Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kila siku ya vita Ukraine, ni dalili ya kutumbukiza taifa hilo kwenye lindi la umaskini- UNDP

Jengo la makazi lililoharibiwa na operesheni za kijeshi zinazoendelea huko Kyiv, Ukraine, tarehe 26 Februari 2022.
© UNICEF/Kolesnik Evgeniy/UNIAN
Jengo la makazi lililoharibiwa na operesheni za kijeshi zinazoendelea huko Kyiv, Ukraine, tarehe 26 Februari 2022.

Kila siku ya vita Ukraine, ni dalili ya kutumbukiza taifa hilo kwenye lindi la umaskini- UNDP

Msaada wa Kibinadamu

Iwapo vita vitaendelea Ukraine, mafanikio yote ya kiuchumi yaliyopatikana katika kipindi cha miaka 18 yatatoweka, huku theluthi moja ya wananchi wakitumbukia kewnye lindi la umaskini katika miezi 12 ijayo, imesema utafiti mpya uliotolewa leo na shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa maendeleo duniani, UNDP.

Taarifa iliyotolewa leo jijini New York, Marekani inasema kuwa utafiti huo unadokeza kuwa asilimia 90 ya wananchi wa Ukraine wanaweza kukumbw ana umaskini na hali ngumu ya uchumi iwapo vita itaendelea na kurudisha nyuma taifa hilo na ukanda wa Ulaya kwenye hali iliyokabiliana nayo miongo kadhaa iliyopita.

Madhara ya baadaye ni makubwa zaidi, vita ikome sasa

UNDP inasema vita nchini Ukraine inasababisha machungu ya kibinadamu  yasiyopimika na mamilioni ya watu wamefurushwa makwao. Wakati mahitaji ya kibinadamu  yakizidi kuongezeka, madhara yake kwa maendeleo iwapo vita itaendelea muda mrefu yako dhahiri,” amesema Achim Steiner, Mtawala Mkuu wa UNDP.

Amesema kutwama kwa uchumi, na machungu yanayokumba taifa hilo yatatumbukiza zaidi wananchi ambao tayari wamekumbwa na kiwewe, “lakini tuna muda wa kubadili mwelekeo wa janga hili.”

UNDP imekuwa inafanya kazi katika mikoa yote 24 ya Ukraine na hiyo inatokana na udau wake wa kuaminiana na serikali ya Ukraine na sasa inatumia mtandao wake wa kina kwa kusambaza misaada kwa wananchi wa Ukraine ikiwemo ya kibinadamu na kusaidia serikali kutekeleza majukumu yake ya utoaji wa huduma kwa umma.

“Ili kuepusha machungu zaidi, uharibifu na  kutwama katika umaskini, UNDP inahaha kulinda mafanikio yaliyokuwa yamepatiakna. Hi ini Pamoja na kusaidia serikali kuendeleza majukumu yake muhimu kimuundo na kihuduma, vitu ambavyo ni ngome ya jamii yoyote ile,” amesema Steiner.

Makadirio ya serikali ya Ukraine yanaonesha kuwa miundombinu yenye thamani ya takribani dola bilioni 100  yakiwemo majengo, barabara, shule, hospitali, madaraja vimeharibiwa. Vita imesababisha asilimia 50 ya biashara Ukraine kufungwa kabisa huku asiilmia nyingine 50 zikiendeshwa chini ya uwezo wake.

UNDP imesalia Ukraine licha ya mashambulizi

UNDP ni miongoni mwa mashirika makubwa zaidi yaliyosalia Ukraine, na linafanya kazi wakati wote wa vita kwa kupeleka wafanyakazi wake kwenye maeneo maalum kufanya kazi kama vile kuondoa vifusi vya majengo, kutathmini uharibifu na kutoa  misaada ya dharura kama vile fedha kwa wananchi ambao wanahitaji msaada.

Halikadhalika intoa msaada wa maeneo ya wadau wa kibinadamu kuelekeza misaada kwa serikali na wanachi.

UNDP inaungana na mratibu wa UN wa janga la Ukraine kusongesha matumizi ya  huduma za kifedha za kibenki kufikisha misaada ya kifedha ambayo itasaidia kufikia haraka zaidi wananchi wengi nchini humo.

“UNDP inakadiria kuwa fungu kubwa zaidi la mgao wa fedha za dharura utagharimu dola milioni 250 kwa mwezi na litasaidia kuziba kipato kinachotarajiwa kupotezwa na watu milioni 2.6 wanaotarajiwa kutumbukia kwenye umaskini kutokana na ukosefu wa mbinu za kujipatia kipato,” imesema taarifa hiyo.

Halikadhalika mgao wa muda wa dola 5.50 kwa kila mtu utagharimu dola milioni 430 kwa mwezi.

Nchi Jirani hazijasahaulika

UNDP inasema nchi Jirani na Ukraine nazo zimekumbukwa na zinapatiwa usaidizi wa kuzijengea mnepo huku wakimbizi nao wakiangaziwa ili kusongesha maendeleo yao ugenini.’

Hilo linafanyika kwa ushirikiano na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR kupitia mpango wa Pamoja wa mashirika wa kusaidia wakimbizi, Regional Refugee Response Plan.

Raia wa Ukraine wamesaka hifadhi nchi kadhaa ikiwemo Poland, Moldova na Hungary.