Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kukabili kesi za ukatili wa kingono, tunawafundisha wanawake kutunza Ushahidi- Jaji Okwengu

Jaji Hannah Okwengu wa Mahakama ya Rufaa nchini Kenya.
UN Video
Jaji Hannah Okwengu wa Mahakama ya Rufaa nchini Kenya.

Kukabili kesi za ukatili wa kingono, tunawafundisha wanawake kutunza Ushahidi- Jaji Okwengu

Wanawake

Dunia ikiwa inaendelea na shamrashamra za mwezi Machi ambao ni mwezi wa wanawake, nchini Kenya, Jaji wa Mahakama ya Rufaa Hannah Okwengu ametaja mafanikio yaliyopatikana tangu kuanza kwa harakati za kuweka jicho la kijinsia katika mahakama.
 

Jaji Okwengu ametaja mafanikio hayo wakati sehemu ya pili ya mahojiano kwa njia ya mtandao na Assumpta Massoi wa Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa akisema ni pamoja na kufundisha wanawake kutunza Ushahidi pindi wanapokuwa wamekumbwa na ukatili wa kingono.

“Tunawaambia pindi unapopatwa na huo mkasa huo usioge, ili utunze ushahidi, kisha uende polisi na baadaye uende hospitali uonane na daktari,” amesema Jaji Okwengu akiongeza kuwa ni sehemu ya vikao vya watumiaji wa mahakama wakiwemo wanawake na wanaume ambako huwapatia mafunzo ya sheria.

Vipi kwa wanawake wasio na fedha za gharama za kesi?

Mara nyingi wanawake wanakosa uwezo wa kifedha kugharimia kesi, kwa hiyo Chama cha kimataifa cha majaji wanawake, IAWJ, tawi la Kenya  linafanya kazi na makundi mbalimbali wakiwemo mawakili ambao hutoa msaada wa sheria kwa wanawake bila gharama yoyote au Pro bono.

Sasa jamii inaona kuna mafanikio

Kwa mujibu wa Jaji Okwengu, jamii imeona mabadiliko kwa kuwa mafunzo ni kwa wanawake na jamii nzima. Kwenye vikao vya watumiaji wa mahakama kuna wazee wa vijiji na machifu ambako huwaeleza “mama ni mtu anastahili heshima, mtoto wa kike anastahili apelekwe shule asome na hatimaye asaidia wazazi na jamii kwa ujumla.” 

Wanafundishwa pia masuala ya jinsia na sheria ili iwapo ukatili wa kingono ukitokea, basi wao waingilie kati waweze kusaidia kwa njia iliyo nzuri. 

"Tunawaeleza mwanamke akidhulumiwa anaweza kuwa mtoto wako, mke wako au dada yako na kama hatuwezi kufundisha jamii kuheshimu mwanamke au mtoto wa kike basi kila mtu atakuwa hatarini," Jaji Hannah Okwengu- Jaji Mahakama ya Rufaa Kenya

Jami inatanabaishwa kuwa mwanamke akidhulumiwa anaweza kuwa ni mama yake, dada yake au mtoto wake “kwa hiyo usione mtu mwingine anadhulumiwa ukaona si wa kwako, kesho pia mtoto wako, mama yako anaweza kuja nyumbani amedhulumiwa, na kama hatuwezi kufundisha jamii kuheshimu mwanamke au mtoto wa kike, basi kila mtu atakuwa hatarini.”

Ni kipi kimemjenga Jaji Okwengu hadi kufikia Jaji wa Mahakama ya Rufaa

Jaji Okwengu aliingia k taatikansia ya mahakama mwaka 1980 na kilichomwezesha kuingia shuleni msichana mmoja kijijini kwao ambaye alikuwa na bidii na akawa mfano hadi baba yake mzazi akaona lazima na bintiye aweze kusoma masuala ya sheria.

“Hata mimi najaribu kuhimiza wengine kwa kuwa sisi tunawafungulia watu njia kuwa mtu anawezekana kuwa Jaji na kuondoa kizingiti kuwa mwanamke anaweza kufika juu” amesema Jaji Okwengu akiongeza kuwa changamoto ni nyingi lakini “ukiwa na nia na kusudi hakuna unachoshindwa kufanya.”

Ujumbe wake kwa Umoja wa Mataifa?

Ni shukrani za kipekee kwa Umoja wa Mataifa kutenga siku ya kimataifa ya majaji wanawake tarehe 10 Machi 2022 akisema harakati hizo zimekuwa chachu kwa Kenya kufungua Mahakama ya Familia ambayo inahusika na kesi za kifamilia kama vile dhuluma za kijinsia.

Na zaidi ya yote amesisitiza ushirikiano zaidi kati ya IAWJ na Umoja wa Mataifa kwa kuwa Umoja huo ni chombo kinachoweza kutumika kuleta mabadiliko makubwa katika kukabili dhuluma au ukatili wa kijinsia.