Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wahamiaji 70 wahofiwa kufa maji pwani ya Libya :IOM

UNHCR na IOM waonya kuhusu kuendelea kuongezeka kwa vifo vya wakimbizi na wahamiaji kwenye bahari ya Meditteranea
© UNHCR/Markel Redondo
UNHCR na IOM waonya kuhusu kuendelea kuongezeka kwa vifo vya wakimbizi na wahamiaji kwenye bahari ya Meditteranea

Wahamiaji 70 wahofiwa kufa maji pwani ya Libya :IOM

Wahamiaji na Wakimbizi

Takriban wahamiaji 70 hawajulikani waliko baharini na wanaohofiwa kufa maji katika ufukwe wa Libya katika muda wa wiki mbili zilizopita, kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji IOM.

Tarehe 12 Machi, boti inayoripotiwa kuwa na wahamiaji 25 ilipinduka karibu na pwani ya Libya ya Tobruk.

Mamlaka ziliokoa wahamiaji sita na kupata miili saba huku watu 12  bado hawajulikani waliko limesema shirika hilo .

Limeongeza kuwa tukio la hivi karibuni linafanya jumla ya idadi ya wahamiaji walioripotiwa kufariki au kupotea katika bahari ya Kati kufikia 215 mwaka huu.

IOM inaendelea kutoa wito wa kuchukuliwa hatua madhubuti  za uokozi ili kupunguza athari za kupotea kwa maisha ya watu wanaosafiri kupitia bahari ya Mediterania pia limechagiza kuwepo na mkakati maalum wa kuruhu watu kuteremka salama kwa mujibu wa sheria za kimataifa.

Wahamiaji katika kituo cha kuzuiliwa cha mji wa Zawiya nchini Libya
Photo: Mathieu Galtier/IRIN
Wahamiaji katika kituo cha kuzuiliwa cha mji wa Zawiya nchini Libya

Akizungumzia matukio hayo Federico Soda, mkuu wa shirika la IOM Libya amesema "Nimeshtushwa na kuendelea kupotea kwa maisha ya watu katika bahari ya Mediterania ya Kati na ukosefu wa hatua za kukabiliana na janga hili linaloendelea. Zaidi ya nusu ya vifo vya mwaka huu vimerekodiwa karibu na pwani ya Libya. Kila ripoti ya wahamiaji waliopotea inawakilisha familia yenye huzuni inayotafuta majibu kuhusu wapendwa wao. Familia zinastahili kujua hatima ya watoto wao, ndugu, wazazi, wapenzi au marafiki zao.”

Ripoti ya ajali ya hivi majuzi ya meli inafuatia ripoti mbaya za tarehe 27 Februari wakati boti ya fiberglass ilipoondoka kwenye bandari ya Sabratah na kupinduka saa nne baadaye kutokana na mawimbi makubwa. Hakuna manusura waliopatikana huku maiti 15, akiwemo mtoto mmoja, zikioshwa ufukweni siku zilizofuata. Takriban wahamiaji 35 bado hawajulikani walipo.

IOM inasisitiza kuwa matukio haya ya kutisha mara nyingi ni matokeo ya kutokuwepo usawa wa upatikanaji wa fursa za uhamaji wa kisheria na salama. Fursa zaidi za uhamiaji salama, wenye utaratibu na wa kawaida zinahitajika haraka, ili watu wasilazimishwe kuhatarisha maisha yao kutafuta usalama na fursa bora.