Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR inahitaji dola bilioni 1.2 kwa ajili ya kutoa msaada kwa wakimbizi milioni 2.3 

Watu walioyakimbia makazi yao katika eneo la Equatoria Magharibi Sudan Kusini
UNMISS
Watu walioyakimbia makazi yao katika eneo la Equatoria Magharibi Sudan Kusini

UNHCR inahitaji dola bilioni 1.2 kwa ajili ya kutoa msaada kwa wakimbizi milioni 2.3 

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumi wakimbizi, UNHCR limesema mzozo wa Sudan Kusini unasalia kuwa mzozo mkubwa zaidi wa wakimbizi huku asilimia 65 ya wakimbizi wakiwa ni watoto.

UNHCR imesema hayo wakati ikitoa ombi la dola bilioni 1.2 kwa ajili ya kuwasilisha msaada wa kibinadamu na ulinzi kwa wakimbizi milioni 2.3 wa Sudan Kusini na jamii zinazowahifadhi. 

Msaada huo unalenga wakimbizi walioko nchi Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, Ethiopia, Kenya, Sudan na Uganda. 

Katika muongo mmoja wa mzozo, Sudan Kusini inashuhudia ukatili wa mara kwa mara, ukosefu wa uhakika wa chakula na athari kutokana na mafuriko na matukio ya mabadiliko ya tabianchi na kuwalazimu mamilioni ya watu kukimbia makwao kusaka msaada. 

Shirika hilo limesema licha ya kupungua kwa raslimali pamoja na athari za virusi vya Covd-19, nchi zimeendelea kufungua milango yao na kuhifadhi mamilioni ya wakimbizi kutoka Sudan Kusini. 

Ufadhili huo utasaidia DRC, Ethiopia, Kenya, Sudan na Uganda kuimarisha juhudi za ulinzi ili kuwezesha wakimbizi wa Sudan Kusini kufikia huduma za msingi na kuimarisha mnepo wao.  

Sambamba na Mkataba wa Kimataifa wa Wakimbizi, UNHCR na washirika wametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuonyesha mshikamano na uungaji mkono kwa nchi zinazowahifadhi kwa kushughulikia ufadhili duni wa shughuli za kibinadamu na kuunga mkono suluhu.