Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Waandishi wa habari acheni kuchanganya Kiswahili na Kingereza:Mwafisi

Mwanamume aliyevaa suti na mwanamume aliyevaa shati jeupe akiwa ameshika nakala kubwa ya kitabu cha 'Kamusi Kuu ya Kiswahili' katika hafla.
UN/ Stella Vuzo Kamusi ya Kiswahili toleo la 3 ilizinduliwa na Makamu wa Rais wa Tanzania Dr.phillip Mpango kwenye Kongamano la dunia la Kiswahili

Waandishi wa habari acheni kuchanganya Kiswahili na Kingereza:Mwafisi

Utamaduni na Elimu

Waandishi wa habari wamekumbusha kutekeleza jukumu lao la kuzungumza lugha fasaha ya Kiswahili ili wananchi wanao wasikiliza waweze kujifunza kutoka kwao. 

Ushauri huo umetolewa na aliyewahi kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania -TBC Samwillu Mwafisi wakati wa kongamalo la idhaa za Kiswahili duniani lililo malizika leo jijini Arusha nchini Tanzania lililoandaliwa na Baraza la Kiswahili la Taifa-BAKITA. 

Akihojiwa na Stella Vuzo wa kituo cha habari cha Umoja wa Mataifa, Mwafisi amesema hapo awali wahariri ndani ya vyumba vya habari walikuwa hawaruhusu mwandishi wa habari kutamka maneno yasiyo fasaha “Iwapo mwandishi alikuwa akikosea kutamka neno mhariri alimuita na kumrekebisha lakini sasa sioni kama wahariri wananguvu hiyo ya kuwaita waandishi wao wa habari na kuwafundisha sababu wao wenyewe hawatamki Kiswahili fasaha na badala yake wanazungumza Kiswaenglish” amesema Mkurugenzi huyo mstaafu akimaanisha kuchanganya maneno ya Kiswahili na kingereza. 

Akikumbuka wakati akifanya kazi ya uandishi wa habari Mzee Mwafisi amesema “Wakati nafanya kazi redio Tanzania ( Sasa Shirika la Utangazaji Tanzania - TBC) miaka ya 1970 na 1980 tulikuwa haturuhusiwi kabisa kuchanganya maneno ya Kiswahili na kingereza, na ili kuhakikisha tunatumia maneno sahihi kila wakati tulikuwa tunashirikiana na BAKITA kunapoibuka msamiati mpya basi walikuwa wanaletewa vitabu na hivyo tulikuwa tunazungumza kiswahili kama kinavyotakiwa, lakini sasa nikisikiliza waandishi nakasirika kabisa.”

Hadhira ya wanaume na wanawake imeketi katika ukumbi mkubwa wakati wa mkutano kuhusu Kiswahili.
UN/Stella Vuzo Wadau wa Kiswahili wakiwa kwenye kongamano lililoandaliwa na BAKITA jijini Arusha Tanzania

Waandishi wakiri 

Alipoulizwa iwapo tabia hiyo ya kuchangaya lugha inaendelea katika vyombo vya habari, Sophia Kessy mtangazaji wa Clouds Media Group amekiri kuwa ni tabia inayoendelea ndani ya vyumba vya habari. “Mtu anaingia katika kipindi anazungumza neno moja la Kiswahili na kuchanganya na neno la kingereza.”

Amesema Mtangaziji huyo na kuongeza kuwa tabia hiyo si kwa wanahabari pekee “hata katika mitaa mbalimbali tunaona wanafunzi na vijana wengi mtaani wamekuwa wakichanganya maneno mengi ya kiswahili na kingereza na wakati mwingine wanachanganya hata na maneno wasiyo elewa.”

Kessy amesema wakati juhudi zikifanyika za kusambaza Kiswahili barani Afrika na duniani kwa ujumla tabia hii ya wanajamii kuchanganya lugha ni “tatizo kubwa sana wakati huu ambapo tunaitangaza lugha ya Kiswahili duniani hivyo tunapaswa kukaa na kuangalia namna ya kutatua hilo tatizo ili kusaidia jamii ielewe lugha halisi bila ya kuchanganya na lugha nyingine.” 

Naye Maulid Kambaya mtangazaji wa Redio One amesema iwapo waandishi wa habari wanania thabiti ya kuzungumza Kiswahili basi wanaweza kuzungumza “Kwa mfano mimi nina kipindi cha kueneza lugha ya Kiswahili na sipati tabu ya kuzungumza kwakuwa nina chachu ya kuelimisha umma na kila wakati najitahidi kuzungumza lugha fasaha na kuchagua msamiati unaoendana na muktadha sahihi”

Kongamano la Idhaa za Kiswahili lilianza tarehe 14 mpaka 18 mwezi Machi 2022 jijini Arusha nchini Tanzania chini ya kauli mbiu Tasnia ya Habari kwa Maendeleo duniani na limehudhuria na wadau wa idhaa za Kiswahili kutoka zaidi ya nchi 13 duniani pamoja na wadau wengine wa Kiswahili ikiwemo Jeshi la wananchi na mabalozi wa Tanzania katika nchi za nje kwakuwa wamepewa jukumu la kueneza Kiswahili nje ya mipaka ya nchi hiyo.