Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chonde chonde Uingereza fikirieni upya mswada wa sheria ya uhamiaji:UN

Michelle Bachelet, Kamishna Mkuu wa haki za binadamu.
UN Photo - Jean-Marc Ferre
Michelle Bachelet, Kamishna Mkuu wa haki za binadamu.

Chonde chonde Uingereza fikirieni upya mswada wa sheria ya uhamiaji:UN

Haki za binadamu

Umoja wa Mataifa umeisihi serikali ya Uingereza na watunga sheria kufikiria upya juu ya mswada wa  sheria mpya ya Utaifa na mipaka ya nchi hiyo kwakuwa ikipitishwa kama iliyo itakuwa na athari kubwa kwa wahamiaji na wakimbizi. Flora Nducha ana taarifa zaidi .

Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Kibinadamu Michelle Bachelet ametoa wito huo na kueleza kuwa mswada huo wa sheria mbali na kudhoofisha ulinzi wa haki za binadamu pia unaenda kinyume na sheria za kimataifa za haki za binadamu.

Miongoni mwa vifungu vilivyopo kwenye mswaada huo vinavyoonekana kutofaa ni pamoja na vile vinavyo pendekeza kuwashughulikia wanaotafuta hifadhi kwa njia tofauti kulingana na jinsi walivyofika nchini Uingereza, walipoomba hifadhi, njia waliyotumia katika kusafiri, na uhusiano wao na zile zinazoitwa nchi za tatu salama. 

Pia mswada huo unapendekeza kuharamisha uingiaji nchini humo bila mpangilio pamoja na kurahisisha uhamiaji usio wa kawaida na kuipa mamlaka nguvu ya kuwavua uraia ambao tajari ni raia wa Uingereza bila taarifa. 

Bachelet amesema ndani ya vifungu hivyo pia kuna pendekezo la kuanzishwa kwa vituo vya kuwashughulikia watu wanaoomba hifadhi katika pwani ya nchi hiyo na kwamba baraza la mawaziri limeukataa mswada huo waziwazi na kutaka ufanyiwe marekebisho makubwa. 

Idadi kubwa ya watu wenye asili ya Afrika na wengine wa makabila madogo hufariki dunia katika magereza nchini Uingereza kutokana na matumizi ya nguvu kupita kiasi.
UN
Idadi kubwa ya watu wenye asili ya Afrika na wengine wa makabila madogo hufariki dunia katika magereza nchini Uingereza kutokana na matumizi ya nguvu kupita kiasi.

"Kukataa kwa mawaziri kwa vifungu muhimu vya mswada huo kunapaswa kutuma ishara ya kulazimisha serikali ya Uingereza kwamba inahitaji kufanya marekebisho muhimu. Ninaiomba serikali na wabunge kufanyia kazi ishara hii na kuleta sheria inayopendekezwa kulingana na sheria za kimataifa za haki za binadamu na mkataba wa wakimbizi wa 1951,” amesema Bachelet.

Akizungumzia athari za vifungu vya mswada huo Bachelet ametolea mfano kile cha kuwavua watu uraia akisema
“ Mswada huo kama ulivyotungwa hapo awali ungeruhusu raia wa Uingereza kunyimwa uraia wao wa Uingereza bila taarifa na kwa njia ya kiholela na hivyo kuhatarisha kuongezeka kwa watu wasiokuwa na utaifa.”

Bachelet amesema mswada huo usiporekebishwa “ sheria itakayopatikana itawaadhibu watu wanaoingia Uingereza kwa njia zisizo za kawaida kana kwamba ni wahalifu, kinyume na sheria na viwango vya kimataifa, na kuwatenganisha waomba hifadhi wanaofika Uingereza katika mafungu mawili na kukiuka haki ya kila mtu, zaidi ya hayo, vituo vya wakimbizi vilivyopendekezwa vya pwani vinaweza kuwaweka wanaotafuta hifadhi katika hatari, kutengwa na kunyimwa uhuru vitu ambavyo ni ukiukwaji wa haki zao za kibinadamu na utu.”.