiyo, Dkt. Mike Ryan, mkuu wa mipango ya dharura wa WHO, ameeleza kuwa mpango huo utaruhusu mamlaka za afya kukabiliana na matishio makubwa lakini yanayohusiana yanayoletwa na homa ya kidingapopo, homa ya manjano, Chikungunya na Zika, katika maeneo tofauti ya nchi duniani. 

"Kwa kila moja ya magonjwa haya kumekuwa na faida katika nyanja tofauti za hatua za ufuatiliaji, utafiti na maendeleo. Lakini uendelevu wa hatua hizo mara nyingi ni mdogo kulingana na upeo na muda na ukubwa wa mahonjwa na miradi mahususi ya magonjwa hayo”. 

Ameongeza kuwa "Kuna hitaji la dharura la kutathmini upya zana zilizopo na jinsi zinavyoweza kutumika katika magonjwa hayo yote ili kuhakikisha mwitikio mzuri, ushahidi wa hatua zilizochukuliwa, wafanyikazi walio na vifaa na mafunzo yanayohitajika na ushiriki wa jamii." 

WHO inasema lengo la mpango wa kimataifa wa Arbovirus litakuwa kuzingatia rasilimali katika ufuatiliaji wa hatari za magonjwa hayo, kuzuia janga la kimataifa, kujiandaa, kugundua na kukabiliana, na milipuko hiyo. 
Limesisitiza kwamba hatua za kimataifa ni muhimu, kwa kuzingatia masafa na ukubwa wa milipuko ya virusi vya arbo, haswa vile ambavyo hupitishwa na mbu aina ya Aedes. 

WHO imeonya kuwa ufikiaji wa mbu hao unakua, pia, ukichochewa na mabadiliko ya tabianchi, ongezeko la watu duniani na kuongezeka na kukua kwa miji. 

Huko Recige nchini Brazil, mama akiwa na mwanae mwenye umri wa miezi 4 ambaye alizaliwa na kichwa kidogo,ugonjwa usababishwao na kirusi cha Zika kinachoenezwa na mbua aina ya aedes aegypti.
UNICEF/Ueslei Marcelino
Huko Recige nchini Brazil, mama akiwa na mwanae mwenye umri wa miezi 4 ambaye alizaliwa na kichwa kidogo,ugonjwa usababishwao na kirusi cha Zika kinachoenezwa na mbua aina ya aedes aegypti.

Madhila ya magonjwa haya 

Kila mwaka, homa ya kidingapopo huambukiza watu milioni 390 katika nchi 130 ambako ni janga. 
Na homa hii inaweza kusababisha uvujaji wa damu katika ubongo na kifo. 

Homa ya manjano inaleta hatari kubwa ya milipuko katika nchi 40 na husababisha homa ya manjano na homa kali ya kuvuja damu na hatan kifo. 

Chikungunya haijulikani sana, lakini iko katika nchi 115 na husababisha ugonjwa mbaya wa mifupa au arthritis. 

Virusi vya Zika vilipata umaarufu duniani kote mwaka wa 2016 wakati vilipogundulika kusababisha kasoro za kuzaliwa kwa watoto kama vile kuzaliwa na kichwa kikubwa au microencephaly na imegunduliwa katika nchi 89. 

WHO inaamini kwamba ingawa kuna chanjo ya homa ya manjano, kwa wengine, kinga bora ni kuzuia kuumwa na mbu kwanza. 

Mtaalam wa maabara akipima sampuli za damu  kuangalia uwepo wa virusi vya Zika
WHO/PAHO
Mtaalam wa maabara akipima sampuli za damu kuangalia uwepo wa virusi vya Zika

Pengo la usawa wa kiafya 

Dkt. Ryan amebainisha kwamba kabla ya kuzinduliwa rasmi leo kwa mpango huo kwa miaka miwili kumekuwa na dalili za watu kufurahishwa na mpango huo licha ya shinikizo la janga linaloendelea hivi sasa la COVID-19, kwani kuna wasiwasi unaoongezeka juu ya magonjwa ya arboviral kuenea na kusababisha milipuko mikubwa ya kikanda, na kuathiri watu wasio na vifaa vya kutosha kukabiliana na milipuko hiyo. 

Amesema cha muhimu katika mpango huo wa WHO ni kujenga uwezo wa kukabiliana na vimelea vya magonjwa ya arboviral katika vituo vya afya vya mstari wa mbele, na pia katika ngazi ya kikanda na kimataifa. 
"WHO iko tayari kuongoza na kuunga mkono mipango hii ya kimkakati ya kujiandaa na janga hili na kujenga muungano wa kimataifa wa nchi na washirika ili kukabiliana na hatari inayoletwa na vimelea hivi," amesisitiza Dkt. Ryan