Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Msaada wa haraka unahitaji kwa wananchi waliozungukwa na maji ya mafuriko Sudan Kusini

Mwanamke mzee akikusanya maua ya lily kwenye maji ya mafuriko huko Fangak, Jimbo la Jonglei, Sudan Kusini.
© WFP/Marwa Awad
Mwanamke mzee akikusanya maua ya lily kwenye maji ya mafuriko huko Fangak, Jimbo la Jonglei, Sudan Kusini.

Msaada wa haraka unahitaji kwa wananchi waliozungukwa na maji ya mafuriko Sudan Kusini

Tabianchi na mazingira

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR limeonya hali Sudan Kusini huenda ikawa mbaya zaidi ifikapo mwezi Mei mwaka huu iwapo msaada wa haraka hautapatikana kusaidia wananchi wanaoishi katika maeneo yakiyozingirwa na maji ya mafuriko ya muda mrefu.

Kuishi katika maeneo yaliyo zingirwa na maji ya mafuriko kwa kipindi cha miaka miwili mpaka mitatu imekuwa ndio maisha ya kawaida kwa takriban wananchi 835,000 wa Sudan Kusini ambao tangu mwaka 2020 wamekuwa wakishuhudia mafuriko yanayozidi kuleta madhara bila ya kuwa na matumaini ya maji kukauka licha ya mbinu mbalimbali wanazotumia. 

Kutokana na kuhamahama kwao wamepoteza si mazao tuu bali zaidi ya mifugo laki 8, Angelina Peter ni mmoja wa waathirika wa mafuriko ambaye kwa sasa yupo katika kambi ya Fangak anasema “Kutokana na mafuriko maji yalizamisha vijiji vyetu, tulifika hapa bila kitu, mali zetu zote zilisombwa na maji, hii ni mara ya 2 inafurika ndani ya miaka 2, mwaka 2020 hali haikuwa mbaya sana kwa sababu tulijenga mitaro.”

Angelina anayejishughulisha na kuuza kuni ili kuwapatia mlo watoto wake anasema “nikishindwa kuuza,wanangu hawali. Sabuni hakuna, hakuna chakula, hakuna chochote.” Kwa huzuni anaeleza kuwa “Hii nyumba nilijenga mimi mwenyewe, ninaishi na watoto wangu hapa, nilienda kukata vijiti msituni na kuleta hapa, kisha nikavifunga kwa kamba, lakini sasa mvua zinakuja, tutakuwa kwenye changamoto kubwa zaidi hapa. . Kwa sababu mvua itaharibu na kuyachukua malazi yetu."

Mitumbwi imekuwa njia pekee ya usafiri kwa wakazi wa Old Fangak, Sudan Kusini.
© UNHCR/Samuel Otieno
Mitumbwi imekuwa njia pekee ya usafiri kwa wakazi wa Old Fangak, Sudan Kusini.

Mshauri Maalum wa UNHCR kuhusu masuala ya Hali ya hewa Andrew Harper ameshuhudia jitihada za wananchi walioko kambi ya Fangak wanaojenga maboma ya kuzuia maji kabla ya mvua kuanza mwezi Mei na anaeleza kusikitishwa na namna jamii zinazojitahidi kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na hali mbaya ya hewa ingawa wao sio waliosababisha. 

“Tunatakiwa kuhimiza wadau wa maendeleo kutoa msaada moja kwa moja kwa jamii hizi, wanahitaji mashine nzito, pampu, kwa sasa wanachimba kwakutumia majembe ili kujenga maboma ya kuzuia maji ya mafuriko yasienee. Wanafanya hivi kupinga athari za mabadiliko ya tabiachi ambazo hawana uhusiano wowote nazo. Mafuriko haya yamekuwa hapa kwa miaka 2 hadi 3 na hayapungui. Nini kitatokea mvua zinazofuata zinakuja katika miezi 2 au 3 ijayo?”

Ulimwenguni kote, mafuriko na ukame vinazidi kushamiri na kuleta madhara makubwa kwa jamii. Nchi zinazoendelea, kama Sudan Kusini zinachangia kwa uchache zaidi katika utoaji wa hewa ukaa, lakini zimeathirika kwa kiasi kikubwa na athari za mabadiliko ya tabianchi.