Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Asante IFAD na ROOTS Gambia, sasa niña akiba ya fedha- Amiata

Vijana wa Afrika wako mstari wa mbele katika ujasiriamali kama inavyoonekana pichanihuko Gambia walipotembelewa na mjumbe maalum wa UN kuhusu vijana, Jayathma Wickramanayake (kulia)
Alhagie Manka/ UNFPA Gambia
Vijana wa Afrika wako mstari wa mbele katika ujasiriamali kama inavyoonekana pichanihuko Gambia walipotembelewa na mjumbe maalum wa UN kuhusu vijana, Jayathma Wickramanayake (kulia)

Asante IFAD na ROOTS Gambia, sasa niña akiba ya fedha- Amiata

Wanawake

Nchini Gambia, mradi wa kupatia fedha wakulima vijijini, RPSF unaotekelezwa na mfumo wa Umoja wa Mataifa wa maendeleo ya kilimo, IFAD kwa kushirikiana na shirika la ROOTS Gambia umeleta nuru kwa wakulima vijana ambao janga la ugonjwa wa Corona au COVID-19 siyo tu liliwatumbukiza kwenye umaskini bali pia liliwaondoa kwenye soko na kukosa wateja. 

 

Miongoni mwa wanufaika wa mradi huo ni Amiata Ndongo, mkulima kijana mwenye umri wa miaka 23, mkazi wa mji wa Kuntaur Warf. 

Katika video ya IFAD, Amiata akiwa kwenye konde lake la mpunga anazungumza na simu na mpunga ama hakika umestawi.
Mpunga anaopata anauza kama mpunga au anatwanga na kuuza kama mchele na mafanikio haya anasema ni kutokana na msaada wa mafunzo na fedha kupitia mradi wa RPSF kutoka

IFAD na ROOTS Gambia.

IFAD ilipatia mafunzo vijana 30 wenye kampuni ndogo na za kati kwa lengo la kuwajengea mnepo wa baadaye na pia kukabiliana na athari za janga la coronavirus">COVID-19 kwani wengi walipoteza njia za kujipatia kipato na pia walipoteza soko.

Amiata anasema, “baada ya kurejea kutoka mafunzoni nilianza shamba langu. Nanunua mbegu, nanunua mashine na pia nalipa vibarua. Fedha hizo ni zile nilipatiwa.”

Mabadiliko ya tabianchi ni kikwazo

Hata hivyo mabadiliko ya tabianchi yamekuwa kikwazo kwa wakulima kwa kwa kuwa mvua hazitabiriki tena na kiwango cha joto ni cha juu.

Ingawa hivyo Amiata bado anaweza kunufaika akisema “nalima wakati wa kiangazi na mvua, lakini mavuno ni mengi wakati wa kiangazi kwa kuwa wakati wa mvua mafuriko yanaharibu mazao.”

Wanapataje masoko?

Na ili kuwawezesha kupata masoko ya bidhaa zao, IFAD iliwapatia mafunzo ya kutumia teknolojia kutangaza bidhaa zao kupitia mitandao kama vile TikTok, Whatsapp na Instagram na sasa kuna mabadiliko.

Sasa idadi ya wateja baada ya mafunzo imeongezeka na Amiata anasema anapokea simu kutoka kila eneo la Gambia watu wakitaka mpunga na mchele. Zaidi ya yote, watu wengi wanatambua biashara yake kuliko awali.

Pamoja na kulima na kuuza mpunga na mchele, Amiata ana biashara pia ya mitumba na mradi wa kuku.

Nashukuru IFAD na ROOTS Gambia

Sasa Amiata anatoa shukrani za dhati kwa IFAD na ROOTS Gambia kwa msaada huo kwani umemwezesha kujiendeleza, kutunza familia yake na pia kujipanga. “Mapato ya biashara zangu natumia kiasi na pia ninatunza kwa sababu katika biashara akiba ni muhimu.”