Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Guterres aomboleza kifo cha Rais wa zamani wa Zambia

Enzi za uhai wake na enzi za Urais, Rupiah Banda akihutubia mkutano wa 64 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa 24/09/2009 jijini New York, Marekani.
UN/Erin Siegal
Enzi za uhai wake na enzi za Urais, Rupiah Banda akihutubia mkutano wa 64 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa 24/09/2009 jijini New York, Marekani.

Guterres aomboleza kifo cha Rais wa zamani wa Zambia

Masuala ya UM

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameeleza masikitiko yake kufuatia kifo cha Rais wa nne wa Zambia, Rupiah Banda. Hayati Banda amekufa akiwa na umri wa miaka 85.

Banda amefariki dunia tarehe 11 mwezi huu wa Machi katika hospitali moja jijini Lusaka, Zambia ambako alikuwa anapatiwa matibabu. Alikuwa na umri wa miaka 85.

Alishika wadhifa wa urais wa Zambia kuanzia mwaka 2008 hadi mwaka 2011 ambapo awali alikuwa Makamu wa Rais chini ya hayati Levy Mwanawasa.

Katika salamu zake za rambirambi alizotoa kupitia taarifa iliyotolewa leo jijini New York, Marekani na msemaji wa Umoja wa Mataifa,  Guterres amesema Hayati Banda alikuwa kiongozi mwenye maono na alikuwa na mchango mkubwa katika amani na umoja wa taifa hilo la Kusini mwa Afrika.

Katibu Mkuu ametuma salamu za rambirambi kwa familia ya Banda, serikali ya Zambia na wananchi wake.

Halikadhalika Guterres amesema, “Umoja wa Mataifa unashikamana na wananchi wa Zambia wakati huu wa maombolezo ya kitaifa.”