Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Katika umri wangu wa miaka 70 sijashuhudia ukame wa kiwango hiki- Mwananchi Somalia

Ahmad Hassan Yarow mwenye umri wa miaka 70 katika kambi ya wakimbizi wa ndani Luuq nchini Somalia
UN Photo/Fardosa Hussein
Ahmad Hassan Yarow mwenye umri wa miaka 70 katika kambi ya wakimbizi wa ndani Luuq nchini Somalia

Katika umri wangu wa miaka 70 sijashuhudia ukame wa kiwango hiki- Mwananchi Somalia

Msaada wa Kibinadamu

Akiwa amesimama mbele ya kibanda chake kwenye makazi ya wakimbizi ya Kulmiye wilayani Luuq nchini Somalia, Ahmad Hassan Yarrow anatazama kile kilichosalia katika mto Juba, ambao ulikuwa ndio tegemeo la uhai wa  eneo lao. Mto umekauka. “Katika umri wangu wa miaka 70 sijawahi kushuhudia ukame kama huu, katika vipindi vyote vya ukame vilivyopita,” anasema Bwana Yarrow katika makala iliyochapishwa kwenye ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa usaidizi nchini Somalia, UNSOM.

Bwana Yarow ni miongoni mwa mamia ya maelfu ya wakimbizi wa ndani Somalia ambao wamekimbia makwao kutokana na ukame wa sasa, wakisaka maji, chakula na malazi.

Taswira kutoka angani kupitia video ya ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kusaidia Somalia, UNSOM inaonesha mto Juba, tegemeo lao umekauka! Mimea halikadhalika! Mizoga ya Wanyama kama vile mbuzi na punda imesambaa. Mifugo ambayo bado iko hai inahaha kusakanya chochote kilichoko angalau ipate shibe!

Kadri hali ya ukame inavyozidi kuwa mbaya nchini Somalia, Umoja wa Mataifa unasema tishio la baa la njaa linanyemelea taifa hilo la pembe ya Afrika wakati huu ambapo tayari wasomali milioni 4.5 wameathiriwa moja kwa moja na ukame ilhali 700,000 wamefurushwa makwao kutokana na ukame. 

Wilaya ya Luuq iko kwenye eneo la Gedo jimboni Jubaland ambako mto Juba unapita. Kwa zaidi ya miezi mitatu sasa maji yamepungua na kuacha vijito vidogo vidogo. 

“Sisi ni wakulima na pia tuna mifugo. Lakini mifugo yote imekufa kwa ukame. Hatuna chochote kilichosalia na tumefika hapa kupata maji, chakula na msaada.” -  Salado Mursaal, Mkimbizi wa ndani

Maji yanavyozidi kupungua kutokana na mabadiliko ya tabianchi, ndivyo yanavyozidi kuyoyoma matumaini ya jamii ya eneo hilo inayoundwa na wakulima na wafugaji. Jamii hii inategemea mto huu wa Juba kwa ajili ya kujipatia kipato. 

Salado Madeer Mursaal akiwa amebeba mwanae kwenye kambi ya wakimbizi ya Boyle anasema, “sisi ni wakulima na pia tuna mifugo. Lakini mifugo yote imekufa kwa ukame. Hatuna chochote kilichosalia na tumefika hapa kupata maji, chakula na msaada.”

Umoja wa Mataifa unasema vipindi vitatu vya mvua vimepita bila mvua, na kwamba msimu wa nne unaoanza mwezi ujao hadi Juni unatarajiwa kuwa na mvua za wastani na iwapo hilo litatokea kuna hatari ya baa la njaa.

Kundi la wanawake likiteka maji kutoka kwenye lori linalosambaza maji kwenye kijiji cha Kureyson huko Galkayo Somalia tarehe 23 Machi 2022
UN /Fardosa Hussein
Kundi la wanawake likiteka maji kutoka kwenye lori linalosambaza maji kwenye kijiji cha Kureyson huko Galkayo Somalia tarehe 23 Machi 2022

Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji, IOM, limekuwa likisambaza maji  kwenye kambi za wakimbizi wa ndani kwa kutumia malori. Kambi hizo ni pamoja na ile ya Boyle.
Halikadhalika IOM inajenga tenki za kuwekea maji pamoja na matundu ya choo ili kusaidia kuimarisha huduma za kujisafi. 

Utapiamlo uliokithiri nao unatesa watoto

Hospitali ya wilaya ya Luuq inapata ufadhili kidogo kutoka shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF. Katika hospitali hii, UNICEF inashirikiana na shirika la misaada la Ireland, Trocaire, kupatia watoto matibabu dhidi ya utapiamlo uliokithiri au unyafuzi pamoja na kuwapatia lishe bora na tiba nyinginezo.

Wahudumu katika wodi ya watoto kwenye hospitali hii wanasema wameona hali tete kuwahi kushuhudia.

Watoto wanapatiwa maziwa na kisha wanahamishiwa vituo vya lishe ambako wanapatiwa biskuti zenye virutubisho vya hali ya juu na matibabu ya magonjwa mengine.

Wadau mkiwemo wasomali mlioko ughaibuni changieni - UNSOM

Naibu Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia, Adam Abdelmoula anasema “tunavyozungumza sasa, watoto milioni 1.4 wenye umri wa chini ya miaka mitano wana utapiamlo uliokithiri. Inakadiriwa kuwa 330,000 kati yao wako hatarini kufa kwa unyafuzi. Nato awito kwa wale wote wanaoweza kuchangia, wakiwemo wasomali walioko ugaibuni, wafanyabiashara na kila mtu achukua hatua sasa.”

Umoja wa Mataifa unasaka dola bilioni 1.5 kwa ajili ya usaidizi wa kibinadamu Somalia kwa mwaka 2022 kukidhi mahitaij ya watu milioni 5.5 walio hatarini wakiwemo wakimbizi wa ndani,, makundi yaliyo hatarini na watu wenye ulemavu.
Hata hivyo hadi sasa ombi hilo limefadhiliwa kwa asilimia 4 pekee n ani dola milioni 56.1 ndio zimeshakusanywa.