Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baadhi ya wakimbizi wa Ukraine wahamishiwa Romania kupunguza mzigo kwa Moldova

Wanawake wakikimbia na watoto wakiingia Romani katika mpaka wa Siret.
© UNICEF/Alex Nicodim
Wanawake wakikimbia na watoto wakiingia Romani katika mpaka wa Siret.

Baadhi ya wakimbizi wa Ukraine wahamishiwa Romania kupunguza mzigo kwa Moldova

Wahamiaji na Wakimbizi

Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR, mamia ya wakimbizi kutoka Ukraine waliokimbilia Moldova, hasa wazee, familia zenye watoto wadogo na wanawake, wanapewa kipaumbele katika uhamisho wa kwenda nchi ya tatu, Romania kutoka Moldova kwa kuwa Moldova nchi iliyoko kwenye mpaka wa kusini mwa Ukraine ina rasilimali chache za kukabiliana na maelfu ya wakimbizi ambao wamevuka mpaka katika wiki za hivi karibuni.

Ni katika eneo la Palanka nchini Moldova, wakimbizi kutoka Ukraine wako hapa wakisubiri basi ili waelekee nchini Romania. Wanakokotana na mabegi na watoto wao na wengine wamewakumbatia mbwa wao ili kuwakinga na baridi kali katika eneo hili. Mmoja wao hapa ni Yevgeniya, ameshakaa kwenye basi huku akilengwalengwa na machozi anasema, “tulifanya uamuzi wetu wa kuondoka Ukraine haraka sana; tuliweka mizigo yetu haraka sana. Sijui hata kama tulibeba kila kitu.” Richard Schilling, Mwakilishi wa UNHCR katika Ulaya ya Kati, anasema, "Moldova imepokea takribani watu 300,000, wakimbizi kutoka Ukraine, n ahata raia wa nchi nyingine. Hiki ni kiasi kikubwa kwa Moldova; ni karibu sawa na asilimia 10 ya watu wa Moldova. Tunahitaji kusaidia. Kwa sababu hili, watu wanahama, kwenda mahali pengine, hadi Romania.” Uhamisho huu wa wakimbizi wa Ukraine, kuondoka Moldova kuelekea Romania umepangwa kama ishara ya mshikamano na watu wa Moldova na serikali za nchi zote mbili na kwa msaada wa UNHCR na Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji, IOM. UNHCR inasema misafara hii ya magari itaendelea kwa kadri inavyohitaji ili kupunguza msongamano wenye mpaka wa Modova na kuwalinda wanawake, wasichana na watu wengine dhidi ya hatari kama biashara haramu ya binadamu na unyanayasaji wa kijinsia.