Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ni wakati wa kuhakikisha usimamizi bora na endelevu wa misitu:Guterres

Nyani katika msitu wa Amazon , Coca
Unsplash/Andres Medina
Nyani katika msitu wa Amazon , Coca

Ni wakati wa kuhakikisha usimamizi bora na endelevu wa misitu:Guterres

Tabianchi na mazingira

Misitu bora ni muhimu kwa ajili ya watu na sayari dunia amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres katika ujumbe wake wa kuadhimisha siku ya kimataifa ya misitu hii leo.  

Ameongeza kuwa misitu “Inafanya kazi kama vichungi vya asili, kutoa hewa safi na maji, na ni maskani ya bayoanuwai .Pia inasaidia kudhibiti hali ya hewa yetu kwa kushawishi mifumo ya mvua, kupoza maeneo ya mijini dhidi ya hali ya joto na kunyonya theluthi moja ya gesi chafuzi,"  

Ameongeza kuwa watu bilioni 1.6 duniani kote wanategemea moja kwa moja misitu kwa chakula, makazi, dawa na mapato hivyo misitu yenye afya ni muhimu kwa watu na sayari. 

Utegemezi wa moja kwa moja 

Siku hii ya kimataifa inayoadhimishwa kila mwaka Machi 21 husisitiza umuhimu wa usimamizi endelevu wa misitu na rasilimali zake ambazo ni muhimu katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuchangia ustawi wa kizazi cha sasa na kijacho. 

Takwimu za Umoja wa Mataifa zinathibitisha kuwa watu bilioni 1.6 wanategemea moja kwa moja misitu kwa kkuweza kuishi.  

Guterres anadokeza kuwa jamii nyingi na watu wa kiasili wananufaika kutokana na riziki na hifadhi zinazotolewa na misitu. 

Licha ya manufaa yote ya misitu, ukataji miti duniani unaendelea kwa kasi ya kutisha: "kila mwaka, hekta milioni 10 za misitu zinaharibiwa", anasema Katibu Mkuu. 

Komesha hulka zisizoendelevu 

Guterres anatoa wito wa kutekelezwa kwa azimio la viongozi la Glasgow kuhusu misitu na ardhi, akisisitiza zaidi kwamba "sasa ni wakati wa hatua za kuaminika na zinazoonekana mashinani". 

Ameongeza kuwa hii ina maana kukomesha mifumo ya matumizi na uzalishaji isiyo endelevu ambayo inatishia misitu huku ikitoa usaidizi kwa usimamizi endelevu katika nchi na kwa watu wanaouhitaji zaidi. 

António Guterres anatoa ombi moja zaidi, ili katika siku ya kimataifa ya misitu, watu warejeree upya "dhamira ya kuhakikisha misitu yenye afya kwa ajili ya maisha yenye afya." 

Siku ya kimataifa ya misitu ilitangazwa na Baraza Kuu mwaka 2012 ili kusherehekea na kuongeza uelewa wa aina zote za misitu.