Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wanawake Nigeria wanavyopinga unyanyapaa dhidi ya warejeao baada ya kushindwa kuhamia Ulaya

Kwa mapato kutoka kwa duka lake, Success anaweza kumtunza binti yake na kumlipia ada ya shule
IOM 2022/Ultrashot
Kwa mapato kutoka kwa duka lake, Success anaweza kumtunza binti yake na kumlipia ada ya shule

Wanawake Nigeria wanavyopinga unyanyapaa dhidi ya warejeao baada ya kushindwa kuhamia Ulaya

Wanawake

Simulizi za wasichana raia wa Nigeria wanaorejeshwa makwao baada ya ndoto zao za kutaka kukimbilia Ulaya kutafuta maisha mazuri kukwamia njiani nchini Libya ambapo wengi wanajikuta katika maisha magumu ikiwemo kulazimishwa kutumbukia kwenye biashara ya ukahaba. 

Success msichana mwenye umri wa miaka 24 akiwa nje ya eneo lake la biashara huko katika mji wa Benin katika jimbo la Edo nchini Nigeria, anapanga nguo alizoshona na nyingine alizoletewa na wateja kwa ajili ya kurekebisha na kuweka viraka , mtoto wake aitwaye Choice yupo pembeni yake akicheza na vikaragosi vyake, mtoto huyu wiki hii shule zimefungwa kwa ajili ya mapumziko mafupi. 

Familia ya Success ilimfukuza yeye na mtoto wake 

Success anakumbuka mwaka 2016 akiwa na umri wa miaka 18 aliondoka nyumbani kwao Nigeria akiwa na dhamira ya kwenda kutafuta maisha bora Ulaya kwa ajili yake na familia yake lakini ndoto yake hiyo ikakwamia Libya na anasema ‘Kule si sehemu nzuri kabisa, kuna mateso sana kuna kupigwa, kubakwa na kulazimishwa kushiriki kwenye ukahaba.” 

Kwa msaada wa shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji IOM, Sucess aliweza kurejea nchini Nigeria kupitia programu ya kuwarejesha na kuwuanganisha wahamiaji hao na familia zao kwa hiari, AVRR.  
 
Hata hivyo familia yake haikufurahi kurejea kwake nyumbani kwao huko katika jimbo la Edo kwa kuwa walikuwa na matarajio makubwa kuwa angewasaidia pindi ambapo angefika Ulaya. 
 
“Walikataa kuniruhusu niingie ndani ya nyumba na kuniambia nirudi kule nilikotoka, walisema wametumia fedha nyingi na sikurejea na chochoe na zaidi ya yote niliondoka bila mtoto na sasa nimerejeana mtoto.” 
 
Kufukuzwa huku yeye na mtoto wake kulimchanganya sana Success na kuwaza labda arejee tena Libya au aende kokote maana familia yake haikumtaka lakini hapo ndipo alipokutana tena na IOM ambayo ilimsaidia. 

Joy anapinga unyanyapaa katika jamii yake na kurejesha maisha yake.
IOM 2022/Ultrashot
Joy anapinga unyanyapaa katika jamii yake na kurejesha maisha yake.

Msichana Joy naye aingia kwenye ukahaba 

Simulizi ya Success ni kama ya binti mwingine aitwaye Joy ambaye mwanzoni mwa mwaka 2018 akijikuta akiishia kufanya biashara ya ukahaba nchini Libya bila kupenda. 
 
Joy alifahamu anaenda nchini Ujerumani kukutana na mpenzi wake waliyekutana mtandaoni lakini baada ya kufika Libya akajikuta amepokonywa vitu vyake na kulazimishwa kuingia kwenye ukahaba. 
 
“Sikuweza kurejea nyumbani maana wazazi wangu walitumia zaidi ya dola 3000 kwa ajili ya safari yangu ya kwenda Ulaya wakijua nitarejea na mafaniko na kuikomboa familia yangu kutoka kwenye umasikini, nilisikia aibu, niliona nimeleta aibu kwa familia.” 
 
Mama yake Joy alimtumia fedha na akafanikiwa kukimbia kwenye eneo hilo waliloshikiliwa kwa biashara ya ukahaba na kupanda boti ndogo katika bahari ya Mediterania kwa ajili ya kuanza safari ya kuelekea Ulaya. 
 
Lakini bahati haikuwa upande wake kwa kuwa walikamatwa na kushindwa kusafiri na ndio hapo alipopata msaada wa nguo, viatu na dawa za matibabu kutoka shirika la IOM 

Wanawake na wasichana kugeuzwa kafara za kukomboa familia zao 

Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na IOM wasichana wengi ambao wanakuwa wamekwama kwenda Ulaya na ambao IOM inataka kuwasaidia kurejea nchini mwao wamekuwa wakikataa kuunganishwa na familia zao kwa hofu ya kutengwa na jamii na familia zao kwa kuwa wanahusishwa na kuwa makahaba. 
 
Utafiti huu unadhihirika hata kwa simulizi ya Success ambaye alikataliwa yeye na mtoto wake baada ya kurejea nyumbani kwao. 
 
“Wanawake wanakuwa kama kafara za kukomboa familia zao kutoka kwenye umasikini” anasema Ayo Amen Ediae, afisa wa kukabiliana na biashara haramu katika IOM Benin nakuongeza kuwa  “Wanaporudi mikono mitupu, hiyo tayari ni changamoto kwao kwani jamii na familia inawakataa, wanaambiwa ‘Hapana, unarudi mikono mitupu, utaitunzaje familia?” 

Nikutokana na sababu hiyo ndio maana IOM inatoa mafunzo ya ufundi stadi ya siku 10 kwa wahamiaji waliorejea makwao na pia wanapewa msaada unaozingatia mahitaji yao na ushauri wa kuwafanya waweze kmujumuika vyema kwenye jamii. 
  
“Katika mafunzo tunayotoa , pia tunatoa elimu ya kisaikolojia kwa wote wanaorejea. Elimu ya kisaikolojia inajaribu kuwapa matumaini, kuwahakikishia kuwa wanaweza kurudi nyuma, kuwatayarisha na kujenga kuwa na ustahimilivu,” anaelezea Paradang Gogwim, Msaidizi Mwandamizi wa Mradi wa Msaada wa Afya ya Akili kwa Wahamiaji Waliorudishwa katika IOM Lagos. 
IOM pia huwapatia vitabu ya kuwasaidia katika safari wanapoungana tena katika jumuiya zao. 

Wahamiaji kutoka Nigeria ambao waliokolewa na Walinzi wa Pwani ya Libya wakati mashua yao ilipokuwa ikipinduka, wamejikunyata katika ua katika kituo cha kizuizini, ambako wanazuiliwa, nchini Libya.
© UNICEF/Alessio Romenzi
Wahamiaji kutoka Nigeria ambao waliokolewa na Walinzi wa Pwani ya Libya wakati mashua yao ilipokuwa ikipinduka, wamejikunyata katika ua katika kituo cha kizuizini, ambako wanazuiliwa, nchini Libya.

Sio kila anayerejea kutoka Libya anaishia kuwa kahaba 

Joy alirejea mji wa Benin na kuanza kazi kama fundi cherehani baada ya kumaliza mafunzo ya IOM, ingawa bado analipa deni lake alilokopeswa na familia na watu mbalimbali kabla ya kuondoka, lakini biashara yake inamruhusu kuisaidia kifedha familia yake, kupata chakula yeye na mtoto wake  na kumlipia mtoto wake ada ya shule “ Ninaweza kujisimamia mwenyewe.” Amesema kwa furaha 

Joy ameongeza kuwa ingawa watu wa karibu wanafikiri mara tu unapotoka Libya, jambo la pili unalofanya ni ukahaba, kuishi maisha ya porini lakini hilo sio lililo moyoni mwake. 

“Hapana! Nina kazi yangu. Rafiki yangu ana duka la dawa. Mwingine anafanya kazi katika Benki ndogo ya fedha, sote tunaendelea vizuri. Na hao ni wanawake, si wanaume, hawafanyi ukahaba; wanaendelea vizuri. Kwa hiyo, tunajaribu kuwathibitishia, hata kama unatoka Libya au Mali au popote ulipotoka, unaweza kuwa mtu fulani, na kuwa na manufaa kwa jamii yako.” 

Kwa upande wake Success anakumbuka hali ya kukataliwa na jamii na familia iliyomfanya kutaka kuondoka nchini Nigeria kwenda kuishi nchi nyingine. “IOM waliniambia hapana, waliniambia nisiende, waliniambia hata kama sina pesa, angalau maisha yangu ni muhimu. Kwa vile walinipa duka sasa naweza kumlisha binti yangu, naweza kumvisha, naweza kumlipia ada ya shule, nafanya mambo mengi peke yangu sasa hivi.” 
  
ANGALIZO: Taarifa hii iliandikwa kwa mara ya kwanza kwa lugha ya kiingereza na Alpha Ba and Kim Winkler. Majina yaliyotumika katika makala hii si halisi kwa ajili ya kuwalinda.