Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Guterres aunga mkono maandalizi ya azimio la kupinga vilipuzi

Matumizi ya silaha za vilipulizi huleta madhara kwenye makazi ya raia kama pichani kwenye mji mkuu wa Ukraine, Kyiv ambapo msichana anaonekana akistaajabu shambulizi mbele ya jengo la nyumba, shambulizi lililofanywa na operesheni za kijeshi zinazoendelea.
UNICEF/Anton Skyba for The Globe and Mail
Matumizi ya silaha za vilipulizi huleta madhara kwenye makazi ya raia kama pichani kwenye mji mkuu wa Ukraine, Kyiv ambapo msichana anaonekana akistaajabu shambulizi mbele ya jengo la nyumba, shambulizi lililofanywa na operesheni za kijeshi zinazoendelea.

Guterres aunga mkono maandalizi ya azimio la kupinga vilipuzi

Amani na Usalama

Huko Geneva, Uswisi kuanzia tarehe 6 hadi 8 ya mwezi ujao wa Aprili kunafanyika mashauriano yasiyo rasmi yenye lengo la kuandaa azimio la kisiasa la kulinda raia dhidi ya matumizi ya vilipuzi katika maeneo ya makazi ya watu wengi.

Hatua hiyo imekaribishwa vyema na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kupitia taarifa iliyotolewa na msemaji wake leo Jumatatu jijini New York Marekani.

“Tangu mwaka 2009, Katibu Mkuu mara kwa mara amekuwa akiangazia madhara ya matumizi ya silaha hizo kwenye maeneo yenye raia wengi na kutoa wito kwa pande kinzani kwenye mizozo kuepuka matumizi yake ili wasidhuru raia na miundombinu yao,” imesema taarifa hiyo.

Guterres anasema silaha za vilipuzi zinapotumika kwenye maeneo ya aina hiyo, asilimia 90 ya wanaodhurika ni raia na huwaacha na kiwewe cha muda mrefu hasa kwa wasichana, wavulana na wanawake na wanaume.

Katika maeneo mengi duniani yenye wakazi wengi wamekubwa na madhara kutokana na matumizi ya vilipuzi akisema, “baadhi ya vilipuzi hivyo vilitengenezwa kutumika kwenye viwanja vya wazi vya mapambano. Pindi vinapotumika kwenye maeneo ya raia vinaleta madhara bila kujali ikiwemo, kuharibu hospitali, shule, miradi ya maji, nishati na miundombinu mingine ikiwemo mazingira.

Ni kwa kuzingatia hilo, Katibu Mkuu anakaribisha hatua z anchi kuandaa azimio la kisiasa la kushughulikia suala hilo la kibinadamu sambamba na madhara ya haki za binadamu kutokana na matumizi ya silaha hizo kwenye maeneo yenye raia wengi.

Katibu Mkuu anatoa wito kwa nyaraka hiyo kuwa na maandiko thabiti yanayoelezea ahadi ya kuepuka kutotumia silaha za vilipuzi kwenye maeneo yenye raia kwa sababu ya kutambuliwa kuwa zinaweza kuleta madhara bila kuchagua.

“Katibu Mkuu anaunga mkono maandalizi ya azimio hilo la kisisa, sambamba na kanuni mahusisi za ukomo wa matumizi, será za matumizi yake kulindana na mazingira na kwa mujibu wa sheria za kimataifa za kibinadamu pamoja na sheria kuhusu matumizi ya vilipuzi kwenye maeneo ya raia.