Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mahitaji yanaongezeka na rasilimali maji inazidi kuwa adimu, tuchukue hatua sasa:Guterres 

Mtoto akichota maji kutoka kwa bwawa kijiji cha Bhor nchini India wakati wa msimu wa mvua.
Unsplash/Bradford Zak
Mtoto akichota maji kutoka kwa bwawa kijiji cha Bhor nchini India wakati wa msimu wa mvua.

Mahitaji yanaongezeka na rasilimali maji inazidi kuwa adimu, tuchukue hatua sasa:Guterres 

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mastaifa Antonio Guterres ametoa rai kwa dunia kuchukua hatua sasa ili kuilinda na kuienzi rasilimali maji kwa ajili ya kizazi hiki na mustakbali wa kizazi kicjacho wakati huu rasilimali hiyo ikizidi kuwa adimu. 

Kupitia ujumbe wake wa siku ya maji duniani inayoadhimishwa kila mwaka Machi 22 Guterres amesema “Mahitaji ya wanadamu ya maji yanaongezeka. Shinikizo juu ya rasilimali za maji zinaongezeka kutokana na matumizi makubwa, uchafuzi wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi. Ukame na mawimbi ya joto yanazidi kuwa makali na ni mara kwa mara. Kupanda kwa kina cha bahari kunasababisha kuingiliwa kwa maji ya chumvi kwenye chemichemi za pwani na maji ya chini ya ardhi nayo yanapungua.” 

Ameongeza kuwa maji yanaweza kuwa chanzo cha migogoro lakini pia cha ushirikiano.  

Hivyo amesisitiza “Ni muhimu kwamba tufanye kazi pamoja ili kutoa usimamizi bora wa vyanzo vyote vya maji, ikiwa ni pamoja na usambazaji wa maji ya chini ya ardhi duniani. Maji ya ardhini hayaonekani, lakini hatuwezi kumudu kuyasahau. Yakiwa yamehifadhiwa kwenye miamba na udongo, maji ya chini ya ardhi ndio chanzo chetu kikubwa cha maji safi. “ 

Ameongeza kuwa maji hayo ya chini ya radhi ndio yanasimamia usambazaji wa maji ya kunywa, mifumo ya usafi wa mazingira, kilimo, viwanda na mifumo ya ikolojia.  

Hata hivyo, asilimia 20 hivi ya chemichemi za maji duniani zinatumiwa kupita kiasi. 

Hatujui thamani halisi yam aji 

Katibu Mkuu amesema katika maeneo mengi, “hatujui ni kiasi gani cha rasilimali hii ya thamani inaweza kuwepo. Tunahitaji kuboresha uchunguzi wetu, ufuatiliaji na uchanganuzi wa rasilimali za maji chini ya ardhi ili kuzilinda na kuzidhibiti vyema na kusaidia kufikia malengo ya maendeleo endelevu.” 

Amehitimisha kwa kusema kwamba mkutano wa maji wa Umoja wa Mataifa wa mwaka ujao unatoa fursa madhubuti ya kuhimiza hatua za maji kwa maendeleo endelevu.  

Hivyo amehimiza “Katika siku hii ya maji duniani, tujitolee kuimarisha ushirikiano kati ya sekta na kimataifa ili tuweze kuleta uwiano baina ya mahitaji ya watu na asili na kutumia maji ya ardhini kwa vizazi vya sasa na vijavyo.”