Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Miradi ya maji yaboresha afya na kilimo nchini Rwanda

Wakulima nchini Rwanda na juhudi za kuimarisha ardhi.
© FAO/Petterik Wiggers
Wakulima nchini Rwanda na juhudi za kuimarisha ardhi.

Miradi ya maji yaboresha afya na kilimo nchini Rwanda

Wanawake

Ikiwa leo ni siku ya maji duniani (22 Machi) nchini Rwanda mradi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kilimo na Chakula FAO wa ujenzi wa mabwawa umebadilisha maisha ya wakulima wa mboga mboga kwa kuwaongezea kipato na pia kuwapatia maji safi na salama. 

Nchini Rwanda katika wilaya Magharibi ya Rulindo kumezungukwa na milima na uoto mzuri wa kijani, wananchi wake wengi wanajishughulisha na kilimo cha mbogamboga na matunda. Lakini kutokana na jiografia ya nchi hiyo kuwa na milima, katika msimu wa kiangazi wakulima inawawia vigumu kupata maji ya kutosha kumwagilia mazao yao na pia kukosa maji safi na salama ya kunywa kutokana na kutegemea chanzo kimoja pekee cha maji kutoka ziwa Yanze.

Ili kuboresha usimamizi wa maji na kuwasaidia wananchi, Shirika la FAO limejenga mabwawa sita ya maji ili kusaidia wakulima wa Yanze kupitia chama chao cha ushirika na sasa wananchi hao wanaweza kulima muda wote kama anavyoeleza mkulima Jean d'Arc Mubaranyang "Hatukai tena bila kufanya kazi wakati wa msimu wa jua, tulikuwa na wasiwasi kuhusu jinsi tunavyoweza kumwagilia. Hakuna tatizo kama hilo sasa, tuna maji na mashine ambayo inatusaidia kusukuma maji moja kwa moja."

FAO pia imetoa msaada wa kuboresha chemchem za maji katika wilaya ya Ngoma kwa kuwajengea mabomba yanayotiririsha maji safi na salama kutoka katika vyanzo vya maji vya ardhini. 

Alphonsine Mukeshimana ni mkulima na mama wa watoto nane anasema hapo awali alisafiri umbali wa saa 3 kwenda kusaka maji ambayo hata hivyo hayakuwa salama kwa afya. “Lakini kwa vile FAO wametupa maji safi, sisi ni wazima, hatuugui magonjwa yanayohusiana na maji machafu kwa sababu sasa tunakunywa maji safi na salama.”

Wanawake nchini Rwanda wanafanya kazi katika shamba kama sehemu ya fedha kwa ajili ya mpango wa kazi.
World Bank/A'Melody Lee
Wanawake nchini Rwanda wanafanya kazi katika shamba kama sehemu ya fedha kwa ajili ya mpango wa kazi.

Gualbert Gbehounou ni mwakilishi wa FAO nchini Rwanda na anasema “Hiki ndicho FAO na Umoja wa Mataifa tunahusika nacho. Tunahakikisha tunaongeza mchango wetu kwa kile kinachoweza kufanya maisha ya wanawake wa vijijini kuwa mazuri na kuibua uwezo wao. Kupata maji kunaondoa kikwazo cha uzalishaji wa kilimo kwa wanawake wa vijijini. Sasa wanaweza kupanda mazao, kufuga mifugo, na hata kuzalisha samaki, bila kujali msimu. Wanazipatia familia zao chakula chenye afya na hata kuboresha mapato yao.”

Kauli mbiu ya Siku ya maji kwa mwaka huu inasema "Maji ya chini ya ardhi, kufanya visivyoonekana kuonekana”.