COVID-19 yahatarisha kufanya elimu kuongeza mgawanyiko badala ya kujenga usawa- UNICEF

30 Machi 2022

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF linasema janga la ugonjwa Corona au COVID-19 likiingia mwaka wa tatu, nchi 23 bado hazijafungua shule zao kikamilifu na hivyo kuwaweka watoto milioni 405 katika hatari ya kuacha shule na zaidi ya yote kuongeza pengo la ufahamu duniani badala ya kuchochea usawa.

 Katika ripoti yake iliyotolewa leo jijini New York, Marekani, UNICEF inasema watoto milioni 147 duniani kote walikosa takribani nusu ya muda wao wa kuweko shuleni katika kipindi cha miaka miwili ya COVID-19, ikimaanisha wamekosa jumla ya saa trilioni 2 za muda wa masomo darasani.

Ikipatiwa jina Je watoto kweli wanajifunza? Ripoti inachambua takwimu za kitaifa juu ya madhara ya COVID-19 katika watoto kujifunza hususan kufungwa kwa shule huku ikilinganisha na kipindi cha kabla ya COVID-19.

Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF, Catherine Russel ansema pindi watoto wanashindwa kuchangamana na walimu pamoja na wenzao shuleni, uwezo wao wa kujifunza  unapata mkwamo na kile walichopoteza kwenye kujifunza kinakuwa kimepotea kabisa.

Watoto wakijifunza kupitia kompyuta ndogo au Tablet kwenye shule moja huko Yaoundé nchini Cameroon
© UNICEF/Frank Dejongh
Watoto wakijifunza kupitia kompyuta ndogo au Tablet kwenye shule moja huko Yaoundé nchini Cameroon

“Ongezeko hili la ukosefu wa usawa katika kupata fursa ya elimu, linamaanisha kuwa elimu iko katika tisho la kuwa jambo kubwa linaloongeza mgawanyiko badala ya kuwa jambo kubwa la kuongeza usawa,” amesema Bi. Russel huku akisema kuwa pindi dunia inashindwa kuelimisha watoto, basi kila mtu atapata tabu.

Takwimu zaongeza hofu Afrika Kusini, Malawi, Uganda

Kando ya takwimu kuhusu kupotea kwa fursa ya kujifunza, ripoti pia inaonesha Ushahidi mpya ya kwamba watoto wengi hawakuweza kurejea shuleni pindi shule zilifunguliwa. Mathalani nchini Liberia, asilimia 43 ya wanafunzi katika shule za umma hawakurejea shuleni mwezi Desemba mwaka 2020, ilhali nchini Afrika Kusini idadi ya watoto wasiokuweko shuleni iliongezeka mara tatu kutoka 250,000 Machi 2020 hadi 750,000 mwezi Julai mwaka 2021.

Nchini Uganda, mwanafunzi 1 kati ya 10 hawakuweza kurejea shuleni mwezi Januari mwaka huu wa 2022 shule zilipofunguliwa baada ya kufungwa kwa miaka miwili. Huko Malawi, kiwango cha utoro shuleni miongoni mwa wanafunzi wa kike kwenye shule za sekondari iliongezeka kwa asilimia 48 kutoka asilimia 6.4 hadi asilimia 9.5 kati yam waka 2020 hadi 2021.

Huko Kenya, tafiti miongoni mwa barubaru 4,000 wenye  umri wa kati yamiaka 10 hadi 19 ulibaini kuwa asilimia 16 ya wasichana na asilimia 8 ya wavulana hawakurejea shuleni pindi zilipofunguliwa.

Madhara yaliyopatikana

Watoto wasiokwenda shuleni wako hatarini zaidi na ndio walioenguliwa zaidi kwenye jamii, imesema UNICEF katika taarifa hiyo.

“Wanakuwa na uwezo mdogo zaidi wa kuweza kusoma, kuandika na kufanya hesabu za kawaida na wanaenguliwa katika fursa ya kunufaika na mipango kama vile ya usalama, na ulinzi pamoja na mlo shuleni hali inayowaweka katika mazingira hatari ya kutumikishwa, kunyanyaswa na hatimaye kuwa maskini,’ imesema UNICEF.

Wazazi wakiweka chakula kwenye sahani tayri kuwapatia wanafunzi shuleni nchini Niger
© WFP/Evelyn Fey
Wazazi wakiweka chakula kwenye sahani tayri kuwapatia wanafunzi shuleni nchini Niger

Mtoto wa darasa la 8 hajui kusoma na kufanya hesabu

Ripoti hiyo ya kurasa 60, inaangazia kuwa ilhali watoto wasio shuleni waliathirika zaidi, takwimu za kabla ya COVID-19 kutoka nchi 32 na maeneo zinaonesha kiwango cha chini ya kujifunza hata kwa walio shuleni, hali ambayo inaweza kuwa ilikuwa mbaya zaidi wakati wa Corona.

Takwimu zinaonesha kuweko kwa kasi ndogo ya kujifunza ambayo inaweza kuhitaji miaka 7 kwa wanafunzi wengi kujifunza misingi ya kusoma, misingi ambayo wangaliweza kujifunza katika kipindi cha miaka miwili,. Halikadhalika kwa kasi ya sasa misinig ya stadi za kuhesabu zilizopotea itahitaji miaka 11.

UNICEF inasema hakuna hakikisho kuwa katika kipindi cha COVID-19 wanafunzi walijifunza misingi ya masomo kwa kuwa katika nchi 32 zilizochunguzwa, robo ya wanafunzi wa darasa la 8 wenye umri wa miaka 14 hawakuwa na msingi wa kusoma na zaidi ya nusu hawakuwa na stadi za hesabu zinazotakiwa kwa mtoto wa darasa la 2 ambaye kwa wastani anakuwa na umri wa miaka 7.

Mukasa Herbert mwanafunzi katika Shule ya Nakivubo Settlement Nursery na Primary School nchini Uganda ananawa mikono siku ya kwanza ya kufungua tena shule, Januari 10, 2022.
© UNICEF/Maria Wamala
Mukasa Herbert mwanafunzi katika Shule ya Nakivubo Settlement Nursery na Primary School nchini Uganda ananawa mikono siku ya kwanza ya kufungua tena shule, Januari 10, 2022.

Hali ya kujifunza hata kabla ya COVID-19 ilikuwa ni tatizo, ni kwa mantiki hiyo , Bi. Russel anasema “hatuwezi kukubali kurejea katika hali ya kawaida kabla ya COVID-19. Tunahitaji ‘kawaida mpya’ watoto tuwarejeshe darasani, tutathmini kiwango chao cha kujifunza na tuwapatie msaada wote unaohitajika ili waweze kupata kile walichopoteza na tuhakikishe walimu wana mafunzo na rasilimali wanazohitaji.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter